2 Thessalonians (Swahili)

2 Thessalonians (Swahili)

1

1:1b.2TH.001.001 Mimi Paulo, Silwano na Timotheo tunawaandikia ninyi jumuiya ya kanisa la Thesalonike, ambao ni watu wake Mungu Baba yetu na wa Bwana Yesu Kristo.

1:2b.2TH.001.002 Tunawatakieni neema na amani kutoka kwa Mungu Baba yetu na kwa Bwana Yesu Kristo.

1:3b.2TH.001.003 Ndugu, tunapaswa kushukuru Mungu daima kwa ajili yenu. Inafaa kwetu kufanya hivyo kwani imani yenu inakua sana na kupendana kwenu kunaongezeka sana.

1:4b.2TH.001.004 Ndio maana sisi tunajivunia ninyi katika makanisa ya Mungu. Tunaona fahari juu ya jinsi mnavyoendelea kuamini na kustahimili katika udhalimu wote na mateso mnayopata.

1:5b.2TH.001.005 Hayo yote yanathibitisha kwamba hukumu ya Mungu ni ya haki, na matokeo yake ninyi mtastahili Utawala wake ambao kwa ajili yake mnateseka.

1:6b.2TH.001.006 Mungu atafanya jambo la haki: atawalipa mateso wale wanaowatesa ninyi,

1:7b.2TH.001.007 na kuwapeni nafuu ninyi mnaoteseka, na sisi pia. Atafanya jambo hilo wakati Bwana atakapotokea kutoka mbinguni pamoja na malaika wake na wakuu

1:8b.2TH.001.008 na miali ya moto, kuwaadhibu wale wanaomkataa Mungu na wale wasiotii Habari Njema ya Bwana wetu Yesu.

1:9b.2TH.001.009 Adhabu yao itakuwa kuangamizwa milele na kutengwa mbali na utukufu wake mkuu,

1:10b.2TH.001.010 wakati atakapokuja Siku ile kupokea utukufu kutoka kwa watu wake na heshima kutoka kwa wote wanaoamini. Ninyi pia mtakuwa miongoni mwao, kwani mmeuamini ule ujumbe tuliowaletea.

1:11b.2TH.001.011 Ndiyo maana tunawaombeeni daima. Tunamwomba Mungu wetu awawezeshe muyastahili maisha aliyowaitia myaishi. Tunamwomba, kwa uwezo wake, atimize nia yenu ya kutenda mema na kukamilisha kazi yenu ya imani.

1:12b.2TH.001.012 Kwa namna hiyo, jina la Bwana wetu Yesu litapata utukufu kutoka kwenu, nanyi mtapata utukufu kutoka kwake kwa neema ya Mungu wetu na ya Bwana Yesu Kristo.

2

2:1b.2TH.002.001 Sasa yahusu kuja kwake Bwana wetu Yesu Kristo na kukusanywa kwetu pamoja tukae naye. Ndugu, tunawaombeni sana

2:2b.2TH.002.002 msifadhaike upesi moyoni, na wala msitiwe wasiwasi kwa sababu ya madai kwamba Siku ya Bwana imekwisha fika. Labda inadhaniwa kwamba jambo hili limetokana na uaguzi fulani, mahubiri au barua inayosemekana kuwa imetoka kwetu.

2:3b.2TH.002.003 Msikubali kudanganywa na mtu yeyote kwa namna yoyote ile. Maana Siku hiyo haitakuja mpaka kwanza ule Uasi Mkuu utokee na yule Mwovu aonekane ambaye mwisho wake ni kuangamizwa kabisa.

2:4b.2TH.002.004 Yeye atapinga kila kitu wanachokiona watu kuwa ni mungu, au wanachokiabudu. Naam, hata ataingia na kuketi ndani ya Hekalu la Mungu akijidai kuwa Mungu.

2:5b.2TH.002.005 Je, hamkumbuki kwamba niliwaambieni haya yote wakati nilipokuwa pamoja nanyi?

2:6b.2TH.002.006 Lakini kuna kitu kinachomzuia sasa, nanyi mwakijua kitu hicho. Basi, huyo Mwovu ataonekana wakati wake ufaao.

2:7b.2TH.002.007 Hata hivyo, Mwovu huyo aliyefichika anafanya kazi sasa, lakini hataonekana mpaka yule anayemzuia aondolewe.

2:8b.2TH.002.008 Hapo ndipo Mwovu atakapotokea; lakini Bwana Yesu anapokuja atamuua kwa pumzi ya kinywa chake na kumwangamiza kwa mng'ao wa kuja kwake.

2:9b.2TH.002.009 Huyo Mwovu atakuja na nguvu za Shetani na kufanya kila namna ya miujiza na maajabu ya uongo,

2:10b.2TH.002.010 na kutumia udanganyifu wa kila namna kwa wale walio katika mkumbo wa kupotea. Hao watapotea kwa sababu hawakuupokea na kuupenda ule ukweli ili waokolewe.

2:11b.2TH.002.011 Ndiyo maana Mungu amewaweka chini ya nguvu ya upotovu, wauamini uongo.

2:12b.2TH.002.012 Matokeo yake ni kwamba wote wasioamini ukweli, ila wafurahia dhambi, watahukumiwa.

2:13b.2TH.002.013 Tunapaswa kumshukuru Mungu daima kwa ajili yenu ninyi ndugu, ninyi mnaopendwa na Bwana, kwa maana Mungu amewateua tangu mwanzo mpate kuokolewa kwa nguvu ya Roho mfanywe watu wake watakatifu kwa imani yenu katika ukweli.

2:14b.2TH.002.014 Mungu aliwaitieni jambo hili kwa njia ya Habari Njema tuliyowahubirieni; aliwaiteni mpate kupokea sehemu yenu katika utukufu wa Bwana wetu Yesu Kristo.

2:15b.2TH.002.015 Basi, ndugu, simameni imara na zingatieni yale mafundisho tuliyowafundisheni kwa mahubiri yetu na barua zetu.

2:16b.2TH.002.016 Tunamwomba Bwana wetu Yesu Kristo mwenyewe na Mungu Baba yetu ambaye alitupenda, na kwa neema yake akatujalia faraja ya milele na tumaini jema,

2:17b.2TH.002.017 aifariji mioyo yenu na kuwaimarisheni ili mweze daima kutenda na kusema yaliyo mema.

3

3:1b.2TH.003.001 Hatimaye, ndugu, tuombeeni ili ujumbe wa Bwana uzidi kuenea upesi na kupokelewa kwa heshima kama vile ulivyo kati yenu.

3:2b.2TH.003.002 Ombeni pia ili Mungu atuokoe na watu wapotovu na waovu, maana si wote wanaoamini ujumbe huu.

3:3b.2TH.003.003 Lakini Bwana ni mwaminifu. Yeye atawaimarisheni na kuwalinda salama na yule Mwovu.

3:4b.2TH.003.004 Naye Bwana anatupatia tumaini kubwa juu yenu, na hatuna shaka kwamba mnafanya na mtaendelea kufanya yale tuliyowaambieni.

3:5b.2TH.003.005 Bwana aiongoze mioyo yenu katika upendo wa Mungu na katika uvumilivu tunaopewa na Kristo.

3:6b.2TH.003.006 Ndugu, tunawaamuru kwa jina la Bwana wetu Yesu Kristo, mjiepushe na ndugu wote walio wavivu na ambao hawafuati maagizo tuliyowapa.

3:7b.2TH.003.007 Ninyi wenyewe mnajua kwamba mnapaswa kufuata mfano wetu. Sisi tulipokuwa nanyi hatukuwa wavivu;

3:8b.2TH.003.008 hatukula chakula kwa mtu yeyote bila ya kumlipa. Tulifanya kazi kwa bidii na taabu mchana na usiku ili tusiwe mzigo kwa mtu yeyote kati yenu.

3:9b.2TH.003.009 Tulifanya hivyo si kwa kuwa hatuna haki ya kutaka msaada wenu, ila kwa sababu tunataka kuwapeni mfano.

3:10b.2TH.003.010 Tulipokuwa pamoja nanyi tulikuwa tukiwaambieni, "Mtu asiyefanya kazi, asile."

3:11b.2TH.003.011 Tunasema mambo hayo kwa sababu tumesikia kwamba wako baadhi yenu ambao ni wavivu na ambao hawafanyi chochote, isipokuwa tu kujiingiza katika mambo ya watu wengine.

3:12b.2TH.003.012 Kwa jina la Bwana wetu Yesu Kristo tunawaamuru na kuwaonya watu hao wawe na nidhamu na kufanya kazi ili wajipatie maslahi yao wenyewe.

3:13b.2TH.003.013 Lakini ninyi ndugu, msichoke kutenda mema.

3:14b.2TH.003.014 Huenda kwamba huko kuna mtu ambaye hatautii huu ujumbe tunaowapelekeeni katika barua hii. Ikiwa hivyo, basi, mfichueni mtu huyo na msiwe na uhusiano wowote naye kusudi aone aibu.

3:15b.2TH.003.015 Lakini msimtendee mtu huyo kama adui, bali mwonyeni kama ndugu.

3:16b.2TH.003.016 Bwana mwenyewe ndiye chanzo cha amani, awajalieni amani siku zote kwa kila namna. Bwana awe nanyi nyote.

3:17b.2TH.003.017 Kwa mkono wangu mwenyewe naandika hivi: Salamu kutoka kwa Paulo! Hivi ndivyo ninavyotia sahihi kila barua; ndivyo ninavyoandika.

3:18b.2TH.003.018 Tunawatakieni nyote neema ya Bwana wetu Yesu Kristo.


Holder of rights
Multilingual Bible Corpus

Citation Suggestion for this Object
TextGrid Repository (2025). Swahili Collection. 2 Thessalonians (Swahili). 2 Thessalonians (Swahili). Multilingual Parallel Bible Corpus. Multilingual Bible Corpus. https://hdl.handle.net/21.11113/0000-0016-B996-E