1 Thessalonians (Swahili)

1 Thessalonians (Swahili)

1

1:1b.1TH.001.001 Mimi Paulo, Silwano na Timotheo tunawaandikia ninyi jumuiya ya kanisa la Thesalonike, ambao ni watu wake Mungu Baba, na wa Bwana Yesu Kristo.

1:2b.1TH.001.002 Tunamshukuru Mungu daima kwa ajili yenu ninyi nyote na kuwakumbukeni daima katika sala zetu.

1:3b.1TH.001.003 Maana, mbele ya Mungu Baba yetu, twakumbuka jinsi mnavyoonyesha imani yenu kwa matendo, jinsi upendo wenu unavyowawezesha kufanya kazi kwa bidii, na jinsi tumaini lenu katika Bwana wetu Yesu Kristo lilivyo thabiti.

1:4b.1TH.001.004 Ndugu, twajua kwamba Mungu anawapenda na kwamba amewateua muwe watu wake,

1:5b.1TH.001.005 maana wakati tulipowahubirieni ile Habari Njema haikuwa kwa maneno tu, bali pia kwa nguvu na kwa Roho Mtakatifu, tukiwa na hakika kwamba ujumbe huo ulikuwa wa kweli. Mnajua jinsi tulivyoishi pamoja nanyi; tuliishi kwa manufaa yenu.

1:6b.1TH.001.006 Ninyi mlifuata mfano wetu, na kumwiga Bwana. Ingawa mliteswa sana, mliupokea ujumbe huo kwa furaha itokayo kwa Roho Mtakatifu.

1:7b.1TH.001.007 Kwa hiyo ninyi mmekuwa mfano mzuri kwa waumini wote wa Makedonia na Akaya.

1:8b.1TH.001.008 Maana, kutokana na bidii yenu ujumbe wa Bwana umesikika si tu huko Makedonia na Akaya, bali imani yenu kwa Mungu imeenea popote. Tena hatuhitaji kusema zaidi.

1:9b.1TH.001.009 Watu hao wanazungumza juu ya ziara yetu kwenu: jinsi mlivyotukaribisha, jinsi mlivyoziacha sanamu mkamgeukia Mungu aliye hai na wa kweli,

1:10b.1TH.001.010 na sasa mwamngojea Mwanae ashuke kutoka mbinguni, Yesu, ambaye Mungu alimfufua kutoka wafu, na ambaye anatuokoa katika ghadhabu ya Mungu inayokuja.

2

2:1b.1TH.002.001 Ndugu, ninyi wenyewe mnafahamu kwamba ziara yetu kwenu haikuwa bure.

2:2b.1TH.002.002 Mnajua jinsi tulivyodhulumiwa na kutukanwa kule Filipi kabla ya kufika kwenu Thesalonike. Ingawa kulikuwa na upinzani mwingi, Mungu wetu alitujalia uhodari wa kuwahubirieni Habari Njema yake.

2:3b.1TH.002.003 Jambo tunalosisitiza kwenu si jambo linalotegemea uongo au nia mbaya; wala hatupendi kumdanganya mtu yeyote.

2:4b.1TH.002.004 Sisi twanena daima kama atakavyo Mungu kwani yeye alituona kwamba tunafaa, akatukabidhi hii Habari Njema. Si nia yetu kuwapendeza watu hata kidogo, bali twataka kumpendeza Mungu ambaye anajua mioyo yetu mpaka ndani.

2:5b.1TH.002.005 Ninyi mnajua kwamba sisi hatukuja kwenu na maneno matamu ya kubembeleza wala hatukutumia maneno ya kijanja ya kuficha ubinafsi fulani; Mungu ni shahidi!

2:6b.1TH.002.006 Hatukutafuta sifa kutoka kwa watu, wala kutoka kwenu, wala kutoka kwa mtu yeyote,

2:7b.1TH.002.007 ingawa sisi tukiwa mitume wa Kristo, tungeweza kudai mambo fulani kwenu. Lakini sisi tulikuwa Wapole kati yenu kama alivyo mama kwa watoto wake.

2:8b.1TH.002.008 Tuliwapenda ninyi sana hata tukawa tayari kuwashirikisha si tu Habari Njema ya Mungu, bali pia na maisha yetu. Ndivyo mlivyokuwa wapenzi wetu!

2:9b.1TH.002.009 Ndugu, mnakumbuka jinsi tulivyofanya kazi na kutaabika. Tulipowaleteeni Habari Njema ya Mungu tulifanya kazi mchana na usiku kusudi tusiwe mzigo kwa mtu yeyote miongoni mwenu.

2:10b.1TH.002.010 Ninyi mnaweza kushuhudia, na Mungu pia ni shahidi, jinsi mwenendo wetu kati yenu ninyi mnaoamini ulivyokuwa mzuri, mwadilifu na usio na lawama.

2:11b.1TH.002.011 Mnajua kwamba sisi tulimtendea kila mmoja wenu kama vile baba anavyowatendea watoto wake mwenyewe.

2:12b.1TH.002.012 Tuliwapeni moyo, tuliwafarijini na kuwahimiza ili mpate kuishi maisha yampendezayo Mungu ambaye aliwaiteni mshiriki Utawala na utukufu wake.

2:13b.1TH.002.013 Tena tunayo sababu nyingine ya kumshukuru Mungu: tulipowaleteeni ujumbe wa Mungu, ninyi mliusikia mkaupokea, si kama vile ujumbe wa binadamu, bali kama ujumbe wa Mungu, na kweli ndivyo ulivyo. Maana Mungu anafanya kazi ndani yenu ninyi mnaoamini.

2:14b.1TH.002.014 Ndugu, ninyi mmepatwa na mambo yaleyale yaliyoyapata makanisa ya Mungu kule Yudea, mambo yaliyowapata watu walio wake Kristo Yesu. Ninyi mlidhulumiwa na wananchi wenzenu kama vile wao walivyodhulumiwa na wenzao Wayahudi,

2:15b.1TH.002.015 ambao walimuua Bwana Yesu na manabii, wakatutesa na sisi pia. Watu hao wanamchukiza Mungu, tena ni adui za kila mtu!

2:16b.1TH.002.016 Hata walijaribu kutuzuia kuwahubiria watu wa mataifa mengine ujumbe utakaowaletea wokovu. Ndivyo walivyokamilisha orodha ya dhambi zote walizotenda siku zote. Lakini sasa hasira ya Mungu imewaangukia.

2:17b.1TH.002.017 Ndugu, kuachana kwetu nanyi kulikuwa kwa muda tu, tena kuachana huko kulikuwa kwa mwili tu na si kwa roho. Kitambo kifupi baadaye, tulishikwa na hamu kubwa ya kuwaoneni tena!

2:18b.1TH.002.018 Kwa hiyo tuliamua kuwatembeleeni tena. Nami, Paulo, nilijaribu kuja kwenu zaidi ya mara moja, lakini Shetani alituzuia.

2:19b.1TH.002.019 Je, tutakaposimama mbele ya Bwana Yesu wakati atakapokuja, fahari ya ushindi wetu itakuwa nini? Itakuwa ni ninyi wenyewe; ninyi ndio tumaini letu na furaha yetu.

2:20b.1TH.002.020 Naam, ninyi ni utukufu wetu na furaha yetu!

3

3:1b.1TH.003.001 Mwishowe hatukuweza kuvumilia zaidi. Basi, tuliamua kubaki kule Athene peke yetu,

3:2b.1TH.003.002 na kumtuma kwenu ndugu yetu Timotheo, ambaye ni mfanyakazi mwenzetu kwa ajili ya Mungu katika kuhubiri Habari Njema ya Kristo. Tulimtuma ili awaimarisheni na kuwafarijini,

3:3b.1TH.003.003 kusudi imani ya mtu yeyote miongoni mwenu isije ikafifia kwa sababu ya taabu hizo. Ninyi mnajua kwamba tunapaswa kupata mateso.

3:4b.1TH.003.004 Maana, tulipokuwa pamoja nanyi, tuliwaambieni kwamba tutateswa; na kama mjuavyo ndivyo ilivyotukia.

3:5b.1TH.003.005 Ndio maana nilimtuma Timotheo kwenu. Sikuweza kungoja zaidi, na hivyo nilimtuma nipate habari za imani yenu. Isije ikawa labda Mshawishi aliwajaribuni na kazi yote tuliyofanya miongoni mwenu imepotea bure!

3:6b.1TH.003.006 Sasa Timotheo amekwisha rudi, naye ametupa habari za kufurahisha kuhusu imani na upendo wenu. Ametuarifu kwamba mnatukumbuka daima, na kwamba mna hamu ya kutuona sisi kama nasi tulivyo na hamu ya kuwaoneni.

3:7b.1TH.003.007 Basi, habari za imani yenu zimetutia moyo katika taabu na mateso yetu yote,

3:8b.1TH.003.008 kwani sasa tunaishi kweli ikiwa ninyi mnasimama imara katika kuungana na Bwana.

3:9b.1TH.003.009 Sasa twaweza kumshukuru Mungu wetu kwa ajili yenu. Tunamshukuru kwa furaha tuliyo nayo mbele yake kwa sababu yenu.

3:10b.1TH.003.010 Tunazidi kumwomba Mungu usiku na mchana kwa moyo wetu wote ili atupatie fursa ya kuwaoneni uso kwa uso ili tuweze kurekebisha chochote kilichopungua katika imani yenu.

3:11b.1TH.003.011 Tunamwomba Mungu, Baba yetu mwenyewe, na Bwana wetu Yesu atutayarishie njia ya kuja kwenu.

3:12b.1TH.003.012 Bwana awawezeshe ninyi kupendana na kuwapenda watu wote zaidi na zaidi, kama vile sisi tunavyowapenda ninyi.

3:13b.1TH.003.013 Hivyo ataiimarisha mioyo yenu, nanyi mtakuwa wakamilifu na watakatifu mbele ya Mungu na Baba yetu wakati Bwana wetu Yesu atakapokuja pamoja na wote walio wake.

4

4:1b.1TH.004.001 Hatimaye, ndugu zangu, mmejifunza kutoka kwetu namna mnavyopaswa kuishi ili kumpendeza Mungu. Na kweli mmekuwa mnaishi hivyo. Sasa tunawaombeni na kuwasihi kwa jina la Bwana Yesu mfanye vema zaidi.

4:2b.1TH.004.002 Maana mnayajua yale maagizo tuliyowapeni kwa mamlaka ya Bwana Yesu.

4:3b.1TH.004.003 Mungu anataka ninyi muwe watakatifu na mjiepushe kabisa na maisha ya zinaa.

4:4b.1TH.004.004 Kila mwanamume anapaswa kujua namna ya kuishi na mkewe kwa utakatifu na heshima,

4:5b.1TH.004.005 na si kwa tamaa mbaya kama watu wa mataifa mengine wasiomjua Mungu.

4:6b.1TH.004.006 Basi, mtu yeyote asimkosee au kumpunja mwenzake kuhusu jambo hili. Tulikwisha waambieni hayo na kuwaonya kwamba Bwana atawaadhibu wanaofanya mambo hayo.

4:7b.1TH.004.007 Mungu hakutuita tuishi maisha ya zinaa, bali tuishi katika utakatifu.

4:8b.1TH.004.008 Kwa hiyo basi, anayedharau mafundisho hayo hamdharau mtu, bali amdharau Mungu mwenyewe anayewapeni Roho wake Mtakatifu.

4:9b.1TH.004.009 Hakuna haja ya kuwaandikieni juu ya kuwapenda ndugu zenu waumini. Ninyi wenyewe mmefundishwa na Mungu namna mnavyopaswa kupendana.

4:10b.1TH.004.010 Na mmekuwa mkiwatendea hivyo ndugu zenu wote kila mahali katika Makedonia. Basi, ndugu tunawaombeni mfanye hata zaidi.

4:11b.1TH.004.011 Muwe na nia ya kuishi maisha ya utulivu, kila mmoja ashughulikie mambo yake mwenyewe na afanye kazi kwa mikono yake mwenyewe kama tulivyowaagiza pale awali.

4:12b.1TH.004.012 Kwa namna hiyo mtajipatia sifa nzuri kutoka kwa wale wasio Wakristo, na hamtakuwa na lazima ya kuwategemea wengine kwa mahitaji yenu.

4:13b.1TH.004.013 Ndugu, twataka mjue ukweli kuhusu wale ambao wamekwisha fariki dunia, ili msipatwe na huzuni kama watu wengine wasio na matumaini.

4:14b.1TH.004.014 Sisi tunaamini kwamba Yesu alikufa, akafufuka; na hivyo sisi tunaamini kwamba Mungu atawaleta pamoja na Yesu wale wote waliofariki wakiwa wanamwamini.

4:15b.1TH.004.015 Hili tunalowaambieni ni fundisho la Bwana; sisi tulio hai, ambao tutakuwa tumebaki, wakati Bwana atakapokuja, hakika hatutawatangulia wale waliokwisha fariki dunia.

4:16b.1TH.004.016 Maana patatolewa amri, sauti ya malaika mkuu, sauti ya tarumbeta ya Mungu, naye Bwana mwenyewe atashuka kutoka mbinguni. Ndipo wale waliokufa wakiwa wanamwamini Kristo watafufuliwa kwanza.

4:17b.1TH.004.017 Kisha sisi tulio hai wakati huo tutakusanywa pamoja nao katika mawingu kumlaki Bwana hewani. Na hivyo tutakuwa daima pamoja na Bwana.

4:18b.1TH.004.018 Basi, farijianeni kwa maneno haya.

5

5:1b.1TH.005.001 Ndugu, hakuna haja ya kuwaandikieni juu ya nyakati na majira yatakapotukia mambo haya.

5:2b.1TH.005.002 Maana ninyi wenyewe mwajua kwamba Siku ya Bwana itakuja kama mwizi ajavyo usiku.

5:3b.1TH.005.003 Watu watakapokuwa wanasema: "Kila kitu ni shwari na salama" ndipo uharibifu utakapowaangukia ghafla! Mambo hayo yatatukia ghafla kama uchungu wa uzazi unavyomjia mama anayejifungua, wala watu hawataweza kuepukana nayo.

5:4b.1TH.005.004 Lakini ninyi ndugu, hamko gizani, na siku hiyo haipaswi kuwajieni ghafla kama vile mwizi.

5:5b.1TH.005.005 Ninyi nyote ni watu mnaoishi katika mwanga, watu wa mchana. Sisi si watu wa usiku, wala wa giza.

5:6b.1TH.005.006 Basi, tusilale usingizi kama wengine; tunapaswa kukesha na kuwa na kiasi.

5:7b.1TH.005.007 Wanaolala hulala usiku, na walevi hulewa usiku.

5:8b.1TH.005.008 Lakini sisi ni watu wa mchana na tunapaswa kuwa na kiasi. Tunapaswa kuvaa imani na upendo kama vazi la kujikinga kifuani, na tumaini letu la wokovu kama kofia ya chuma.

5:9b.1TH.005.009 Maana Mungu hakututeua ili tuangamizwe na ghadhabu yake, bali tuupate wokovu kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo,

5:10b.1TH.005.010 ambaye alikufa kwa ajili yetu, ili tuishi pamoja naye, iwe tu hai au tumekufa.

5:11b.1TH.005.011 Kwa hiyo farijianeni na kusaidiana ninyi kwa ninyi kama mnavyofanya sasa.

5:12b.1TH.005.012 Ndugu, tunawaombeni muwastahi wale wanaofanya kazi kati yenu, wale wanaowaongoza na kuwafundisheni kuhusu maisha ya Kikristo.

5:13b.1TH.005.013 Wapeni heshima kubwa na kuwapenda kwa sababu ya kazi wanayofanya. Muwe na amani kati yenu.

5:14b.1TH.005.014 Ndugu, tunawahimizeni muwaonye watu walio wavivu, muwatie moyo watu wanyonge, muwasaidie watu dhaifu, muwe na subira kwa wote.

5:15b.1TH.005.015 Angalieni mtu yeyote asimlipe mwingine maovu kwa maovu, ila nia yenu iwe kutendeana mema daima na kuwatendea mema watu wote.

5:16b.1TH.005.016 Furahini daima,

5:17b.1TH.005.017 salini kila wakati

5:18b.1TH.005.018 na muwe na shukrani katika kila hali. Hayo ndiyo anayotaka Mungu kwenu katika kuungana kwenu na Kristo Yesu.

5:19b.1TH.005.019 Msimpinge Roho Mtakatifu;

5:20b.1TH.005.020 msidharau unabii.

5:21b.1TH.005.021 Pimeni kila kitu: zingatieni kilicho chema,

5:22b.1TH.005.022 na epukeni kila aina ya uovu.

5:23b.1TH.005.023 Mungu anayetupatia amani awafanye ninyi watakatifu kwa kila namna na kuzilinda nafsi zenu--roho, mioyo na miili yenu--mbali na hatia yoyote wakati wa kuja kwake Bwana wetu Yesu Kristo.

5:24b.1TH.005.024 Yeye anayewaita ninyi atafanya hivyo kwani ni mwaminifu.

5:25b.1TH.005.025 Ndugu, tuombeeni na sisi pia.

5:26b.1TH.005.026 Wasalimuni ndugu wote kwa ishara ya upendo.

5:27b.1TH.005.027 Nawahimizeni kwa jina la Bwana muwasomee ndugu zetu wote barua hii.

5:28b.1TH.005.028 Tunawatakieni neema ya Bwana wetu Yesu Kristo.


Holder of rights
Multilingual Bible Corpus

Citation Suggestion for this Object
TextGrid Repository (2025). Swahili Collection. 1 Thessalonians (Swahili). 1 Thessalonians (Swahili). Multilingual Parallel Bible Corpus. Multilingual Bible Corpus. https://hdl.handle.net/21.11113/0000-0016-B993-1