Hebrews (Swahili)
1
1:1b.HEB.001.001 Hapo zamani, Mungu alisema na babu zetu mara nyingi kwa namna nyingi kwa njia ya manabii,
1:2b.HEB.001.002 lakini siku hizi za mwisho, amesema nasi kwa njia ya Mwanae. Yeye ndiye ambaye kwa njia yake Mungu aliumba ulimwengu na akamteua avimiliki vitu vyote.
1:3b.HEB.001.003 Yeye ni mng'ao wa utukufu wa Mungu, na mfano kamili wa hali ya Mungu mwenyewe, akiutegemeza ulimwengu kwa neno lake lenye nguvu. Baada ya kuwapatia binadamu msamaha wa dhambi zao, aliketi huko juu mbinguni, upande wa kulia wa Mungu Mkuu.
1:4b.HEB.001.004 Mwana ni mkuu zaidi kuliko malaika, kama vile jina alilopewa na Mungu ni kuu zaidi kuliko jina lao.
1:5b.HEB.001.005 Maana Mungu hakumwambia kamwe hata mmoja wa malaika wake: "Wewe ni Mwanangu; Mimi leo nimekuwa Baba yako." Wala hakusema juu ya malaika yeyote: "Mimi nitakuwa Baba yake, naye atakuwa Mwanangu."
1:6b.HEB.001.006 Lakini Mungu alipokuwa anamtuma Mwanae mzaliwa wa kwanza ulimwenguni, alisema: "Malaika wote wa Mungu wanapaswa kumwabudu."
1:7b.HEB.001.007 Lakini kuhusu malaika, Mungu alisema: "Mungu awafanya malaika wake kuwa pepo, na watumishi wake kuwa ndimi za moto."
1:8b.HEB.001.008 Lakini kumhusu Mwana, Mungu alisema: "Utawala wako ee Mungu, wadumu milele na milele! Wewe wawatawala watu wako kwa haki.
1:9b.HEB.001.009 Wewe wapenda uadilifu na kuchukia uovu. Ndiyo maana Mungu, Mungu wako amekuweka wakfu na kukumiminia furaha kubwa zaidi kuliko wenzako."
1:10b.HEB.001.010 Pia alisema: "Bwana, wewe uliumba dunia hapo mwanzo, mbingu ni kazi ya mikono yako.
1:11b.HEB.001.011 Hizo zitatoweka, lakini wewe wabaki daima, zote zitachakaa kama vazi.
1:12b.HEB.001.012 Utazikunjakunja kama koti, nazo zitabadilishwa kama vazi. Lakini wewe ni yuleyule daima, na maisha yako hayatakoma."
1:13b.HEB.001.013 Mungu hakumwambia kamwe hata mmoja wa malaika wake: "Keti upande wangu wa kulia, mpaka niwaweke adui zako chini ya miguu yako."
1:14b.HEB.001.014 Malaika ni roho tu wanaomtumikia Mungu, na Mungu huwatuma wawasaidie wale watakaopokea wokovu.
2
2:1b.HEB.002.001 Kwa sababu hiyo tunapaswa kuzingatia kwa makini zaidi yote tuliyosikia, ili tusije tukapotoshwa.
2:2b.HEB.002.002 Ujumbe ule waliopewa wazee wetu na malaika ulionyeshwa kuwa kweli, hata mtu yeyote ambaye hakuufuata au hakuutii aliadhibiwa kama alivyostahili.
2:3b.HEB.002.003 Basi, sisi tutaokokaje kama hatuujali wokovu mkuu kama huu? Kwanza Bwana mwenyewe aliutangaza wokovu huu, na wale waliomsikia walituthibitishia kwamba ni kweli.
2:4b.HEB.002.004 Mungu pia aliongeza hapo ushahidi wake kwa kufanya kila namna ya miujiza na maajabu, na kwa kuwagawia watu vipaji vya Roho Mtakatifu kadiri ya mapenzi yake.
2:5b.HEB.002.005 Mungu hakuwaweka malaika wautawale ulimwengu ujao, yaani ulimwengu ule tunaoongea habari zake.
2:6b.HEB.002.006 Tena yasemwa mahali fulani katika Maandiko: "Mtu ni nini ee Mungu, hata umfikirie; mwanaadamu ni nini hata umjali?
2:7b.HEB.002.007 Ulimfanya kwa kitambo kidogo kuwa chini zaidi kuliko malaika; ukamvika taji ya utukufu na heshima,
2:8b.HEB.002.008 ukaweka kila kitu chini ya miguu yake, avitawale." Yasemwa kwamba Mungu alimweka mtu kuwa mtawala wa vitu vyote yaani bila kuacha hata kimoja. Hata hivyo, hatuoni bado mtu akivitawala vitu vyote sasa.
2:9b.HEB.002.009 Lakini twamwona Yesu ambaye alifanywa kwa kitambo kidogo kuwa chini zaidi kuliko malaika, ili kwa neema ya Mungu afe kwa ajili ya watu wote. Sasa tunamwona ametawazwa kwa utukufu na heshima kwa sababu ya kifo alichoteseka.
2:10b.HEB.002.010 Ilikuwa haki tupu kwamba Mungu, ambaye huumba na kutegemeza vitu vyote, alimfanya Yesu kuwa mkamilifu kabisa kwa njia ya mateso, ili awalete watoto wengi waushiriki utukufu wake. Maana Yesu ndiye anayewaongoza kwenye wokovu.
2:11b.HEB.002.011 Yeye anawatakasa watu dhambi zao, naye pamoja na wale waliotakaswa, wote wanaye Baba mmoja. Ndiyo maana Yesu haoni aibu kuwaita hao ndugu zake;
2:12b.HEB.002.012 kama asemavyo: "Ee Mungu, nitawatangazia ndugu zangu matendo yako. Nitakusifu katika kusanyiko lao."
2:13b.HEB.002.013 Tena asema: "Nitamwekea Mungu tumaini langu." Na tena: "Mimi niko hapa pamoja na watoto alionipa Mungu."
2:14b.HEB.002.014 Basi, kwa vile watoto hao, kama awaitavyo, ni watu wenye mwili na damu, Yesu mwenyewe akawa kama wao na kushiriki ubinadamu wao. Alifanya hivyo ili kwa njia ya kifo chake amwangamize Ibilisi, ambaye ana mamlaka juu ya kifo,
2:15b.HEB.002.015 na hivyo awaokoe wale waliokuwa watumwa maisha yao yote kwa sababu ya hofu yao ya kifo.
2:16b.HEB.002.016 Maana ni wazi kwamba yeye hakuja kwa ajili ya kuwasaidia malaika, bali kama yasemavyo Maandiko; "Anawasaidia wazawa wa Abrahamu."
2:17b.HEB.002.017 Ndiyo maana ilimbidi awe kama ndugu zake kwa kila namna, ili awe Kuhani Mkuu wao aliye mwaminifu na mwenye huruma katika kumtumikia Mungu, ili dhambi za watu ziondolewe.
2:18b.HEB.002.018 Na, anaweza sasa kuwasaidia wale wanaojaribiwa na kuteswa.
3
3:1b.HEB.003.001 Ndugu zangu watu wa Mungu ambao mmeitwa na Mungu, fikirini juu ya Yesu ambaye Mungu alimtuma awe Kuhani Mkuu wa imani tunayoiungama.
3:2b.HEB.003.002 Yeye alikuwa mwaminifu kwa Mungu aliyemteua kufanya kazi yake kama vile Mose alivyokuwa mwaminifu katika nyumba yote ya Mungu.
3:3b.HEB.003.003 Mjenzi wa nyumba hupata heshima zaidi kuliko hiyo nyumba yenyewe. Hali kadhalika naye Yesu anastahili heshima kubwa zaidi kuliko Mose.
3:4b.HEB.003.004 Kila nyumba hujengwa na mjenzi fulani--na Mungu ndiye mjenzi wa vitu vyote.
3:5b.HEB.003.005 Mose alikuwa mwaminifu katika nyumba yote ya Bwana kama mtumishi, na alinena juu ya mambo ambayo Mungu atayasema hapo baadaye.
3:6b.HEB.003.006 Lakini Kristo ni mwaminifu kama Mwana mwenye mamlaka juu ya nyumba ya Mungu. Sisi ni nyumba yake kama tukizingatia uhodari wetu na uthabiti wetu katika kile tunachotumainia.
3:7b.HEB.003.007 Kwa hiyo, basi, kama asemavyo Roho Mtakatifu: "Kama mkisikia sauti ya Mungu leo,
3:8b.HEB.003.008 msiifanye mioyo yenu kuwa migumu kama wazee wenu walivyokuwa wakati walipomwasi Mungu; kama walivyokuwa siku ile kule jangwani,
3:9b.HEB.003.009 Huko wazee wenu walinijaribu na kunichunguza, asema Bwana, ingawa walikuwa wameyaona matendo yangu kwa miaka arobaini.
3:10b.HEB.003.010 Kwa sababu hiyo niliwakasirikia watu hao nikasema, Fikira za watu hawa zimepotoka, hawajapata kamwe kuzijua njia zangu.
3:11b.HEB.003.011 Basi, nilikasirika, nikaapa: Hawataingia huko ambako ningewapa pumziko."
3:12b.HEB.003.012 Basi ndugu, jihadharini asije akawako yeyote miongoni mwenu aliye na moyo mbaya hivyo na asiyeamini hata kujitenga na Mungu aliye hai.
3:13b.HEB.003.013 Maadamu hiyo "Leo" inayosemwa katika Maandiko bado inatuhusu sisi, mnapaswa kusaidiana daima, ili mtu yeyote miongoni mwenu asidanganywe na dhambi na kuwa mkaidi.
3:14b.HEB.003.014 Maana sisi tunashirikiana na Kristo ikiwa tutazingatia kwa uthabiti tumaini tulilokuwa nalo mwanzoni.
3:15b.HEB.003.015 Maandiko yasema hivi: "Kama mkisikia sauti ya Mungu leo, msiifanye mioyo yenu kuwa migumu kama wazee wenu walivyokuwa wakati walipomwasi Mungu."
3:16b.HEB.003.016 Ni akina nani basi, waliosikia sauti ya Mungu wakamwasi? Ni wale wote walioongozwa na Mose kutoka Misri.
3:17b.HEB.003.017 Mungu aliwakasirikia akina nani kwa miaka arobaini? Aliwakasirikia wale waliotenda dhambi, maiti zao zikatapakaa kule jangwani.
3:18b.HEB.003.018 Mungu alipoapa: "Hawataingia huko ambako ningewapa pumziko," alikuwa anawasema akina nani? Alikuwa anasema juu ya hao walioasi.
3:19b.HEB.003.019 Basi, twaona kwamba hawakuingia huko kwa sababu hawakuamini.
4
4:1b.HEB.004.001 Mungu alituahidia kwamba tutaweza kupata pumziko hilo alilosema. Basi, na tuogope ili yeyote kati yenu asije akashindwa kupata pumziko hilo.
4:2b.HEB.004.002 Maana Habari Njema imehubiriwa kwetu kama vile ilivyohubiriwa kwa hao watu wa kale. Lakini ujumbe huo haukuwafaa chochote, maana waliusikia lakini hawakuupokea kwa imani.
4:3b.HEB.004.003 Basi, sisi tunaoamini tunapata pumziko hilo aliloahidi Mungu. Kama alivyosema: "Nilikasirika, nikaapa: Hawataingia huko ambako ningewapa pumziko." Mungu alisema hayo ingawa kazi yake ilikuwa imekwisha malizika tangu alipoumba ulimwengu.
4:4b.HEB.004.004 Maana Maandiko yasema mahali fulani kuhusu siku ya saba: "Mungu alipumzika siku ya saba, akaacha kazi zake zote."
4:5b.HEB.004.005 Tena jambo hili lasemwa pia: "Hawataingia huko ambako ningewapa pumziko."
4:6b.HEB.004.006 Wale waliotangulia kuhubiriwa Habari Njema hawakupata pumziko hilo kwa sababu hawakuamini. Wapo, basi, wengine ambao wangejaliwa kulipata.
4:7b.HEB.004.007 Jambo hili ni wazi, kwani Mungu aliweka siku nyingine ambayo inaitwa "Leo". Miaka mingi baadaye Mungu alisema juu ya hiyo siku kwa maneno ya Daudi katika Maandiko yaliyokwisha tajwa: "Kama mkisikia sauti ya Mungu leo, msiifanye mioyo yenu kuwa migumu."
4:8b.HEB.004.008 Kama Yoshua angaliwapa watu hao hilo pumziko, Mungu hangalisema baadaye juu ya siku nyingine.
4:9b.HEB.004.009 Kwa hiyo, basi, bado lipo pumziko kwa watu wa Mungu kama kule kupumzika kwake Mungu siku ya saba.
4:10b.HEB.004.010 Maana, kila anayepata pumziko aliloahidi Mungu atapumzika baada ya kazi yake kama vile pia Mungu alivyopumzika baada ya yake.
4:11b.HEB.004.011 Basi, tujitahidi kupata pumziko hilo, ili asiwepo yeyote miongoni mwenu atakayeshindwa, kama walivyofanya wao kwa sababu ya ukosefu wao wa imani.
4:12b.HEB.004.012 Neno la Mungu ni hai na lina nguvu; ni kali zaidi kuliko upanga wenye makali kuwili. Hukata kabisa mpaka mahali ambapo moyo na roho hukutana, mpaka pale vikutanapo viungo vya mwili na mafuta. Neno hilo huchambua nia na fikira za mioyo ya watu.
4:13b.HEB.004.013 Hakuna kiumbe chochote kilichofichika mbele ya Mungu; kila kitu kimefunuliwa wazi mbele ya macho yake. Kwake, sisi sote tutapaswa kutoa hoja ya matendo yetu.
4:14b.HEB.004.014 Basi, tunapaswa kuzingatia kwa uthabiti imani tunayoiungama. Maana tunaye Kuhani Mkuu aliyeingia mpaka kwa Mungu mwenyewe--Yesu, Mwana wa Mungu.
4:15b.HEB.004.015 Huyu Kuhani Mkuu wetu si mmoja ambaye hawezi kutuunga mkono katika unyonge wetu, ila ni Kuhani Mkuu ambaye alijaribiwa kama sisi kwa kila namna lakini hakutenda dhambi.
4:16b.HEB.004.016 Basi, na tukikaribie bila hofu kiti cha enzi cha Mungu, palipo na neema, ili tukajipatie huruma na neema ya kutusaidia wakati wa lazima.
5
5:1b.HEB.005.001 Kila kuhani mkuu huchaguliwa kutoka miongoni mwa watu kwa ajili ya kumtumikia Mungu kwa niaba yao, kutolea zawadi na tambiko kwa ajili ya dhambi zao.
5:2b.HEB.005.002 Maadamu yeye mwenyewe yu dhaifu anaweza kuwaonea huruma wale wasiojua kitu na wanaofanya makosa.
5:3b.HEB.005.003 Na kwa vile yeye mwenyewe ni dhaifu, anapaswa kutolea dhabihu si tu kwa ajili ya watu, bali pia kwa ajili ya dhambi zake.
5:4b.HEB.005.004 Hakuna mtu awezaye kujitwalia mwenyewe heshima ya kuwa kuhani mkuu. Kila mmoja huteuliwa na Mungu kuwa kuhani mkuu kama alivyokuwa Aroni.
5:5b.HEB.005.005 Hali kadhalika naye Kristo hakujitwalia mwenyewe heshima ya kuwa kuhani mkuu, bali Mungu alimwambia: "Wewe ni Mwanangu; mimi leo nimekuwa baba yako."
5:6b.HEB.005.006 Alisema pia mahali pengine: "Wewe ni kuhani milele, kufuatana na utaratibu wa ukuhani wa Melkisedeki."
5:7b.HEB.005.007 Yesu alipokuwa anaishi hapa duniani, kwa kilio kikuu na machozi, alisali na kumwomba Mungu ambaye alikuwa na uwezo wa kumwokoa kutoka kifo; naye alisikilizwa kwa sababu ya kumcha Mungu.
5:8b.HEB.005.008 Lakini, ingawa alikuwa Mwana wa Mungu, alijifunza kutii kwa njia ya mateso.
5:9b.HEB.005.009 Na alipofanywa mkamilifu, akawa chanzo cha wokovu wa milele kwa wale wote wanaomtii,
5:10b.HEB.005.010 naye Mungu akamteua kuwa kuhani mkuu kufuatana na utaratibu wa ukuhani wa Melkisedeki.
5:11b.HEB.005.011 Tunayo Mengi ya kusema juu ya jambo hili, lakini ni vigumu kuwaelezeni, kwa sababu ninyi si wepesi wa kuelewa.
5:12b.HEB.005.012 Sasa mngalipaswa kuwa tayari walimu, lakini mnahitaji bado mtu wa kuwafundisheni mafundisho ya mwanzo ya ujumbe wa Mungu. Badala ya kula chakula kigumu, mnapaswa bado kunywa maziwa.
5:13b.HEB.005.013 Kila anayepaswa kunywa maziwa huyo ni mtoto bado, hajui uadilifu ni nini.
5:14b.HEB.005.014 Lakini chakula kigumu ni kwa ajili ya watu waliokomaa, ambao wanaweza kubainisha mema na mabaya.
6
6:1b.HEB.006.001 Basi, tusonge mbele kwa yale yaliyokomaa na kuyaacha nyuma yale mafundisho ya mwanzo ya Kikristo. Hatuhitaji kuweka msingi tena kwa kurudia yale mafundisho ya mwanzo kama vile kuachana na matendo ya kifo, kumwamini Mungu;
6:2b.HEB.006.002 mafundisho juu ya ubatizo na kuwekewa mikono; ufufuo wa wafu na hukumu ya milele.
6:3b.HEB.006.003 tusonge mbele! Hayo tutayafanya, Mungu akitujalia.
6:4b.HEB.006.004 Maana watu wanaoiasi imani yao inawezekanaje kuwarudisha watubu tena? Watu hao walikwisha kuwa katika mwanga wa Mungu, walikwisha onja zawadi ya mbinguni na kushirikishwa Roho Mtakatifu;
6:5b.HEB.006.005 walikwisha onja wema wa neno la Mungu na nguvu za ulimwengu ujao,
6:6b.HEB.006.006 kisha wakaiasi imani yao! Haiwezekani kuwarudisha watubu tena, kwa sababu wanamsulubisha tena Mwana wa Mungu na kumwaibisha hadharani.
6:7b.HEB.006.007 Mungu huibariki ardhi ambayo huipokea mvua inayoinyeshea mara kwa mara, na kuotesha mimea ya faida kwa mkulima.
6:8b.HEB.006.008 Lakini kama ardhi hiyo ikiota miti ya miiba na magugu, haina faida; karibu italaaniwa na Mungu na mwisho wake ni kuchomwa moto.
6:9b.HEB.006.009 Lakini, ingawa twasema namna hii, wapenzi wetu, tunalo tumaini kubwa juu ya hali yenu. Tunajua kwamba mmepokea baraka zile bora za wokovu wenu.
6:10b.HEB.006.010 Mungu hakosi haki; yeye hataisahau kazi mliyoifanya au upendo mlioonyesha kwa ajili ya jina lake katika huduma mliyowapa na mnayowapa sasa watu wake.
6:11b.HEB.006.011 Hamu yetu ni kwamba kila mmoja wenu aonyeshe bidii hiyohiyo mpaka mwisho, ili yale mnayotumainia yapate kutimia.
6:12b.HEB.006.012 Msiwe wavivu, bali muwe kama wale wanaoamini na wenye uvumilivu na hivyo wanapokea yake aliyoahidi Mungu.
6:13b.HEB.006.013 Mungu alipompa Abrahamu ahadi, aliapa kwa jina lake mwenyewe, maana hakuna aliye mkuu kuliko Mungu ambaye kwa huyo angeweza kuapa.
6:14b.HEB.006.014 Mungu alisema: "Hakika nitakubariki na nitakupa wazawa wengi."
6:15b.HEB.006.015 Abrahamu alisubiri kwa uvumilivu na hivyo alipokea kile alichoahidiwa na Mungu.
6:16b.HEB.006.016 Watu wanapoapa, huapa kwa mmoja aliye mkuu zaidi kuliko wao, na kiapo hicho husuluhisha ubishi wote.
6:17b.HEB.006.017 Naye Mungu aliimarisha ahadi yake kwa kiapo; na kwa namna hiyo akawaonyesha wazi wale aliowaahidia kwamba hatabadili nia yake.
6:18b.HEB.006.018 Basi, kuna vitu hivi viwili: ahadi na kiapo, ambavyo haviwezi kubadilika na wala juu ya hivyo Mungu hawezi kusema uongo. Kwa hiyo sisi tuliokimbilia usalama kwake, tunapewa moyo wa kushikilia imara tumaini lililowekwa mbele yetu.
6:19b.HEB.006.019 Tunalo tumaini hilo kama nanga ya maisha yetu. Tumaini hilo ni imara na thabiti, nalo lapenya lile pazia la hekalu la mbinguni mpaka patakatifu ndani.
6:20b.HEB.006.020 Yesu ametangulia kuingia humo kwa niaba yetu, na amekuwa kuhani mkuu milele, kufuatana na utaratibu wa ukuhani wa Melkisedeki.
7
7:1b.HEB.007.001 Melkisedeki alikuwa mfalme wa Salemu, na kuhani wa Mungu Mkuu. Abrahamu alipokuwa anarudi kutoka vitani ambako aliwaua wafalme, Melkisedeki alikutana naye akambariki,
7:2b.HEB.007.002 naye Abrahamu akampa sehemu ya kumi ya vitu vyote alivyokuwa navyo. (Maana ya kwanza ya jina hili Melkisedeki ni "Mfalme wa Uadilifu"; na, kwa vile yeye alikuwa mfalme wa Salemu, jina lake pia lina maana ya "Mfalme wa Amani.")
7:3b.HEB.007.003 Baba yake na mama yake hawatajwi, wala ukoo wake hautajwi; haisemwi alizaliwa lini au alikufa lini. Anafanana na Mwana wa Mungu, na anaendelea kuwa kuhani daima.
7:4b.HEB.007.004 Basi, mwaona jinsi mtu huyu alivyokuwa maarufu. Baba Abrahamu alimpa sehemu moja ya kumi ya vitu vyote alivyoteka vitani.
7:5b.HEB.007.005 Tunajua vilevile kwamba kufuatana na Sheria, wana wa Lawi ambao ni makuhani, wanayo haki ya kuchukua sehemu ya kumi kutoka kwa watu, yaani ndugu zao, ingawaje nao ni watoto wa Abrahamu.
7:6b.HEB.007.006 Lakini huyo Melkisedeki hakuwa wa ukoo wa Lawi, hata hivyo alipokea sehemu ya kumi kutoka kwa Abrahamu; tena akambariki yeye ambaye alikuwa amepewa ahadi ya Mungu.
7:7b.HEB.007.007 Hakuna mashaka hata kidogo kwamba anayebariki ni mkuu zaidi kuliko yule anayebarikiwa.
7:8b.HEB.007.008 Tena, hao makuhani wanaopokea sehemu ya kumi, ni watu ambao hufa; lakini hapa anayepokea sehemu ya kumi, yaani Melkisedeki, anasemekana kwamba hafi.
7:9b.HEB.007.009 Twaweza, basi, kusema kwamba Abrahamu alipotoa sehemu moja ya kumi, Lawi (ambaye watoto wake hupokea sehemu moja ya kumi) alitoa sehemu moja ya kumi pia.
7:10b.HEB.007.010 Maana Lawi hakuwa amezaliwa bado, bali ni kama alikuwa katika mwili wa baba yake, Abrahamu, wakati Melkisedeki alipokutana naye.
7:11b.HEB.007.011 Kutokana na ukuhani wa Walawi, watu wa Israeli walipewa Sheria. Sasa, kama huduma ya Walawi ingalikuwa kamilifu hapangekuwa tena na haja ya kutokea ukuhani mwingine tofauti, ukuhani ambao umefuata utaratibu wa ukuhani wa Melkisedeki, na si ule wa Aroni.
7:12b.HEB.007.012 Maana ukuhani ukibadilika ni lazima Sheria nayo ibadilike.
7:13b.HEB.007.013 Naye Bwana wetu ambaye mambo hayo yote yanasemwa juu yake, alikuwa wa kabila lingine, na wala hakuna hata mmoja wa kabila lake aliyepata kutumikia madhabahuni akiwa kuhani.
7:14b.HEB.007.014 Inafahamika wazi kwamba yeye alizaliwa katika kabila la Yuda ambalo Mose hakulitaja alipokuwa anasema juu ya makuhani.
7:15b.HEB.007.015 Tena jambo hili ni dhahiri zaidi: kuhani mwingine anayefanana na Melkisedeki amekwisha tokea.
7:16b.HEB.007.016 Yeye hakufanywa kuwa kuhani kwa sheria na maagizo ya kibinadamu, bali kwa nguvu ya uhai ambao hauna mwisho.
7:17b.HEB.007.017 Maana Maandiko yasema: "Wewe ni kuhani milele, kufuatana na utaratibu wa ukuhani wa Melkisedeki."
7:18b.HEB.007.018 Basi, ile amri ya zamani ilifutwa kwa sababu ilikuwa hafifu na isiyofaa kitu.
7:19b.HEB.007.019 Maana Sheria ya Mose haikuweza kukamilisha jambo lolote. Lakini sasa, mahali pake pamewekwa tumaini lililo bora zaidi ambalo kwalo tunaweza kumkaribia Mungu.
7:20b.HEB.007.020 Zaidi ya hayo hapa pana kiapo cha Mungu. Wakati wale wengine walipofanywa makuhani hapakuwako kiapo.
7:21b.HEB.007.021 Lakini Yesu alifanywa kuhani kwa kiapo wakati Mungu alipomwambia: "Bwana ameapa, wala hataigeuza nia yake: Wewe ni kuhani milele."
7:22b.HEB.007.022 Basi, kutokana na tofauti hii, Yesu amekuwa mdhamini wa agano lililo bora zaidi.
7:23b.HEB.007.023 Kuna tofauti nyingine pia: hao makuhani wengine walikuwa wengi kwa sababu walikufa na hawakuweza kuendelea na kazi yao.
7:24b.HEB.007.024 Lakini Yesu si kama wao, yeye anaishi milele; ukuhani wake hauondoki kwake.
7:25b.HEB.007.025 Hivyo, yeye anaweza daima kuwaokoa kabisa wote wanaomwendea Mungu kwa njia yake, maana yeye anaishi milele kuwaombea kwa Mungu.
7:26b.HEB.007.026 Basi, Yesu ndiye Kuhani Mkuu ambaye anatufaa sana katika mahitaji yetu. Yeye ni mtakatifu, hana hatia wala dhambi ndani yake; hayumo katika kundi la wenye dhambi na ameinuliwa mpaka juu mbinguni.
7:27b.HEB.007.027 Yeye si kama wale makuhani wakuu wengine; hana haja ya kutoa dhabihu kila siku, kwanza kwa ajili ya dhambi zake mwenyewe, kisha kwa ajili ya dhambi za watu. Yeye alifanya hivyo mara moja tu wakati alipojitoa yeye mwenyewe, na hiyo yatosha kwa nyakati zote.
7:28b.HEB.007.028 Sheria ya Mose huwateua watu waliokuwa dhaifu kuwa makuhani wakuu; lakini ahadi ya Mungu aliyoifanya kwa kiapo na ambayo imefika baada ya sheria imemteua Mwana ambaye amefanywa mkamilifu milele.
8
8:1b.HEB.008.001 Basi, jambo muhimu katika hayo tunayosema ni hili: sisi tunaye Kuhani Mkuu wa namna hiyo, ambaye anaketi upande wa kulia wa kiti cha enzi cha Mwenyezi Mungu mbinguni.
8:2b.HEB.008.002 Yeye hutoa huduma ya Kuhani Mkuu katika Mahali Patakatifu sana, yaani ndani ya ile hema ya kweli iliyojengwa na Bwana, siyo na binadamu.
8:3b.HEB.008.003 Kila Kuhani Mkuu ameteuliwa kumtolea Mungu vipawa na dhabihu, na hivyo Kuhani Mkuu wetu lazima pia awe na kitu cha kutolea.
8:4b.HEB.008.004 Kama yeye angekuwa wa hapa duninani, asingekuwa kamwe kuhani, kwani wako makuhani wengine wanaotoa sadaka kufuatana na Sheria.
8:5b.HEB.008.005 Huduma zao za kikuhani ni mfano tu na kivuli cha yale yaliyoko mbinguni. Ndivyo pia ilivyokuwa kwa Mose. Wakati alipokuwa karibu kuitengeneza ile hema, Mungu alimwambia: "Tengeneza kila kitu kufuatana na ule mfano ulioonyeshwa kule mlimani."
8:6b.HEB.008.006 Lakini sasa Yesu amepewa huduma ya kikuhani iliyo bora zaidi kuliko yao, kama vile agano alilothibitisha kati ya watu na Mungu ni bora zaidi, kwani lina msingi wake katika ahadi za mambo yaliyo bora zaidi.
8:7b.HEB.008.007 Maana kama lile agano la kwanza halingalikuwa na dosari, hakungalikuwa na haja ya agano la pili.
8:8b.HEB.008.008 Lakini Mungu aliwalaumu watu wake aliposema: "Siku zinakuja, asema Bwana, ambapo nitafanya agano jipya na watu wa Israeli na kabila la Yuda.
8:9b.HEB.008.009 Agano hili halitakuwa kama lile nililofanya na babu zao siku ile nilipowaongoza kwa mkono kutoka nchi ya Misri. Hawakuwa waaminifu kwa agano langu; na hivyo mimi sikuwajali, asema Bwana.
8:10b.HEB.008.010 Na hili ndilo agano nitakalofanya na watu wa Israeli siku zijazo, asema Bwana: Nitaweka sheria zangu akilini mwao, na kuziandika mioyoni mwao. Mimi nitakuwa Mungu wao, nao watakuwa watu wangu.
8:11b.HEB.008.011 Hakuna mtu atakayemfundisha mwananchi mwenzake, wala atakayemwambia ndugu yake: Mjue Bwana. Maana watu wote, wadogo na wakubwa, watanijua mimi.
8:12b.HEB.008.012 Nitawasamehe makosa yao, wala sitakumbuka tena dhambi zao."
8:13b.HEB.008.013 Kwa kusema juu ya agano jipya, Mungu alilichakaza lile la kwanza; na chochote kinachochakaa na kuwa kikuukuu kitatoweka karibuni.
9
9:1b.HEB.009.001 Agano la kwanza lilikuwa na taratibu zake za ibada na pia mahali patakatifu pa ibada palipojengwa na watu.
9:2b.HEB.009.002 Palitengenezwa hema ambayo sehemu yake ya nje iliitwa Mahali Patakatifu. Humo mlikuwa na kinara cha taa, meza na mikate iliyotolewa kwa Mungu.
9:3b.HEB.009.003 Nyuma ya pazia la pili, kulikuwa na hema iliyoitwa Mahali Patakatifu Kupita Pote.
9:4b.HEB.009.004 Humo mlikuwa na madhabahu ya dhahabu kwa ajili ya kufukizia ubani, na Sanduku la Agano, ambalo lilikuwa limepakwa dhahabu pande zote, na ndani yake mlikuwa na chungu cha dhahabu kilichokuwa na mana; fimbo ya Aroni iliyokuwa imechanua majani, na vile vibao viwili vilivyoandikwa agano.
9:5b.HEB.009.005 Juu ya hilo Sanduku kulikuwa na viumbe vilivyodhihirisha kuweko kwa Mungu, na mabawa yao yalitanda juu ya mahali ambapo dhambi huondolewa. Lakini sasa, hatuwezi kusema kinaganaga juu ya mambo hayo.
9:6b.HEB.009.006 Mipango hiyo ilitekelezwa kisha ikawa desturi kwa makuhani kuingia kila siku katika hema ya nje kutoa huduma zao.
9:7b.HEB.009.007 Lakini kuhani Mkuu peke yake ndiye anayeingia katika lile hema la pili; naye hufanya hivyo mara moja tu kwa mwaka. Anapoingia ndani huwa amechukua damu ambayo anamtolea Mungu kwa ajili yake mwenyewe na kwa ajili ya dhambi ambazo watu wamezitenda bila wao wenyewe kujua.
9:8b.HEB.009.008 Kutokana na taratibu hizo Roho Mtakatifu anafundisha wazi kwamba wakati ile hema ya nje ingali ipo imesimama, njia ya kuingia Mahali Patakatifu haijafunguliwa.
9:9b.HEB.009.009 Jambo hili ni mfano wa nyakati za sasa. Linaonyesha kwamba zawadi na dhabihu zinazotolewa kwa Mungu haziwezi kuifanya mioyo ya wale wanaoabudu kuwa mikamilifu,
9:10b.HEB.009.010 kwani haya yote yanahusika na vyakula, vinywaji na taratibu mbalimbali za kutawadha. Yote hayo ni maagizo ya njenje tu; na nguvu yake hukoma wakati Mungu atakaporekebisha vitu vyote.
9:11b.HEB.009.011 Lakini Kristo amekwisha fika, akiwa Kuhani Mkuu wa mambo yaliyo mema, ambayo sasa yamekwisha fika. Yeye anatoa huduma zake katika hema iliyo bora na kamilifu zaidi, isiyofanywa kwa mikono ya watu, yaani isiyo ya ulimwengu huu ulioumbwa.
9:12b.HEB.009.012 Yeye aliingia Mahali Patakatifu mara moja tu, tena hakuwa amechukua damu ya mbuzi wala ng'ombe, bali aliingia kwa damu yake yeye mwenyewe, akatupatia ukombozi wa milele.
9:13b.HEB.009.013 Watu waliokuwa najisi kidini waliweza kutakasika na kuwa safi waliponyunyiziwa damu ya mbuzi na ya ng'ombe pamoja na majivu ya ndama.
9:14b.HEB.009.014 Lakini, kwa damu ya Kristo, mambo makuu zaidi hufanyika! Kwa nguvu za Roho wa milele, Kristo alijitolea mwenyewe dhabihu kamilifu kwa Mungu. Damu yake itatutakasa dhamiri zetu kutokana na matendo yaletayo kifo, ili tupate kumtumikia Mungu aliye hai.
9:15b.HEB.009.015 Kwa hiyo, Kristo ndiye aliyeratibisha agano jipya ili wale walioitwa na Mungu wazipokee baraka za milele walizoahidiwa. Watazipata, kwani kifo kimetokea ambacho huwakomboa watu kutoka yale makosa waliyofanya wakati wa lile agano la kale.
9:16b.HEB.009.016 Kwa kawaida wosia hutambuliwa tu kama kifo cha yule aliyeufanya huo wosia kimethibitishwa.
9:17b.HEB.009.017 Wosia hauwezi kutekelezwa mpaka kumetokea kifo, kwani wosia hauna maana ikiwa mwenye kuufanya bado anaishi.
9:18b.HEB.009.018 Ndiyo maana hata lile agano la kwanza halikuwekwa bila damu kumwagwa.
9:19b.HEB.009.019 Kwanza Mose aliwatangazia watu wote amri zote kama ilivyokuwa katika Sheria; kisha akachukua damu ya ndama pamoja na maji, na kwa kutumia majani ya mti uitwao husopo na pamba nyekundu, akakinyunyizia kile kitabu cha Sheria na hao watu wote.
9:20b.HEB.009.020 Mose alisema: "Hii ni damu inayothibitisha agano mliloamriwa na Mungu mlitii."
9:21b.HEB.009.021 Vilevile Mose aliinyunyizia damu ile hema na vyombo vya ibada.
9:22b.HEB.009.022 Naam, kadiri ya Sheria karibu kila kitu chaweza kutakaswa kwa damu, na dhambi nazo zaondolewa tu ikiwa damu imemwagwa.
9:23b.HEB.009.023 Vitu hivi ambavyo ni mfano tu wa mambo halisi ya mbinguni, vililazimika kutakaswa kwa namna hiyo. Lakini vitu vya mbinguni huhitaji dhabihu iliyo bora zaidi.
9:24b.HEB.009.024 Maana Kristo hakuingia Mahali Patakatifu palipojengwa kwa mikono ya watu, ambapo ni mfano tu wa kile kilicho halisi. yeye aliingia mbinguni kwenyewe ambako sasa anasimama mbele ya Mungu kwa ajili yetu.
9:25b.HEB.009.025 Kuhani Mkuu wa Wayahudi huingia Mahali Patakatifu kila mwaka akiwa amechukua damu ya mnyama; lakini Kristo hakuingia humo ili ajitoe mwenyewe mara nyingi,
9:26b.HEB.009.026 maana ingalikuwa hivyo, Kristo angalipaswa kuteswa mara nyingi tangu kuumbwa ulimwengu. Lakini sasa nyakati hizi zinapokaribia mwisho wake, yeye ametokea mara moja tu, kuondoa dhambi kwa kujitoa yeye mwenyewe dhabihu.
9:27b.HEB.009.027 Basi, kama vile kila mtu hufa mara moja tu, kisha husimama mbele ya hukumu ya Mungu,
9:28b.HEB.009.028 vivyo hivyo Kristo naye alijitoa dhabihu mara moja tu kwa ajili ya kuziondoa dhambi za wengi. Atakapotokea mara ya pili si kwa ajili ya kupambana na dhambi, bali ni kwa ajili ya kuwaokoa wale wanaomngojea.
10
10:1b.HEB.010.001 Sheria ya Wayahudi si picha kamili ya mambo yale halisi: ni kivuli tu cha mema yanayokuja. Dhabihu zilezile hutolewa daima, mwaka baada ya mwaka. Sheria yawezaje, basi, kwa njia ya dhabihu hizo, kuwafanya wale wanaoabudu wawe wakamilifu?
10:2b.HEB.010.002 Kama hao watu wanaomwabudu Mungu wangekuwa wametakaswa dhambi zao kweli, hawangejisikia tena kuwa na dhambi, na dhabihu hizo zote zingekoma.
10:3b.HEB.010.003 Lakini dhabihu hizo hufanyika kila mwaka kuwakumbusha watu dhambi zao.
10:4b.HEB.010.004 Maana damu ya fahali na mbuzi haiwezi kamwe kuondoa dhambi.
10:5b.HEB.010.005 Ndiyo maana Kristo alipokuwa anakuja ulimwenguni, alimwambia Mungu: "Hukutaka dhabihu wala sadaka, lakini umenitayarishia mwili.
10:6b.HEB.010.006 Sadaka za kuteketezwa au za kuondoa dhambi hazikupendezi.
10:7b.HEB.010.007 Hapo nikasema: Niko hapa ee Mungu, tayari kufanya mapenzi yako kama ilivyoandikwa juu yangu katika kitabu cha Sheria."
10:8b.HEB.010.008 Kwanza alisema: "Hutaki, wala hupendezwi na dhabihu na sadaka, sadaka za kuteketezwa na za kuondoa dhambi." Alisema hivyo ingawa sadaka hizi zote hutolewa kufuatana na Sheria.
10:9b.HEB.010.009 Kisha akasema: "Niko hapa, ee Mungu, tayari kufanya mapenzi yako." Hivyo Mungu alibatilisha dhabihu za zamani na mahali pake akaweka dhabihu nyingine moja.
10:10b.HEB.010.010 Kwa kuwa Yesu Kristo alitimiza mapenzi ya Mungu, sisi tunatakaswa dhambi zetu kwa ile dhabihu ya mwili wake aliyotoa mara moja tu, ikatosha.
10:11b.HEB.010.011 Kila kuhani Myahudi humhudumia Mungu kila siku, akitoa dhabibu zilezile mara nyingi, dhabibu ambazo haziwezi kuondoa dhambi.
10:12b.HEB.010.012 Lakini Kristo alitoa dhabihu moja tu kwa ajili ya dhambi, dhabihu ifaayo milele, kisha akaketi upande wa kulia wa Mungu.
10:13b.HEB.010.013 Huko anangoja mpaka adui zake watakapowekwa kama kibao chini ya miguu yake.
10:14b.HEB.010.014 Basi, kwa dhabihu yake moja tu, amewafanya kuwa wakamilifu milele wale wanaotakaswa dhambi zao.
10:15b.HEB.010.015 Naye Roho Mtakatifu anatupa ushahidi wake. Kwanza anasema:
10:16b.HEB.010.016 "Hili ndilo agano nitakalofanya nao, katika siku zijazo, asema Bwana: Nitaweka sheria zangu mioyoni mwao, na kuziandika akilini mwao."
10:17b.HEB.010.017 Kisha akaongeza kusema: "Sitakumbuka tena dhambi zao, wala vitendo vyao vya uhalifu."
10:18b.HEB.010.018 Basi, dhambi zikisha ondolewa, hakutakuwa na haja tena ya kutoa dhabihu za kuondoa dhambi.
10:19b.HEB.010.019 Basi, ndugu, kwa damu ya Yesu tunapewa moyo thabiti wa kuingia Mahali Patakatifu.
10:20b.HEB.010.020 Yeye ametufungulia njia mpya na yenye uzima kupitia lile pazia, yaani kwa njia ya mwili wake mwenyewe.
10:21b.HEB.010.021 Basi, tunaye kuhani maarufu aliye na mamlaka juu ya nyumba ya Mungu.
10:22b.HEB.010.022 Kwa hiyo tumkaribie Mungu kwa moyo mnyofu na imani timilifu, kwa mioyo iliyotakaswa dhamiri mbaya, na kwa miili iliyosafishwa kwa maji safi.
10:23b.HEB.010.023 Tushikilie imara tumaini lile tunalokiri, maana Mungu aliyefanya ahadi zake ni mwaminifu.
10:24b.HEB.010.024 Tujitahidi kushughulikiana kwa ajili ya kuongezeana bidii ya kupendana na kutenda mema.
10:25b.HEB.010.025 Tusiache ile desturi ya kukutana pamoja, kama vile wengine wanavyofanya. Bali tunapaswa kusaidiana kwani, kama mwonavyo, Siku ile ya Bwana inakaribia.
10:26b.HEB.010.026 Maana, tukiendelea kutenda dhambi makusudi baada ya kufahamu ukweli, hakuna dhabihu iwezayo kutolewa tena kwa ajili ya kuondoa dhambi.
10:27b.HEB.010.027 Linalobaki ni kungojea tu kwa hofu hukumu ya Mungu na moto mkali utakaowaangamiza wote wanaompinga.
10:28b.HEB.010.028 Mtu yeyote asiyeitii Sheria ya Mose, huuawa bila ya huruma kukiwa na ushahidi wa watu wawili au watatu.
10:29b.HEB.010.029 Je, mtu yule anayempuuza Mwana wa Mungu na kuidharau damu ya agano la Mungu iliyomtakasa, mtu anayemtukana Roho wa Mungu, anastahili kupata adhabu kali ya namna gani?
10:30b.HEB.010.030 Maana tunamfahamu yule aliyesema, "Mimi nitalipiza kisasi, mimi nitalipiza," na ambaye alisema pia, "Bwana atawahukumu watu wake."
10:31b.HEB.010.031 Kuanguka mikononi mwa Mungu aliye hai ni jambo la kutisha mno!
10:32b.HEB.010.032 Kumbukeni yaliyotokea siku zile za kwanza mlipoangaziwa mwanga wa Mungu. Ingawa siku zile mlipatwa na mateso mengi, ninyi mlistahimili.
10:33b.HEB.010.033 Mara nyingine mlitukanwa na kufedheheshwa hadharani; mara nyingine mlikuwa radhi kuungana na wale walioteswa namna hiyohiyo.
10:34b.HEB.010.034 Mlishiriki mateso ya wafungwa, na mliponyang'anywa mali yenu mlistahimili kwa furaha, maana mlijua kwamba mnayo mali bora zaidi na ya kudumu milele.
10:35b.HEB.010.035 Basi, msipoteze uhodari wenu, maana utawapatieni tuzo kubwa.
10:36b.HEB.010.036 Mnahitaji kuwa na uvumilivu, ili mweze kufanya anayotaka Mungu na kupokea kile alichoahidi.
10:37b.HEB.010.037 Maana kama yasemavyo Maandiko: "Bado kidogo tu, na yule anayekuja, atakuja, wala hatakawia.
10:38b.HEB.010.038 Lakini mtu wangu aliye mwadilifu ataamini na kuishi; walakini akirudi nyuma, mimi sitapendezwa naye."
10:39b.HEB.010.039 Basi, sisi hatumo miongoni mwa wale wanaorudi nyuma na kupotea, ila sisi tunaamini na tunaokolewa.
11
11:1b.HEB.011.001 Kuwa na imani ni kuwa na hakika ya mambo tunayotumainia; kusadiki kabisa mambo tusiyoyaona.
11:2b.HEB.011.002 Maana wazee wa kale walipata kibali cha Mungu kwa sababu ya imani yao.
11:3b.HEB.011.003 Kwa imani sisi tunafahamu kwamba ulimwengu uliumbwa kwa neno la Mungu; vitu vinavyoonekana kutoka vitu visivyoonekana.
11:4b.HEB.011.004 Kwa imani Abeli alimtolea Mungu dhabihu iliyokuwa bora zaidi kuliko ile ya Kaini. Kwa imani yake alikubaliwa na Mungu kuwa mwadilifu; Mungu mwenyewe alizikubali sadaka zake. Kwa imani yake ingawa amekufa, bado ananena.
11:5b.HEB.011.005 Kwa imani Henoki alichukuliwa na Mungu, asipate kufa. Hakuonekana tena kwa sababu Mungu alikuwa amemchukua. Maandiko yasema kwamba kabla ya kuchukuliwa kwake, yeye alikuwa amempendeza Mungu.
11:6b.HEB.011.006 Basi, pasipo imani haiwezekani kumpendeza Mungu. Kwa maana kila mtu anayemwendea Mungu ni lazima aamini kwamba Mungu yuko, na kwamba huwatuza wale wanaomtafuta.
11:7b.HEB.011.007 Kwa imani Noa alionywa na Mungu juu ya mambo ya baadaye ambayo hakuweza kuyaona bado. Alimtii Mungu, akajenga ile safina ambamo aliokolewa yeye pamoja na jamaa yake. Kutokana na hayo ulimwengu ulihukumiwa, naye Noa akapokea uadilifu unaotokana na imani.
11:8b.HEB.011.008 Kwa imani Abrahamu alimtii Mungu alipoitwa aende katika nchi ambayo Mungu angempa iwe yake. Ingawa hakujua alikokuwa anakwenda, Abrahamu alihama.
11:9b.HEB.011.009 Kwa imani aliishi kama mgeni katika nchi aliyoahidiwa na Mungu. Aliishi huko katika hema kama walivyoishi Isaka na Yakobo, ambao pia walishiriki ahadi ileile.
11:10b.HEB.011.010 Maana Abrahamu alikuwa akingojea mji wenye misingi imara, mji ambao Mungu mwenyewe ndiye fundi aliyeubuni na kuujenga.
11:11b.HEB.011.011 Kwa imani hata Sara aliamini kwamba Mungu hutimiza ahadi zake, kwa hiyo akajaliwa kuchukua mimba ingawaje alikuwa amepita umri.
11:12b.HEB.011.012 Kwa hiyo, kutoka katika mtu huyo mmoja, Abrahamu, ambaye alikuwa kama amekufa, walitokea watu wengi wasiohesabika kama vile nyota za mbinguni na mchanga wa pwani.
11:13b.HEB.011.013 Watu hawa wote walikufa wakiwa na imani. Walikufa kabla ya kupokea mambo ambayo Mungu alikuwa ameahidi, lakini kwa mbali waliyaona, wakashangilia, na kukiri wazi kwamba wao walikuwa wageni na wakimbizi duniani.
11:14b.HEB.011.014 Watu wanaosema mambo kama hayo, huonyesha wazi kwamba wanaitafuta nchi yao wenyewe.
11:15b.HEB.011.015 Kama wangalikuwa wanaifikiria nchi walikotoka zamani, wangalipata nafasi ya kurudi huko.
11:16b.HEB.011.016 Lakini sasa wanataka nchi iliyo bora zaidi, yaani nchi ya mbinguni. Ndiyo maana Mungu haoni haya wakimwita yeye Mungu wao, kwa sababu yeye mwenyewe amekwisha watayarishia mji.
11:17b.HEB.011.017 Kwa imani, Abrahamu alimtoa mwanae Isaka sadaka wakati Mungu alipomjaribu. Huyo Abrahamu ndiye aliyekuwa amepokea ahadi ya Mungu, lakini, hata hivyo, alikubali kumtoa dhabihu mwanae wa pekee,
11:18b.HEB.011.018 ingawa Mungu alikuwa amemwambia: "Wazawa wako watatokana na Isaka."
11:19b.HEB.011.019 Abrahamu aliamini kwamba Mungu anaweza kuwafufua wafu: na kwa namna fulani kweli Abrahamu alimpata tena mwanae kutoka wafu.
11:20b.HEB.011.020 Kwa imani Isaka aliwabariki Yakobo na Esau, wapate baraka zitakazokuja baadaye.
11:21b.HEB.011.021 Kwa imani Yakobo alipokuwa karibu kufa, aliwabariki kila mmoja wa wana wa Yosefu, akamwabudu Mungu akiegemea ile fimbo yake.
11:22b.HEB.011.022 Kwa imani Yosefu alipokuwa karibu kufa, alinena juu ya kutoka kwa Waisraeli katika nchi ya Misri, na pia akawaachia maagizo kuhusu mifupa yake.
11:23b.HEB.011.023 Kwa imani wazazi wa Mose walimficha huyo mtoto kwa muda wa miezi mitatu baada ya kuzaliwa kwake. Walimwona kuwa ni mtoto mzuri, wala hawakuiogopa amri ya mfalme.
11:24b.HEB.011.024 Kwa imani Mose alipokuwa mtu mzima, alikataa kuitwa mwana wa binti Farao.
11:25b.HEB.011.025 Aliona ni afadhali kuteseka pamoja na watu wa Mungu kuliko kufurahia raha ya dhambi kwa kitambo kidogo.
11:26b.HEB.011.026 Alitambua kwamba kuteseka kwa ajili ya Masiha kuna faida kubwa zaidi kuliko utajiri wote wa nchi ya Misri, maana alikuwa anatazamia tuzo la baadaye.
11:27b.HEB.011.027 Kwa imani Mose alihama kutoka nchi ya Misri bila kuogopa hasira ya mfalme; na wala hakurudi nyuma, kwani alikuwa kama mtu aliyemwona yule Mungu asiyeonekana.
11:28b.HEB.011.028 Kwa imani aliadhimisha siku ya Pasaka, akaamuru damu inyunyizwe juu ya milango, ili yule Malaika Mwangamizi asiwaue wazaliwa wa kwanza wa Israeli.
11:29b.HEB.011.029 Kwa imani watu wa Israeli walivuka bahari ya Shamu, kana kwamba ilikuwa nchi kavu; lakini Wamisri walipojaribu kufanya hivyo walikufa maji.
11:30b.HEB.011.030 Kwa imani kuta za mji wa Yeriko zilianguka watu wa Israeli walipokwisha zunguka kwa muda wa siku saba.
11:31b.HEB.011.031 Kwa imani Rahabu aliyekuwa malaya hakuangamia pamoja na wale waliomwasi Mungu, kwa sababu aliwakaribisha wale wapelelezi.
11:32b.HEB.011.032 Basi, niseme nini zaidi? Wakati hauniruhusu kueleza juu ya Gedeoni, Baraki, Samsoni, Yeftha, Daudi, Samweli na manabii.
11:33b.HEB.011.033 Kwa imani hawa wote walipigana vita na wafalme, wakashinda. Walitenda mambo adili, wakapokea yale aliyoahidi Mungu. Walifunga vinywa vya simba,
11:34b.HEB.011.034 Walizima mioto mikali, waliepuka kuuawa kwa upanga. Walikuwa dhaifu lakini walipata nguvu. Walikuwa hodari katika vita wakashinda majeshi ya kigeni.
11:35b.HEB.011.035 Na, wanawake walioamini walirudishiwa wafu wao wakiwa wamefufuliwa. Baadhi yao walikataa kufunguliwa, wakateswa mpaka kufa ili wapate kufufuliwa na kuingia katika maisha bora zaidi.
11:36b.HEB.011.036 Wengine walidhihakiwa na kupigwa mijeledi, na wengine walifungwa minyororo na kutupwa gerezani.
11:37b.HEB.011.037 Walipigwa mawe, walipasuliwa vipandevipande, waliuawa kwa upanga. Walizungukazunguka wakiwa wamevaa ngozi za kondoo na ngozi za mbuzi, walikuwa watu maskini, walioteswa na kudhulumiwa.
11:38b.HEB.011.038 Ulimwengu haukustahili kuwa na watu hao. Walitangatanga jangwani na mlimani, wakaishi katika mashimo na mapango ya ardhi.
11:39b.HEB.011.039 Watu hawa wote walionekana kuwa mashujaa kwa sababu ya imani yao. Hata hivyo, hawakupokea yale ambayo Mungu aliwaahidia,
11:40b.HEB.011.040 maana Mungu alikuwa ameazimia mpango ulio bora zaidi kwa ajili yetu; yaani wao wangeufikia ukamilifu wakiwa pamoja nasi.
12
12:1b.HEB.012.001 Sisi tunalo kundi hili kubwa la mashahidi mbele yetu. Kwa hiyo tuondoe kila kizuizi kinachotuzuia, na dhambi ile inayotung'ang'ania. Tupige mbio kwa uvumilivu katika mashindano yaliyowekwa mbele yetu.
12:2b.HEB.012.002 Tumwelekee Yesu ambaye ndiye aliyeianzisha imani yetu na ambaye ataikamilisha. Kwa ajili ya furaha iliyokuwa inamngojea, yeye alivumilia kifo msalabani, bila kujali juu ya aibu yake, na sasa anaketi upande wa kulia wa kiti cha enzi cha Mungu.
12:3b.HEB.012.003 Fikirini juu ya mambo yaliyompata Yesu, jinsi alivyostahimili upinzani mkubwa kwa watu wenye dhambi. Basi, msife moyo, wala msikate tamaa.
12:4b.HEB.012.004 Maana katika kupambana na dhambi, ninyi hamjapigana mpaka kiasi cha kumwaga damu yenu.
12:5b.HEB.012.005 Je, mmesahau yale maneno ya kutia moyo ambayo Mungu anawataja ninyi kuwa wanawe? "Mwanangu, usidharau adhabu ya Bwana, wala usife moyo anapokukanya.
12:6b.HEB.012.006 Maana Bwana humwadhibu kila anayempenda, humpinga kila anayekubali kuwa mwanae."
12:7b.HEB.012.007 Vumilieni adhabu kwani ni mafundisho; Mungu huwatendea ninyi kama wanawe. Maana ni mwana gani asiyeadhibiwa na baba yake?
12:8b.HEB.012.008 Lakini msipoadhibiwa kama wana wengine, basi, ninyi si wanawe, bali ni wana haramu.
12:9b.HEB.012.009 Zaidi ya hayo sisi tunawaheshimu wazazi wetu waliotuzaa hata wanapotuadhibu. Basi, tunapaswa kumtii zaidi Baba yetu wa kiroho ili tupate kuishi.
12:10b.HEB.012.010 Wazazi wetu hapa duniani walituadhibu kwa muda, kama wao wenyewe walivyoona kuwa vema; lakini Mungu anatuadhibu kwa ajili ya faida yetu wenyewe, tupate kuushiriki utakatifu wake.
12:11b.HEB.012.011 Kuadhibiwa si jambo la kufurahisha bali la kuhuzunisha. Lakini wale waliofunzwa kuwa na nidhamu mwishowe watavuna tuzo la amani kutoka katika maisha adili!
12:12b.HEB.012.012 Basi, inueni mikono yenu inayolegea na kuimarisha magoti yenu yaliyo dhaifu.
12:13b.HEB.012.013 Endeleeni kutembea katika njia iliyonyoka, ili kile kilicholemaa kisiumizwe, bali kiponywe.
12:14b.HEB.012.014 Jitahidini kuishi kwa amani na watu wote. Ishini maisha ya utakatifu, kwa sababu hakuna mtu atakayemwona Bwana bila ya maisha kama hayo.
12:15b.HEB.012.015 Jitahidini sana mtu yeyote asije akapoteza neema ya Mungu. Muwe waangalifu ili mti mchungu usizuke kati yenu na kuwaua wengi kwa sumu yake.
12:16b.HEB.012.016 Jihadharini ili miongoni mwenu pasiwe na mtu mwasherati au mtu asiyemcha Mungu kama Esau, aliyeuza haki yake ya mzaliwa wa kwanza kwa mlo mmoja.
12:17b.HEB.012.017 Ninyi mnafahamu kwamba hata alipotaka kuipata tena ile baraka iliyokuwa yake, alikataliwa, maana hakupata tena nafasi ya kutubu, ingawa aliitafuta kwa machozi.
12:18b.HEB.012.018 Ninyi hamkuwasili mlimani Sinai, ambao unaweza kushikika kama walivyofanya watu wa Israeli, hamkufika kwenye moto uwakao, penye giza, tufani,
12:19b.HEB.012.019 mvumo wa tarumbeta na sauti ya maneno. Wale waliosikia sauti hiyo waliomba wasisikie tena neno jingine,
12:20b.HEB.012.020 kwani hawakuweza kustahimili amri iliyotolewa: "Atakayegusa mlima huu, hata kama ni mnyama, atapigwa mawe."
12:21b.HEB.012.021 Hayo yote yalionekana ya kutisha mno, hata Mose akasema, "Naogopa na kutetemeka."
12:22b.HEB.012.022 Lakini ninyi mmefika katika mlima wa Sioni, kwenye mji wa Mungu aliye hai. Mmefika Yerusalemu, mji wa mbinguni, ambapo wamekusanyika malaika elfu nyingi wasiohesabika.
12:23b.HEB.012.023 Mmefika kwenye kusanyiko kubwa la wazaliwa wa kwanza wa Mungu, ambao majina yao yameandikwa mbinguni. Mnasimama mbele ya Mungu aliye hakimu wa wote, na mbele ya roho za watu waadilifu waliofanywa kuwa wakamilifu.
12:24b.HEB.012.024 Mmefika kwa Yesu ambaye ameratibisha agano jipya, na ambaye damu yake iliyomwagika inasema mambo mema zaidi kuliko ile ya Abeli.
12:25b.HEB.012.025 Basi, jihadharini msije mkakataa kumsikiliza yeye ambaye anasema nanyi. Kama wale walikataa kumsikiliza yule aliyewaonya hapa duniani hawakuokoka, sisi tutawezaje kuokoka kama tukikataa kumsikiliza yule anayetuonya kutoka mbinguni?
12:26b.HEB.012.026 Wakati ule sauti ilitetemesha nchi, lakini sasa ameahidi: "Nitatetemesha nchi tena, lakini si nchi tu bali pia mbingu."
12:27b.HEB.012.027 Neno hili: "tena" linatuonyesha kwamba vitu vyote vilivyoumbwa vitatetemeshwa na kutoweka ili vibaki vile visivyotetemeshwa.
12:28b.HEB.012.028 Sisi basi, na tushukuru kwani tunapokea utawala usiotikisika. Tuwe na shukrani na kumwabudu Mungu kwa namna itakayompendeza, kwa ibada na hofu;
12:29b.HEB.012.029 maana Mungu wetu kweli ni moto mkali unaoteketeza.
13
13:1b.HEB.013.001 Endeleeni kupendana kidugu.
13:2b.HEB.013.002 Msisahau kuwakaribisha wageni; maana kwa kufanya hivyo watu wengine walipata kuwakaribisha malaika bila kujua.
13:3b.HEB.013.003 Wakumbukeni wale waliofungwa kana kwamba mmefungwa pamoja nao. Wakumbukeni wale wanaoteseka kana kwamba nanyi mnateseka kama wao.
13:4b.HEB.013.004 Ndoa inapaswa kuheshimiwa na watu wote, na haki zake zitekelezwe kwa uaminifu. Mungu atawahukumu waasherati na wazinzi.
13:5b.HEB.013.005 Msiwe watu wa kupenda fedha; toshekeni na vile vitu mlivyo navyo. Mungu mwenyewe amesema: "Sitakuacha kamwe, wala sitakutupa."
13:6b.HEB.013.006 Ndiyo maana tunathubutu kusema: "Bwana ndiye msaada wangu, sitaogopa. Binadamu atanifanya nini?"
13:7b.HEB.013.007 wakumbukeni viongozi wenu waliowatangazieni ujumbe wa Mungu. Fikirieni juu ya mwenendo wao, mkaige imani yao.
13:8b.HEB.013.008 Yesu Kristo ni yuleyule, jana, leo na milele.
13:9b.HEB.013.009 Msipeperushwe huku na huku kwa mafundisho tofauti ya kigeni. Neema ya Mungu ndiyo inayoimarisha roho zetu na wala si masharti juu ya chakula; masharti hayo hayakumsaidia kamwe mtu yeyote aliyeyafuata.
13:10b.HEB.013.010 Sisi tunayo madhabahu ambayo wale wanaotumikia bado katika hema la Wayahudi, hawana haki ya kula vitu vyake.
13:11b.HEB.013.011 Kuhani Mkuu wa Kiyahudi huleta damu ya wanyama katika Mahali Patakatifu na kuitoa dhabihu kwa ajili ya dhambi; lakini nyama za hao wanyama huteketezwa nje ya kambi.
13:12b.HEB.013.012 Ndiyo maana Yesu pia, kusudi apate kuwatakasa watu kwa damu yake mwenyewe, aliteswa na kufa nje ya mji.
13:13b.HEB.013.013 Basi, tumwendee huko nje ya kambi tukajitwike laana yake.
13:14b.HEB.013.014 Maana hapa duniani hatuna mji wa kudumu; lakini tunautafuta ule unaokuja.
13:15b.HEB.013.015 Basi, kwa njia ya Yesu, tumtolee Mungu dhabihu ya sifa daima, yaani sifa zinazotolewa na midomo inayoliungama jina lake.
13:16b.HEB.013.016 Msisahau kutenda mema na kusaidiana, maana hizi ndizo dhabihu zinazompendeza Mungu.
13:17b.HEB.013.017 Watiini viongozi wenu na kushika amri zao; wao huchunga roho zenu usiku na mchana, na watatoa ripoti ya utumishi wao mbele ya Mungu. Kama mkiwatii watafanya kazi zao kwa furaha, la sivyo, watazifanya kwa huzuni, na hiyo haitakuwa na faida kwenu.
13:18b.HEB.013.018 Tuombeeni na sisi. Tuna hakika kwamba tunayo dhamiri safi, maana twataka kufanya lililo sawa daima.
13:19b.HEB.013.019 Nawasihi sana mniombee ili Mungu anirudishe kwenu upesi iwezekanavyo.
13:20b.HEB.013.020 Mungu amemfufua Bwana wetu Yesu Kristo ambaye ni Mchungaji Mkuu wa kondoo kwa sababu ya kumwaga damu yake iliyothibitisha agano la milele.
13:21b.HEB.013.021 Mungu wa amani awakamilishe katika kila tendo jema ili mtekeleze mapenzi yake; yeye na afanye ndani yetu kwa njia ya Kristo yale yanayompendeza mwenyewe. Utukufu uwe kwake, milele na milele! Amina.
13:22b.HEB.013.022 Basi, ndugu, nawasihi mpokee kwa utulivu ujumbe huu wa kuwatieni moyo. Hii ni barua fupi tu ambayo nimewaandikieni.
13:23b.HEB.013.023 Napenda kuwajulisheni kwamba ndugu yetu Timotheo amekwisha funguliwa gerezani. Kama akifika hapa mapema, nitakuja naye nitakapokuja kwenu.
13:24b.HEB.013.024 Wasalimieni viongozi wenu wote pamoja na watu wa Mungu! Ndugu wa Italia wanawasalimuni.
13:25b.HEB.013.025 Tunawatakieni nyote neema ya Mungu.
- Holder of rights
- Multilingual Bible Corpus
- Citation Suggestion for this Object
- TextGrid Repository (2025). Swahili Collection. Hebrews (Swahili). Hebrews (Swahili). Multilingual Parallel Bible Corpus. Multilingual Bible Corpus. https://hdl.handle.net/21.11113/0000-0016-B9A5-D