James (Swahili)

James (Swahili)

1

1:1b.JAM.001.001 Mimi Yakobo, mtumishi wa Mungu na wa Bwana Yesu Kristo, nawaandikia ninyi, makabila kumi na mawili, yaliyotawanyika ulimwenguni! Salaam!

1:2b.JAM.001.002 Ndugu zangu, muwe na furaha mnapopatwa na majaribu mbalimbali,

1:3b.JAM.001.003 kwani mwajua kwamba imani yenu ikisha stahimili, itawapatieni uvumilivu.

1:4b.JAM.001.004 Muwe na hakika kwamba uvumilivu wenu utawategemeza mpaka mwisho, mpate kuwa wakamilifu na watimilifu, bila kupungukiwa chochote.

1:5b.JAM.001.005 Lakini kama mmoja wenu ametindikiwa hekima, basi, anapaswa kumwomba Mungu ambaye atampatia; kwani Mungu huwapa wote kwa wingi na kwa ukarimu.

1:6b.JAM.001.006 Lakini anapaswa kuomba kwa imani bila mashaka yoyote. Mtu aliye na mashaka ni kama mawimbi ya bahari ambayo husukumwa na kutupwatupwa na upepo.

1:7b.JAM.001.007 Mtu wa namna hiyo, mwenye nia mbili na asiye na msimamo katika mwenendo wake wote,

1:8b.JAM.001.008 asidhani ya kwamba atapata chochote kile kutoka kwa Bwana.

1:9b.JAM.001.009 Ndugu aliye maskini anapaswa kufurahi wakati Mungu anapomkweza,

1:10b.JAM.001.010 naye tajiri anapaswa kufurahi anaposhushwa na Mungu. Maana tajiri atatoweka kama ua la porini.

1:11b.JAM.001.011 Jua huchomoza na kwa joto lake kali hukausha mimea, nayo maua yake huanguka, na uzuri wake wote huharibika. Vivyo hivyo, tajiri ataangamizwa katika shughuli zake.

1:12b.JAM.001.012 Heri mtu anayebaki mwaminifu katika majaribu, kwani akisha stahimili atapewa tuzo la uzima ambalo Mungu aliwaahidia wale wanaompenda.

1:13b.JAM.001.013 Kama mtu akijaribiwa, asiseme: "Ninajaribiwa na Mungu." Maana Mungu hawezi kujaribiwa na uovu, wala yeye hamjaribu mtu yeyote.

1:14b.JAM.001.014 Lakini mtu hujaribiwa anapovutwa na kunaswa na tamaa zake mbaya.

1:15b.JAM.001.015 Tamaa ikiiva huzaa dhambi; nayo dhambi ikikomaa huzaa kifo.

1:16b.JAM.001.016 Ndugu zangu wapenzi, msidanganyike!

1:17b.JAM.001.017 Kila kipaji chema na kila zawadi kamilifu hutoka mbinguni; hutoka kwa Baba, Muumba wa mianga, ambaye habadiliki wala hana alama yoyote ya ugeugeu.

1:18b.JAM.001.018 Kwa kupenda kwake mwenyewe alituzaa kwa neno lake la ukweli, ili tuwe namna ya matunda ya kwanza miongoni mwa viumbe vyake.

1:19b.JAM.001.019 Ndugu zangu wapenzi, kumbukeni jambo hili! Kila mtu na awe mwepesi wa kusikia lakini asiwe mwepesi wa kusema wala mwepesi wa kukasirika.

1:20b.JAM.001.020 Mwenye hasira hawezi kutimiza matakwa ya Mungu yaliyo ya haki.

1:21b.JAM.001.021 Kwa hiyo, tupilieni mbali mwenendo mchafu na tabia zote mbovu; jiwekeni chini ya Mungu na kupokea ule ujumbe uliopandwa mioyoni mwenu, ambao waweza kuziokoa nafsi zenu.

1:22b.JAM.001.022 Msijidanganye wenyewe kwa kusikiliza tu neno lake, bali litekelezeni kwa vitendo.

1:23b.JAM.001.023 Yeyote anayesikiliza hilo neno lakini halitekelezi, huyo ni kama mtu anayejiangalia sura yake mwenyewe katika kioo.

1:24b.JAM.001.024 Hujiangalia mwenyewe, kisha huenda zake, na mara husahau jinsi alivyo.

1:25b.JAM.001.025 Lakini mtu anayeangalia kwa makini sheria kamilifu ambayo huwapa watu uhuru, mtu anayeendelea kuizingatia, na si kuisikia tu na kuisahau baadaye, bali anaitekeleza, mtu huyo atabarikiwa katika kila kitu anachofanya.

1:26b.JAM.001.026 Kama mtu akijiona kuwa ni mtu mwenye dini, lakini hawezi kuutawala ulimi wake, dini yake haifai kitu, na anajidanganya mwenyewe.

1:27b.JAM.001.027 Dini iliyo safi na isiyo na hitilafu mbele ya Mungu Baba ni hii: Kuwasaidia yatima na wajane katika shida zao, na kujilinda mwenyewe usichafuliwe na ulimwengu huu.

2

2:1b.JAM.002.001 Ndugu zangu, mkiwa mnamwamini Bwana Yesu Kristo, Bwana wa utukufu, msiwabague watu kamwe.

2:2b.JAM.002.002 Tuseme mtu mmoja ambaye amevaa pete ya dhahabu na mavazi nadhifu anaingia katika mkutano wenu, na papo hapo akaingia mtu maskini aliyevaa mavazi machafu.

2:3b.JAM.002.003 Ikiwa mtamstahi zaidi yule aliyevaa mavazi ya kuvutia na kumwambia: "Keti hapa mahali pazuri," na kumwambia yule maskini: "Wewe, simama huko," au "Keti hapa sakafuni miguuni pangu,"

2:4b.JAM.002.004 je, huo si ubaguzi kati yenu? Je, na huo uamuzi wenu haujatokana na fikira mbaya?

2:5b.JAM.002.005 Ndugu zangu wapenzi, sikilizeni! Mungu amechagua watu ambao ni maskini katika ulimwengu huu ili wapate kuwa matajiri katika imani na kupokea Utawala aliowaahidia wale wanaompenda.

2:6b.JAM.002.006 Lakini ninyi mnawadharau watu maskini! Je, matajiri si ndio wanaowakandamizeni na kuwapeleka mahakamani?

2:7b.JAM.002.007 Je, si haohao wanaolitukana hilo jina lenu zuri mlilopewa?

2:8b.JAM.002.008 Kama mnaitimiza ile sheria ya Utawala kama ilivyoandikwa katika Maandiko Matakatifu: "Mpende binadamu mwenzako kama unavyojipenda wewe mwenyewe", mtakuwa mnafanya vema kabisa.

2:9b.JAM.002.009 Lakini mkiwabagua watu, basi, mwatenda dhambi, nayo Sheria inawahukumu ninyi kuwa mna hatia.

2:10b.JAM.002.010 Anayevunja amri mojawapo ya Sheria, atakuwa na hatia ya kuivunja Sheria yote.

2:11b.JAM.002.011 Maana yuleyule aliyesema: "Usizini," alisema pia "Usiue". Kwa hiyo, hata ikiwa hukuzini lakini umeua, wewe umeivunja Sheria.

2:12b.JAM.002.012 Basi, semeni na kutenda kama watu watakaohukumiwa kwa sheria iletayo uhuru.

2:13b.JAM.002.013 Maana, Mungu hatakuwa na huruma atakapomhukumu mtu asiyekuwa na huruma. Lakini huruma hushinda hukumu.

2:14b.JAM.002.014 Ndugu zangu, kuna faida gani mtu kusema ana imani, lakini haonyeshi kwa vitendo? Je, hiyo imani yawezaje kumwokoa?

2:15b.JAM.002.015 Tuseme kaka au dada hana nguo au chakula.

2:16b.JAM.002.016 Yafaa kitu gani ninyi kuwaambia hao: "Nendeni salama mkaote moto na kushiba," bila kuwapatia mahitaji yao ya maisha?

2:17b.JAM.002.017 Vivyo hivyo, imani peke yake bila matendo imekufa.

2:18b.JAM.002.018 Lakini mtu anaweza kusema: "Wewe unayo imani, mimi ninayo matendo!" Haya! Nionyeshe jinsi mtu anavyoweza kuwa na imani bila matendo, nami nitakuonyesha imani yangu kwa matendo yangu.

2:19b.JAM.002.019 Je, wewe unaamini kwamba yuko Mungu mmoja? Sawa! Lakini hata pepo huamini hilo, na hutetemeka kwa hofu.

2:20b.JAM.002.020 Mpumbavu wee! Je, wataka kuonyeshwa kwamba imani bila matendo imekufa?

2:21b.JAM.002.021 Je, Abrahamu baba yetu alipataje kukubalika mbele yake Mungu? Kwa matendo yake, wakati alipomtoa mwanae Isaka sadaka juu ya madhabahu.

2:22b.JAM.002.022 Waona basi, kwamba imani yake iliandamana na matendo yake; imani yake ilikamilishwa kwa matendo yake.

2:23b.JAM.002.023 Hivyo yakatimia yale Maandiko Matakatifu yasemayo: "Abrahamu alimwamini Mungu na kwa imani yake akakubaliwa kuwa mtu mwadilifu; na hivyo Abrahamu akaitwa rafiki wa Mungu."

2:24b.JAM.002.024 Mnaona basi, kwamba mtu hukubaliwa kuwa mwadilifu kwa matendo yake na si kwa imani peke yake.

2:25b.JAM.002.025 Ilikuwa vivyo hivyo kuhusu yule malaya Rahabu; yeye alikubaliwa kuwa mwadilifu kwa sababu aliwapokea wale wapelelezi na kuwasaidia waende zao kwa kupitia njia nyingine.

2:26b.JAM.002.026 Basi, kama vile mwili bila roho umekufa, vivyo hivyo imani bila matendo imekufa.

3

3:1b.JAM.003.001 Ndugu zangu, wengi wenu msiwe walimu. Kama mjuavyo, sisi walimu tutapata hukumu kubwa zaidi kuliko wengine.

3:2b.JAM.003.002 Lakini kama mtu hakosi katika usemi wake, basi, huyo ni mkamilifu, na anaweza kutawala nafsi yake yote.

3:3b.JAM.003.003 Sisi huwatia farasi lijamu kinywani mwao ili watutii; na kwa njia hiyo twaweza kuwaongoza kokote tunakotaka.

3:4b.JAM.003.004 Meli nazo pia, ingawa ni kubwa sana, na husukumwa na upepo mkali, huweza kugeuzwa kwa usukani mdogo sana, zikaelekea kokote nahodha anakotaka.

3:5b.JAM.003.005 Vivyo hivyo, ulimi, ingawa ni kiungo kidogo cha mwili, hujisifia makuu sana. Moto mdogo waweza kuteketeza msitu mkubwa.

3:6b.JAM.003.006 Hali kadhalika ulimi ni kama moto. Umejaa maovu chungu nzima, unayo nafasi yake katika miili yetu na hueneza ubaya katika nafsi zetu zote. Huteketeza maisha yetu yote kwa moto utokao Jehanamu kwenyewe.

3:7b.JAM.003.007 Binadamu anaweza kuwafuga wanyama, na amefaulu kufuga viumbe vyote--wanyama wa mwituni, ndege, nyoka na viumbe vya baharini.

3:8b.JAM.003.008 Lakini hakuna mtu aliyeweza kuufuga ulimi. Ulimi ni kitu kiovu, hakitawaliki, na kimejaa sumu inayoua.

3:9b.JAM.003.009 Kwa ulimi sisi twamshukuru Bwana na Baba yetu. Kwa ulimi huohuo twawalaani watu, watu ambao wameumbwa kwa mfano wa Mungu.

3:10b.JAM.003.010 Maneno ya laana na ya kusifia hutoka katika kinywa kimoja. Ndugu zangu, mambo haya hayapaswi kuwa hivyo.

3:11b.JAM.003.011 Je, chemchemi moja yaweza kutoa maji matamu na maji machungu pamoja?

3:12b.JAM.003.012 Ndugu zangu, je, mti wa mtini waweza kuzaa zeituni? Au, mzabibu waweza kuzaa tini? Chemchemi ya maji ya chumvi haiwezi kutoa maji matamu.

3:13b.JAM.003.013 Je, ni nani mwenye hekima na akili miongoni mwenu? Basi, aonyeshe jambo hilo kwa mwenendo wake mzuri na kwa matendo yake mema yanayofanyika kwa unyenyekevu na hekima.

3:14b.JAM.003.014 Lakini ikiwa mioyo yenu imejaa wivu, chuki na ubinafsi, basi, msijisifu na kusema uongo dhidi ya ukweli.

3:15b.JAM.003.015 Hekima ya namna hiyo haitoki juu mbinguni; hekima hiyo ni ya ulimwengu, na ya kidunia, tena ni ya kishetani.

3:16b.JAM.003.016 Maana popote palipo na wivu na ubinafsi hapo pana fujo na kila aina ya uovu.

3:17b.JAM.003.017 Lakini hekima itokayo juu mbinguni, kwanza ni safi; inapenda amani, upole na huwajali watu; imejaa huruma na huzaa matunda ya matendo mema; haina ubaguzi wala unafiki.

3:18b.JAM.003.018 Uadilifu ni mazao ya mbegu ambazo wapenda amani hupanda katika amani.

4

4:1b.JAM.004.001 Mapigano na magombano yote kati yenu yanatoka wapi? Hutoka katika tamaa zenu mbaya ambazo hupigana daima ndani yenu.

4:2b.JAM.004.002 Mnatamani vitu na kwa vile hamvipati mko tayari kuua; mwatamani sana kupata vitu, lakini hamvipati, hivyo mnagombana na kupigana. Hampati kile mnachotaka kwa sababu hamkiombi kwa Mungu.

4:3b.JAM.004.003 Tena, mnapoomba hampati kwa sababu mnaomba kwa nia mbaya; mnaomba ili mpate kutosheleza tamaa zenu.

4:4b.JAM.004.004 Ninyi ni watu msio na uaminifu kama wazinzi. Je, hamjui kwamba kuwa rafiki wa ulimwengu ni kuwa adui wa Mungu? Yeyote anayetaka kuwa rafiki wa ulimwengu anajifanya adui wa Mungu.

4:5b.JAM.004.005 Msifikiri kwamba Maandiko Matakatifu yamesema maneno ya bure, yanaposema: "Roho ambaye Mungu amemweka ndani yetu ana wivu mkubwa."

4:6b.JAM.004.006 Lakini, neema tunayopewa na Mungu ina nguvu zaidi; kama yasemavyo Maandiko: "Mungu huwapinga wenye majivuno lakini huwapa neema wanyenyekevu."

4:7b.JAM.004.007 Basi, jiwekeni chini ya Mungu; mpingeni Ibilisi naye atawakimbieni.

4:8b.JAM.004.008 Mkaribieni Mungu, naye atakuja karibu nanyi. Osheni mikono yenu enyi wakosefu! Safisheni mioyo yenu enyi wanafiki!

4:9b.JAM.004.009 Oneni huzuni, lieni na kuomboleza; kicheko chenu na kiwe kilio; na furaha yenu iwe huzuni kubwa.

4:10b.JAM.004.010 Nyenyekeeni mbele ya Bwana, naye atawainueni.

4:11b.JAM.004.011 Ndugu, msilaumiane ninyi kwa ninyi. Anayemlaumu ndugu yake na kumhukumu, huyo huilaumu na kuihukumu Sheria. Kama ukiihukumu Sheria, basi, wewe huitii Sheria, bali waihukumu.

4:12b.JAM.004.012 Mungu peke yake ndiye mwenye kuweka Sheria na kuhukumu. Ni yeye peke yake anayeweza kuokoa na kuangamiza. Basi, wewe ni nani hata umhukumu binadamu mwenzako?

4:13b.JAM.004.013 Basi, sasa sikilizeni ninyi mnaosema: "Leo au kesho tutakwenda katika mji fulani na kukaa huko mwaka mzima tukifanya biashara na kupata faida."

4:14b.JAM.004.014 Ninyi hamjui hata maisha yenu yatakavyokuwa kesho! Ninyi ni kama ukungu unaotokea kwa muda mfupi tu na kutoweka tena.

4:15b.JAM.004.015 Mngalipaswa kusema: "Bwana akitujalia tutaishi na tutafanya hiki au kile."

4:16b.JAM.004.016 Lakini sasa mwajivuna na kujigamba; majivuno ya namna hiyo ni mabaya.

4:17b.JAM.004.017 Basi, mtu ambaye hafanyi lile jambo jema analojua kwamba anapaswa kulifanya, anatenda dhambi.

5

5:1b.JAM.005.001 Na sasa sikilizeni enyi matajiri! Lieni na kuomboleza kwa sababu ya taabu zitakazowajieni.

5:2b.JAM.005.002 Mali zenu zimeoza, na nguo zenu zimeliwa na nondo.

5:3b.JAM.005.003 Dhahabu yenu na fedha vimeota kutu, na kutu hiyo itakuwa ushahidi dhidi yenu, nayo itakula miili yenu kama vile moto. Ninyi mmejilundikia mali katika siku hizi za mwisho!

5:4b.JAM.005.004 Hamkuwalipa mishahara watumishi waliofanya kazi katika mashamba yenu. Sikilizeni malalamiko yao! Kilio cha hao wanaovuna mashamba yenu kimefika masikioni mwa Bwana, Mwenye Nguvu.

5:5b.JAM.005.005 Mmeishi duniani maisha ya kujifurahisha na ya anasa. Mmejinenepesha tayari kwa siku ya kuchinjwa.

5:6b.JAM.005.006 Mmemhukumu na kumwua mtu asiye na hatia, naye hakuwapigeni.

5:7b.JAM.005.007 Basi, ndugu zangu, muwe na subira mpaka Bwana atakapokuja. Tazameni mkulima anavyongoja kwa subira mimea yake itoe mavuno mazuri. Yeye hungojea kwa subira mvua za masika na za vuli.

5:8b.JAM.005.008 Nanyi pia mnapaswa kuwa na subira; imarisheni mioyo yenu, maana siku ya kuja kwake Bwana inakaribia.

5:9b.JAM.005.009 Ndugu zangu, msinung'unikiane ninyi kwa ninyi msije mkahukumiwa na Mungu. Hakimu yu karibu, tayari kuingia.

5:10b.JAM.005.010 Ndugu, mkitaka kuona mfano wa subira na uvumilivu katika mateso, fikirini juu ya manabii ambao walinena kwa jina la Bwana.

5:11b.JAM.005.011 Tunawaita hao wenye heri kwa sababu walivumilia. Mmesikia habari za uvumilivu wa Yobu, na mnajua jinsi Bwana alivyomtendea mwishoni. Maana Bwana amejaa huruma na rehema.

5:12b.JAM.005.012 Zaidi ya hayo yote, ndugu zangu, msiape kwa mbingu, wala kwa dunia, wala kwa kitu kingine chochote. Semeni "Ndiyo" kama maana yenu ni ndiyo, na "La" kama maana yenu ni la, na hapo hamtahukumiwa na Mungu.

5:13b.JAM.005.013 Je, pana mtu yeyote miongoni mwenu aliye na shida? Anapaswa kusali. Je, yuko mwenye furaha? Anapaswa kuimba nyimbo za sifa.

5:14b.JAM.005.014 Je, yuko mgonjwa kati yenu? Anapaswa kuwaita wazee wa kanisa, nao watamwombea na kumpaka mafuta kwa jina la Bwana.

5:15b.JAM.005.015 Wakiomba kwa imani mgonjwa ataponyeshwa; Bwana atampatia nafuu, na dhambi alizotenda zitaondolewa.

5:16b.JAM.005.016 Basi, ungamanianeni dhambi zenu, na ombeaneni, ili mpate kuponywa. Sala ya mtu mwema ina nguvu ya kutenda mengi.

5:17b.JAM.005.017 Eliya alikuwa binadamu kama sisi. Aliomba kwa moyo mvua isinyeshe, nayo haikunyesha nchini kwa muda wa miaka mitatu na miezi sita.

5:18b.JAM.005.018 Kisha akaomba tena, mvua ikanyesha kutoka angani na nchi ikatoa mazao yake.

5:19b.JAM.005.019 Ndugu zangu, mmoja wenu akipotoka kuhusu ukweli, na mwingine akamrudisha,

5:20b.JAM.005.020 fahamuni kwamba, huyo anayemrudisha mwenye dhambi kutoka njia yake ya upotovu, ataiokoa roho yake kutoka kifo, na dhambi nyingi zitaondolewa.


Holder of rights
Multilingual Bible Corpus

Citation Suggestion for this Object
TextGrid Repository (2025). Swahili Collection. James (Swahili). James (Swahili). Multilingual Parallel Bible Corpus. Multilingual Bible Corpus. https://hdl.handle.net/21.11113/0000-0016-B9A8-A