1 John (Swahili)
1
1:1b.1JO.001.001 Habari hii ya yahusu Neno la uzima lililokuwako tangu mwanzo. Sisi tumepata kulisikia na kuliona kwa macho yetu wenyewe; tulilitazama na kulishika kwa mikono yetu wenyewe.
1:2b.1JO.001.002 Uzima huo ulipotokea sisi tuliuona na sasa tunasema habari zake na kuwaambieni juu ya uzima huo wa milele uliokuwa kwa Baba na uliodhihirishwa kwetu.
1:3b.1JO.001.003 Tulichokiona na kukisikia ndicho tunachowatangazieni ninyi pia ili nanyi mpate kushirikiana nasi katika umoja tulio nao na Baba na Mwanae Yesu Kristo.
1:4b.1JO.001.004 Tunawaandikia ninyi mambo haya kusudi furaha yetu ikamilike.
1:5b.1JO.001.005 Basi, habari tuliyoisikia kwake Yesu na tunayowahubirieni ndiyo hii: Mungu ni mwanga na hamna giza lolote ndani yake.
1:6b.1JO.001.006 Tukisema kwamba tuna umoja naye, na papo hapo twaishi gizani, tutakuwa tumesema uongo kwa maneno na matendo.
1:7b.1JO.001.007 Lakini tukiishi katika mwanga, kama naye alivyo katika mwanga, basi tutakuwa na umoja sisi kwa sisi, na damu yake Yesu Kristo, Mwanae, inatutakasa dhambi zote.
1:8b.1JO.001.008 Tukisema kwamba hatuna dhambi, tunajidanganya wenyewe na ukweli haumo ndani yetu.
1:9b.1JO.001.009 Lakini tukiziungama dhambi zetu, basi Mungu ni mwaminifu na mwadilifu, naye atatusamehe dhambi zetu na kututakasa na uovu wote.
1:10b.1JO.001.010 Tukisema kwamba hatujatenda dhambi, tutakuwa tumemfanya Mungu mwongo, na neno lake halimo ndani yetu.
2
2:1b.1JO.002.001 Watoto wangu, ninawaandikieni mambo haya, kusudi msitende dhambi. Lakini, ikijatokea mtu akatenda dhambi, tunaye mmoja ambaye hutuombea kwa Baba, ndiye Yesu Kristo aliye mwadilifu kabisa.
2:2b.1JO.002.002 Kristo ndiye sadaka iondoayo dhambi zetu; wala si dhambi zetu sisi tu, bali pia dhambi za ulimwengu wote.
2:3b.1JO.002.003 Tukizitii amri za Mungu, basi, tunaweza kuwa na hakika kwamba tunamjua.
2:4b.1JO.002.004 Mtu akisema kwamba anamjua, lakini hazitii amri zake, basi mtu huyo ni mwongo, na ukweli haumo ndani yake.
2:5b.1JO.002.005 Lakini mtu yeyote anayeshika neno la Mungu, huyo ndiye aliye na upendo kamili wa Mungu ndani yake. Hivi ndivyo tunavyoweza kuwa na hakika kwamba tunaungana naye:
2:6b.1JO.002.006 mtu yeyote anayesema kwamba ameungana na Mungu, anapaswa kuishi kama alivyoishi Yesu Kristo.
2:7b.1JO.002.007 Wapenzi wangu, amri hii ninayowaandikieni si amri mpya; ni amri ileile ya zamani mliyokuwa nayo tangu mwanzo. Amri hiyo ya zamani ni ule ujumbe mliousikia.
2:8b.1JO.002.008 Hata hivyo, amri hii ninayowaandikieni ni amri mpya, na ukweli wake unaonekana ndani ya Kristo na ndani yenu pia. Maana giza linatoweka, na mwanga wa ukweli umekwisha anza kuangaza.
2:9b.1JO.002.009 Yeyote asemaye kwamba yumo katika mwanga, lakini anamchukia ndugu yake, mtu huyo bado yumo gizani.
2:10b.1JO.002.010 Yeyote ampendaye ndugu yake, yuko katika mwanga, na hamna chochote ndani yake kiwezacho kumkwaza mtu mwingine.
2:11b.1JO.002.011 Lakini anayemchukia ndugu yake, yumo gizani; anatembea gizani, na hajui anakokwenda, maana giza limempofusha.
2:12b.1JO.002.012 Ninawaandikieni ninyi watoto, kwa kuwa dhambi zenu zimeondolewa kwa jina la Kristo.
2:13b.1JO.002.013 Nawaandikieni ninyi kina baba kwani mnamjua yeye ambaye amekuwako tangu mwanzo, Nawaandikieni ninyi vijana kwa sababu mmemshinda yule Mwovu.
2:14b.1JO.002.014 Nawaandikieni ninyi watoto, kwa sababu mnamjua Baba. Nawaandikieni ninyi kina baba, kwa kuwa mnamjua yeye ambaye amekuwako tangu mwanzo. Nawaandikieni ninyi vijana kwa sababu mna nguvu; neno la Mungu limo ndani yenu na mmemshinda yule Mwovu.
2:15b.1JO.002.015 Msiupende ulimwengu, wala chochote kilicho cha ulimwengu. Mtu anayeupenda ulimwengu, upendo wa Baba hauwezi kuwamo ndani yake.
2:16b.1JO.002.016 Vitu vyote vya ulimwengu-tamaa mbaya za mwili, vitu wanavyoviona watu na kuvitamani, majivuno yasababishwayo na mali-vyote hivyo havitoki kwa Baba, bali vyatoka kwa ulimwengu.
2:17b.1JO.002.017 Ulimwengu pamoja na vitu vyake vyote vyenye kutamanika unapita; lakini mtu atendaye atakalo Mungu, anaishi milele.
2:18b.1JO.002.018 Watoto, mwisho u karibu! Mlikwisha sikia kwamba adui wa Kristo anakuja, na sasa adui wengi wa Kristo wamekwisha fika, na hivyo twajua kwamba mwisho u karibu.
2:19b.1JO.002.019 Watu hao wametokea kati yetu lakini hawakuwa kweli wa kwetu na ndiyo maana walituacha; Kama wangalikuwa wa kwetu, wangalibaki nasi. Lakini waliondoka, wakaenda zao, kusudi ionekane wazi kwamba hawakuwa kamwe wa kwetu.
2:20b.1JO.002.020 Ninyi, lakini, mlipata kumiminiwa Roho Mtakatifu na Kristo, na hivyo mnaujua ukweli.
2:21b.1JO.002.021 Basi, nawaandikieni, si kwa kuwa hamuujui ukweli, bali kwa sababu mnaujua; na pia mnajua kwamba uongo wowote haupatikani katika ukweli.
2:22b.1JO.002.022 Mwongo ni nani? Ni yule anayekana kwamba Yesu ni Masiha. Mtu wa namna hiyo ni adui wa Kristo--anamkana Baba na Mwana.
2:23b.1JO.002.023 Maana yeyote anayemkana Mwana, anamkana pia Baba; na yeyote anayemkubali Mwana, anampata Baba pia.
2:24b.1JO.002.024 Basi, ujumbe ule mliousikia tangu mwanzo na ukae mioyoni mwenu. Kama ujumbe huo mliousikia tangu mwanzo ukikaa ndani yenu, basi, mtaishi daima katika umoja na Mwana na Baba.
2:25b.1JO.002.025 Na ahadi aliyotuahidia sisi ndiyo hii: uzima wa milele.
2:26b.1JO.002.026 Nimewaandikieni mambo haya kuhusu wale wanaotaka kuwapotosha ninyi.
2:27b.1JO.002.027 Lakini, kwa upande wenu ninyi, Kristo aliwamiminieni Roho wake. Na kama akiendelea kukaa ndani yenu, hamhitaji kufundishwa na mtu yeyote. Maana Roho wake anawafundisheni kila kitu na mafundisho yake ni ya kweli, si ya uongo. Basi shikeni mafundisho ya huyo Roho na kubaki katika muungano na Kristo.
2:28b.1JO.002.028 Naam, watoto, kaeni ndani yake kusudi wakati atakapotokea tuwe hodari bila kuwa na sababu ya kujificha kwa aibu Siku ya kuja kwake.
2:29b.1JO.002.029 Mnajua kwamba Kristo ni mwadilifu kabisa; basi, mnapaswa kujua pia kwamba kila mtu atendaye mambo adili ni mtoto wa Mungu.
3
3:1b.1JO.003.001 Oneni basi, jinsi Baba alivyotupenda mno hata tunaitwa watoto wa Mungu! Na kweli, ndivyo tulivyo. Ndiyo maana ulimwengu haututambui sisi, kwani haumjui Mungu.
3:2b.1JO.003.002 Wapenzi wangu, sisi ni watoto wa Mungu sasa, lakini bado haijaonekana wazi jinsi tutakavyokuwa. Lakini tunajua kwamba wakati Kristo atakapotokea, tutafanana naye kwani tutamwona vile alivyo.
3:3b.1JO.003.003 Basi, kila mtu aliye na tumaini hili katika Kristo, hujiweka safi kama vile Kristo alivyo safi kabisa.
3:4b.1JO.003.004 Kila mtu atendaye dhambi anavunja sheria ya Mungu, maana dhambi ni uvunjaji wa sheria.
3:5b.1JO.003.005 Mnajua kwamba Kristo alikuja kuziondoa dhambi zetu, na kwamba kwake hamna dhambi yoyote.
3:6b.1JO.003.006 Basi, kila aishiye katika muungano na Kristo hatendi dhambi; lakini kila mtu atendaye dhambi hakupata kamwe kumwona, wala kumjua Kristo.
3:7b.1JO.003.007 Basi, watoto wangu, msikubali kupotoshwa na mtu yeyote. Mtu atendaye matendo maadilifu ni mwadilifu kama vile Kristo alivyo mwadilifu kabisa.
3:8b.1JO.003.008 Lakini atendaye dhambi ni wa Ibilisi, maana Ibilisi ametenda dhambi tangu mwanzo. Lakini Mwana wa Mungu alikuja duniani kuiharibu kazi ya Ibilisi.
3:9b.1JO.003.009 Kila aliye mtoto wa Mungu hatendi dhambi, maana anayo hali ya kimungu ndani yake; hawezi kutenda dhambi kwa sababu yeye ni mtoto wa Mungu.
3:10b.1JO.003.010 Lakini yeyote asiyetenda mambo maadilifu, au asiyempenda ndugu yake, huyo si mtoto wa Mungu. Hiyo ndiyo tofauti iliyoko kati ya watoto wa Mungu na watoto wa Ibilisi.
3:11b.1JO.003.011 Na, ujumbe mliousikia tangu mwanzo ndio huu: Tunapaswa kupendana!
3:12b.1JO.003.012 Tusiwe kama Kaini ambaye, kwa kuongozwa na yule Mwovu, alimuua ndugu yake. Na, kwa nini alimuua? Kwa sababu matendo yake yalikuwa maovu, lakini yale ya ndugu yake yalikuwa mema!
3:13b.1JO.003.013 Basi, ndugu zangu, msishangae kama ulimwengu unawachukia ninyi.
3:14b.1JO.003.014 Sisi tunajua kwamba tumekwisha pita kutoka katika kifo na kuingia katika uzima kwa sababu tunawapenda ndugu zetu. Mtu asiye na upendo hubaki katika kifo.
3:15b.1JO.003.015 Kila anayemchukia ndugu yake ni muuaji; nanyi mnajua kwamba muuaji yeyote yule hana uzima wa milele ndani yake.
3:16b.1JO.003.016 Sisi tumepata kujua upendo ni nini, kwani Kristo aliyatoa maisha yake kwa ajili yetu. Nasi vilevile tunapaswa kuyatoa maisha yetu kwa ajili ya ndugu zetu.
3:17b.1JO.003.017 Basi, mtu akiwa na mali za hapa duniani, halafu akamwona ndugu yake ana shida, lakini akawa na moyo mgumu bila kumwonea huruma, anawezaje kusema kwamba anampenda Mungu?
3:18b.1JO.003.018 Watoto wangu, upendo wetu usiwe maneno matupu, bali uwe upendo wa kweli na wa vitendo.
3:19b.1JO.003.019 Hivyo ndivyo tuwezavyo kuwa na hakika kwamba sisi ni watu wa ukweli; na hatutakuwa na wasiwasi mbele ya Mungu.
3:20b.1JO.003.020 Kwa maana, hata kama dhamiri yetu yatuhukumu, twajua kwamba Mungu ni mkuu zaidi kuliko dhamiri, na kwamba yeye ajua kila kitu.
3:21b.1JO.003.021 Wapenzi wangu, kama dhamiri yetu haina lawama juu yetu, basi, twaweza kuwa na uthabiti mbele ya Mungu,
3:22b.1JO.003.022 na twaweza kupokea kwake chochote tunachoomba, maana tunazitii amri zake na kufanya yale yanayompendeza.
3:23b.1JO.003.023 Na, amri yake ndiyo hii: Kumwamini Mwanae Kristo, na kupendana kama alivyotuamuru.
3:24b.1JO.003.024 Anayezitii amri za Mungu anaishi katika muungano na Mungu na Mungu anaishi katika muungano naye. Kwa njia ya Roho ambaye Mungu ametujalia, sisi twajua kwamba Mungu anaishi katika muungano nasi.
4
4:1b.1JO.004.001 Wapenzi wangu, msimsadiki kila mtu asemaye kwamba ana Roho wa Mungu, bali chunguzeni kwa makini kama huyo mtu anaongozwa na Roho wa Mungu au la, Maana manabii wengi wa uongo wamezuka ulimwenguni.
4:2b.1JO.004.002 Hii ndiyo njia ya kujua kama mtu anaongozwa na Roho wa Mungu: Kila anayekiri kwamba Kristo alikuja, akawa binadamu, mtu huyo anaye Roho wa Mungu.
4:3b.1JO.004.003 Lakini mtu yeyote asiyemkiri Kristo hivyo, hana huyo Roho atokaye kwa Mungu. Mtu huyo ana roho ambaye ni wa Adui wa Kristo; nanyi mlikwisha sikia kwamba anakuja, na sasa tayari amekwisha wasili ulimwenguni!
4:4b.1JO.004.004 Lakini ninyi, watoto, ni wake Mungu na mmekwisha washinda hao manabii wa uongo; maana Roho aliye ndani yenu ana nguvu zaidi kuliko roho aliye ndani ya hao walio wa ulimwengu.
4:5b.1JO.004.005 Wao husema mambo ya ulimwengu, nao ulimwengu huwasikiliza kwani wao ni wa ulimwengu.
4:6b.1JO.004.006 Lakini sisi ni wake Mungu. Mtu anayemjua Mungu hutusikiliza, mtu asiye wa Mungu hatusikilizi. Basi, kwa njia hiyo tunaweza kutambua tofauti kati ya Roho wa ukweli na roho wa uongo.
4:7b.1JO.004.007 Wapenzi wangu, tupendane, maana upendo hutoka kwa Mungu. Kila mtu aliye na upendo ni mtoto wa Mungu, na anamjua Mungu.
4:8b.1JO.004.008 Mtu asiye na upendo hamjui Mungu, maana Mungu ni upendo.
4:9b.1JO.004.009 Na Mungu alionyesha upendo wake kwetu kwa kumtuma Mwanae wa pekee ulimwenguni, ili tuwe na uzima kwa njia yake.
4:10b.1JO.004.010 Hivi ndivyo upendo ulivyo: si kwamba sisi tulikuwa tumempenda Mungu kwanza, bali kwamba yeye alitupenda hata akamtuma Mwanae awe sadaka ya kutuondolea dhambi zetu.
4:11b.1JO.004.011 Wapenzi wangu, ikiwa Mungu alitupenda hivyo, basi, nasi tunapaswa kupendana.
4:12b.1JO.004.012 Hakuna mtu aliyekwisha mwona Mungu kamwe; lakini kama tukipendana Mungu anaishi katika muungano nasi, na upendo wake unakamilika ndani yetu.
4:13b.1JO.004.013 Tunajua kwamba tunaishi katika umoja na Mungu, naye Mungu anaishi katika umoja nasi, kwani yeye ametupa Roho wake.
4:14b.1JO.004.014 Sisi tumeona na kuwaambia wengine kwamba Baba alimtuma Mwanae awe Mwokozi wa ulimwengu.
4:15b.1JO.004.015 Kila mtu anayekiri kwamba Yesu ni Mwana wa Mungu, Mungu anaishi katika muungano na mtu huyo, naye anaishi katika muungano na Mungu.
4:16b.1JO.004.016 Basi, sisi tunajua na tunaamini upendo alio nao Mungu kwetu sisi. Mungu ni upendo, na kila mtu aishiye katika upendo, anaishi katika muungano na Mungu, na Mungu anaishi katika muungano naye.
4:17b.1JO.004.017 Upendo umekamilika ndani yetu kusudi tuweze kuwa na ujasiri Siku ile ya Hukumu; kwani maisha yetu hapa duniani ni kama yale ya Kristo.
4:18b.1JO.004.018 Palipo na upendo hapana uoga; naam, upendo kamili hufukuza uoga wote. Basi, mtu mwenye uoga hajakamilika bado katika upendo, kwani uoga huhusikana na adhabu.
4:19b.1JO.004.019 Sisi tuna upendo kwa sababu Mungu alitupenda kwanza.
4:20b.1JO.004.020 Mtu akisema kwamba anampenda Mungu, hali anamchukia ndugu yake, huyo ni mwongo. Maana mtu asiyempenda ndugu yake ambaye anamwona, hawezi kumpenda Mungu ambaye hamwoni.
4:21b.1JO.004.021 Basi, hii ndiyo amri aliyotupa Kristo: Anayempenda Mungu anapaswa pia kumpenda ndugu yake.
5
5:1b.1JO.005.001 Kila mtu anayeamini kwamba Yesu ni Kristo, huyo ni mtoto wa Mungu; na, anayempenda mzazi humpenda pia mtoto wa huyo mzazi.
5:2b.1JO.005.002 Hivi ndivyo tunavyojua kwamba tunawapenda watoto wa Mungu: Kwa kumpenda Mungu na kuzitii amri zake;
5:3b.1JO.005.003 maana kumpenda Mungu ni kuzitii amri zake. Na, amri zake si ngumu,
5:4b.1JO.005.004 maana kila aliye mtoto wa Mungu anaweza kuushinda ulimwengu. Hivi ndivyo tunavyoushinda ulimwengu: kwa imani yetu.
5:5b.1JO.005.005 Nani, basi, awezaye kuushinda ulimwengu? Ni yule anayeamini kwamba Yesu ni Mwana wa Mungu.
5:6b.1JO.005.006 Yesu Kristo ndiye aliyekuja kwa maji ya ubatizo wake na kwa damu ya kifo chake. Hakuja kwa maji tu, bali kwa maji na kwa damu. Naye Roho anashuhudia kwamba ni kweli, kwani Roho ni ukweli.
5:7b.1JO.005.007 Basi, wako mashahidi watatu:
5:8b.1JO.005.008 Roho, maji na damu; na ushahidi wa hawa watatu waafikiana.
5:9b.1JO.005.009 Ikiwa twaukubali ushahidi wa binadamu, ushahidi wa Mungu una uzito zaidi; na huu ndio ushahidi alioutoa Mungu mwenyewe juu ya Mwanae.
5:10b.1JO.005.010 Anayemwamini mwana wa Mungu anao ushahidi huo ndani yake; lakini asiyemwamini Mungu, anamfanya yeye kuwa mwongo, maana hakuamini ushahidi alioutoa Mungu juu ya Mwanae.
5:11b.1JO.005.011 Na, ushahidi wenyewe ndio huu: Mungu alitupatia uzima wa milele, na uzima huo uko kwa Bwana.
5:12b.1JO.005.012 Yeyote, aliye na Mwana wa Mungu anao uzima huo; asiye na Mwana wa Mungu, hana uzima.
5:13b.1JO.005.013 Nawaandikieni mpate kujua kwamba mnao uzima wa milele ninyi mnaoamini kwa jina la Mwana wa Mungu.
5:14b.1JO.005.014 Na sisi tuko thabiti mbele ya Mungu kwani tuna hakika kwamba tukimwomba chochote kadiri ya mapenzi yake, yeye hutusikiliza.
5:15b.1JO.005.015 Yeye hutusikiliza kila tunapomwomba; na kwa vile tunajua kwamba yeye hutusikiliza kila tunapomwomba, twajua pia kwamba atupatia yote tunayomwomba.
5:16b.1JO.005.016 Mtu akimwona ndugu yake ametenda dhambi isiyompeleka kwenye kifo anapaswa kumwombea kwa Mungu, naye Mungu atampatia uzima. Nasema jambo hili kuhusu wale waliotenda dhambi ambazo si za kifo. Lakini ipo dhambi yenye kumpeleka mtu kwenye kifo nami sisemi kwamba mnapaswa kumwomba Mungu kwa ajili ya hiyo.
5:17b.1JO.005.017 Kila tendo lisilo adilifu ni dhambi, lakini kuna dhambi isiyompeleka mtu kwenye kifo.
5:18b.1JO.005.018 Tunajua kwamba kila aliye mtoto wa Mungu hatendi dhambi, kwa sababu Mwana wa Mungu humlinda salama, na yule Mwovu hawezi kumdhuru.
5:19b.1JO.005.019 Tunajua kwamba sisi ni wake Mungu ingawa ulimwengu wote unatawaliwa na yule Mwovu.
5:20b.1JO.005.020 Twajua pia kwamba Mwana wa Mungu amekuja, akatupa elimu ili tumjue Mungu wa kweli; tuishi katika muungano na Mungu wa kweli--katika muungano na Mwanae, Yesu Kristo. Huyu ndiye Mungu wa kweli, na huu ndio uzima wa milele.
5:21b.1JO.005.021 Watoto wangu, epukaneni na sanamu za miungu.
- Holder of rights
- Multilingual Bible Corpus
- Citation Suggestion for this Object
- TextGrid Repository (2025). Swahili Collection. 1 John (Swahili). 1 John (Swahili). Multilingual Parallel Bible Corpus. Multilingual Bible Corpus. https://hdl.handle.net/21.11113/0000-0016-B9B1-F