Galatians (Swahili)

Galatians (Swahili)

1

1:1b.GAL.001.001 Mimi Paulo mtume,

1:2b.GAL.001.002 na ndugu wote walio pamoja nami, tunayaandikia makanisa yaliyoko Galatia. Mimi nimepata kuwa mtume si kutokana na mamlaka ya binadamu, wala si kwa nguvu ya mtu, bali kwa uwezo wa Yesu Kristo na wa Mungu Baba aliyemfufua Yesu kutoka wafu.

1:3b.GAL.001.003 Tunawatakieni neema na amani kutoka kwa Mungu Baba yetu na kutoka kwa Bwana Yesu Kristo.

1:4b.GAL.001.004 Kristo alijitoa mwenyewe kwa ajili ya dhambi zetu kufuatana na mapenzi ya Mungu wetu na Baba, ili apate kutuokoa katika ulimwengu huu mbaya wa sasa.

1:5b.GAL.001.005 Kwake yeye uwe utukufu milele! Amina.

1:6b.GAL.001.006 Nashangaa kwamba muda mfupi tu umepita, nanyi mnamwasi yule aliyewaita kwa neema ya Kristo, mkafuata Habari Njema ya namna nyingine.

1:7b.GAL.001.007 Lakini hakuna "Habari Njema" nyingine. Ukweli ni kwamba wako watu wanaowavurugeni, watu wanaotaka kuipotosha Habari Njema ya Kristo.

1:8b.GAL.001.008 Lakini, hata kama mmoja wetu au malaika kutoka mbinguni, atawahubirieni Habari Njema tofauti na ile tuliyowahubirieni sisi, basi huyo na alaaniwe!

1:9b.GAL.001.009 Tulikwisha sema, na sasa nasema tena: kama mtu yeyote anawahubirieni Habari Njema ya aina nyingine, tofauti na ile mliyokwisha pokea, huyo na alaaniwe!

1:10b.GAL.001.010 Sasa nataka kibali cha nani: cha binadamu, ama cha Mungu? Au je, nataka kuwapendeza watu? Kama ningefanya hivyo, mimi singekuwa kamwe mtumishi wa Kristo.

1:11b.GAL.001.011 Ndugu, napenda mfahamu kwamba ile Habari Njema niliyoihubiri si ujumbe wa kibinadamu.

1:12b.GAL.001.012 Wala mimi sikuipokea kutoka kwa binadamu, wala sikufundishwa na mtu. Yesu Kristo mwenyewe ndiye aliyenifunulia.

1:13b.GAL.001.013 Bila shaka mlikwisha sikia jinsi nilivyokuwa ninaishi zamani kwa kuzingatia dini ya Kiyahudi, na jinsi nilivyolitesa kanisa la Mungu kupita kiasi na kutaka kuliharibu kabisa.

1:14b.GAL.001.014 Naam, mimi niliwashinda wengi wa wananchi wenzangu wa rika langu katika kuizingatia dini ya Kiyahudi, nikajitahidi sana kuyashika mapokeo ya wazee wetu.

1:15b.GAL.001.015 Lakini Mungu, kwa neema yake, alikuwa ameniteua hata kabla sijazaliwa, akaniita nimtumikie.

1:16b.GAL.001.016 Mara tu alipoamua kunifunulia Mwanae kusudi niihubiri Habari Njema yake kwa watu wa mataifa mengine, bila kutafuta maoni ya binadamu,

1:17b.GAL.001.017 na bila kwenda kwanza Yerusalemu kwa wale waliopata kuwa mitume kabla yangu, nilikwenda kwanza Arabia, kisha nikarudi tena Damasko.

1:18b.GAL.001.018 Ilikuwa tu baada ya miaka mitatu, ndipo nilipokwenda Yerusalemu kuonana na Kefa; nilikaa kwake siku kumi na tano.

1:19b.GAL.001.019 Lakini sikuwaona mitume wengine isipokuwa Yakobo, ndugu yake Bwana.

1:20b.GAL.001.020 Haya ninayowaandikieni, Mungu anajua; sisemi uongo.

1:21b.GAL.001.021 Baadaye nilikwenda katika tarafa za Siria na Kilikia.

1:22b.GAL.001.022 Wakati huo, mimi binafsi sikujulikana kwa jumuiya za Wakristo kule Yudea.

1:23b.GAL.001.023 Walichokuwa wanajua ni kile tu walichosikia: "Mtu yule aliyekuwa akitutesa hapo awali, sasa anaihubiri imani ileile aliyokuwa anajaribu kuiangamiza."

1:24b.GAL.001.024 Basi, wakamtukuza Mungu kwa sababu yangu.

2

2:1b.GAL.002.001 Baada ya miaka kumi na minne, nilikwenda tena Yerusalemu pamoja na Barnaba; nilimchukua pia Tito pamoja nami.

2:2b.GAL.002.002 Kwenda kwangu kulitokana na ufunuo alionipa Mungu. Katika kikao cha faragha niliwaeleza hao viongozi ujumbe wa Habari Njema niliohubiri kwa watu wa mataifa. Nilifanya hivyo kusudi kazi yangu niliyokuwa nimefanya, na ile ninayofanya sasa isije ikawa bure.

2:3b.GAL.002.003 Lakini, hata mwenzangu Tito, ambaye ni Mgiriki, hakulazimika kutahiriwa,

2:4b.GAL.002.004 ingawa kulikuwa na ndugu wengine wa uongo waliotaka atahiriwe. Watu hawa walijiingiza kwa ujanja na kupeleleza uhuru wetu tulio nao katika kuungana na Kristo Yesu, ili wapate kutufanya watumwa.

2:5b.GAL.002.005 Hatukukubaliana nao hata kidogo ili ukweli wa Habari Njema ubaki nanyi daima.

2:6b.GAL.002.006 Lakini watu hawa wanaosemekana kuwa ni viongozi--kama kweli walikuwa hivyo au sivyo, kwangu si kitu, maana Mungu hahukumu kwa kuangalia mambo ya nje--watu hawa hawakuwa na kitu cha kuongeza katika Habari hii Njema kama niihubirivyo.

2:7b.GAL.002.007 Badala yake, walitambua kwamba Mungu alikuwa amenituma kuhubiri Habari Njema kwa watu wa mataifa mengine kama vile Petro alivyokuwa ametumwa kuihubiri kwa Wayahudi.

2:8b.GAL.002.008 Maana, yule aliyemwezesha Petro kuwa mtume kwa Wayahudi, ndiye aliyeniwezesha nami pia kuwa mtume kwa watu wa mataifa mengine.

2:9b.GAL.002.009 Basi, Yakobo, Kefa na Yohane, ambao waonekana kuwa viongozi wakuu, walitambua kwamba Mungu alinijalia neema hiyo, wakatushika sisi mkono, yaani Barnaba na mimi, iwe ishara ya ushirikiano. Sisi ilitupasa tukafanye kazi kati ya watu wa mataifa mengine, na wao kati ya Wayahudi.

2:10b.GAL.002.010 Wakatuomba lakini kitu kimoja: tuwakumbuke maskini; jambo ambalo nimekuwa nikijitahidi kutekeleza.

2:11b.GAL.002.011 Lakini Kefa alipofika Antiokia nilimpinga waziwazi maana alikuwa amekosea.

2:12b.GAL.002.012 Awali, kabla ya watu kadhaa waliokuwa wametumwa na Yakobo kuwasili hapo, Petro alikuwa akila pamoja na watu wa mataifa mengine. Lakini, baada ya hao watu kufika, aliacha kabisa kula pamoja na watu wa mataifa mengine, kwa kuogopa kikundi cha waliosisitiza tohara.

2:13b.GAL.002.013 Hata ndugu wengine Wayahudi walimuunga mkono Petro katika kitendo hiki cha unafiki, naye Barnaba akakumbwa na huo unafiki wao.

2:14b.GAL.002.014 Basi, nilipoona kuwa msimamo wao kuhusu ukweli wa Habari Njema haukuwa umenyooka, nikamwambia Kefa mbele ya watu wote: "Ingawa wewe ni Myahudi, unaishi kama watu wa mataifa mengine na si kama Myahudi! Unawezaje, basi kujaribu kuwalazimisha watu wa mataifa mengine kuishi kama Wayahudi?"

2:15b.GAL.002.015 Kweli, sisi kwa asili ni Wayahudi, na si watu wa mataifa mengine hao wenye dhambi!

2:16b.GAL.002.016 Lakini, tunajua kwa hakika kwamba mtu hawezi kukubaliwa kuwa mwadilifu kwa kuitii Sheria, bali tu kwa kumwamini Yesu Kristo. Na sisi pia tumemwamini Yesu Kristo ili tupate kukubaliwa kuwa waadilifu kwa njia ya imani yetu kwa Kristo, na si kwa kuitii Sheria.

2:17b.GAL.002.017 Sasa, ikiwa katika kutafuta kukubaliwa kuwa waadilifu kwa kuungana na Kristo sisi tunaonekana kuwa wenye dhambi, je, jambo hili lina maana kwamba Kristo anasaidia utendaji wa dhambi? Hata kidogo!

2:18b.GAL.002.018 Lakini ikiwa ninajenga tena kile nilichokwisha bomoa, basi nahakikisha kwamba mimi ni mhalifu.

2:19b.GAL.002.019 Maana, kuhusu Sheria hiyo, mimi nimekufa; Sheria yenyewe iliniua, nipate kuishi kwa ajili ya Mungu. Mimi nimeuawa pamoja na Kristo msalabani,

2:20b.GAL.002.020 na sasa naishi, lakini si mimi tena, bali Kristo anaishi ndani yangu. Maisha haya ninayoishi sasa naishi kwa imani, imani katika Mwana wa Mungu aliyenipenda hata akayatoa maisha yake kwa ajili yangu.

2:21b.GAL.002.021 Sipendi kuikataa neema ya Mungu. Kama mtu huweza kukubaliwa kuwa mwadilifu kwa njia ya Sheria, basi, Kristo alikufa bure!

3

3:1b.GAL.003.001 Enyi Wagalatia, mmekuwa wajinga kweli! Ni nani aliyewaloga? Habari juu ya kusulubiwa kwake Yesu Kristo ilielezwa waziwazi mbele ya macho yenu.

3:2b.GAL.003.002 Napenda kujua tu kitu kimoja kutoka kwenu: Je, mlipokea Roho wa Mungu kwa sababu ya kutimiza matakwa ya Sheria ama kwa sababu ya kuisikia na kuiamini Habari Njema?

3:3b.GAL.003.003 Je, mu wajinga kiasi hicho? Ninyi mlianza yote kwa msaada wa Roho je, mnataka sasa kumaliza kwa nguvu zenu wenyewe?

3:4b.GAL.003.004 Je, mambo yale yote yaliyowapata ninyi yamekuwa bure tu? Haiwezekani!

3:5b.GAL.003.005 Je, Mungu huwajalia Roho na kutenda miujiza kati yenu ati kwa sababu mnatimiza yanayotakiwa na sheria, ama kwa sababu mnasikia Habari Njema na kuiamini?

3:6b.GAL.003.006 Chukueni kwa mfano habari za Abrahamu: yeye alimwamini Mungu, naye Mungu akamkubali kuwa mwadilifu.

3:7b.GAL.003.007 Sasa basi jueni kwamba watu wenye kumwamini ndio walio watoto halisi wa Abrahamu.

3:8b.GAL.003.008 Maandiko Matakatifu yalionyesha kabla kwamba Mungu atawakubali watu wa mataifa kuwa waadilifu kwa njia ya imani. Hivyo Maandiko Matakatifu yalitangulia kumtangazia Abrahamu Habari Njema: "Katika wewe mataifa yote yatabarikiwa."

3:9b.GAL.003.009 Basi, wale walio na imani wanabarikiwa pamoja na Abrahamu aliyeamini.

3:10b.GAL.003.010 Lakini wote wanaotegemea tu kutimiza yanayotakiwa na Sheria, wako chini ya laana. Maana, Maandiko Matakatifu yasema: "Yeyote asiyeshika na kutimiza yote yaliyoandikwa katika kitabu cha Sheria, yuko chini ya laana."

3:11b.GAL.003.011 Ni dhahiri kwamba Sheria haiwezi kumfanya mtu akubaliwe kuwa mwadilifu; maana Maandiko Matakatifu yasema: "Mwadilifu kwa imani ataishi."

3:12b.GAL.003.012 Lakini Sheria haitegemei imani, ila Maandiko yasema: "Mwenye kutimiza yanayotakiwa na Sheria ataishi."

3:13b.GAL.003.013 Kristo alitukomboa kutoka katika laana ya Sheria kwa kujitwalia laana hiyo kwa ajili yetu; maana Maandiko yanasema: "Yeyote aliyetundikwa msalabani amelaaniwa."

3:14b.GAL.003.014 Jambo hili lilifanyika kusudi ile baraka aliyopewa Abrahamu iwashukie watu wa mataifa mengine kwa njia ya Kristo, na ili kwa imani, tumpokee yule Roho ambaye Mungu alituahidia.

3:15b.GAL.003.015 Ndugu, nitawapeni mfano kutoka maisha yetu ya kila siku. Fikirini juu ya mkataba kati ya watu wawili. Mkataba ukisha fanyika na kutiwa sahihi hapana mtu anayeuweka kando au kuuongezea kitu.

3:16b.GAL.003.016 Basi, Abrahamu alipewa ahadi, yeye pamoja na mzawa wake. Maandiko hayasemi: "Na wazawa wake," yaani wengi, bali yasema, "Na mzawa wake," yaani mmoja, naye ndiye Kristo.

3:17b.GAL.003.017 Ninachotaka kusema ni hiki: Mungu alifanya agano lake akalithibitisha; Sheria ambayo ilitokea miaka mia nne na thelathini baadaye, haiwezi kulitangua hilo agano wala kuibatilisha hiyo ahadi.

3:18b.GAL.003.018 Maana, kama urithi ya Mungu inategemea Sheria, basi, haiwezi kutegemea tena ahadi ya Mungu. Kumbe, lakini Mungu alimkirimia Abrahamu kwa sababu aliahidi.

3:19b.GAL.003.019 Ya nini basi, Sheria? Iliongezwa hapo ili kuonyesha uhalifu ni kitu gani, mpaka atakapokuja yule mzawa wa Abrahamu aliyepewa ile ahadi. Sheria ililetwa na malaika kwa mkono wa mpatanishi.

3:20b.GAL.003.020 Ama hakika, mpatanishi hahitajiwi ikiwa jambo lenyewe lamhusu mtu mmoja; na Mungu ni mmoja.

3:21b.GAL.003.021 Je, Sheria inapingana na ahadi za Mungu? Hata kidogo! Maana, kama kungalitolewa sheria ambayo ingeweza kuwapa watu uzima, basi, tungeweza kukubaliwa kuwa waadilifu kwa njia ya Sheria.

3:22b.GAL.003.022 Lakini sivyo; Maandiko Matakatifu yamekwisha sema kwamba ulimwengu wote upo chini ya utawala wa dhambi; na hivyo, kwa kumwamini Yesu Kristo, wenye kuamini watimiziwe ile ahadi.

3:23b.GAL.003.023 Kabla ya kujaliwa imani, Sheria ilitufanya wafungwa mpaka imani hiyo iliyokuwa inakuja ifunuliwe.

3:24b.GAL.003.024 Basi, hiyo Sheria ilikuwa kama mlezi wetu mpaka alipokuja Kristo, ili kwa njia ya imani, tukubaliwe kuwa waadilifu.

3:25b.GAL.003.025 Tangu kufika kwa hiyo imani, Sheria si mlezi wetu tena.

3:26b.GAL.003.026 Kwa njia ya imani, ninyi nyote mmekuwa watoto wa Mungu katika kuungana na Kristo.

3:27b.GAL.003.027 Ninyi nyote mliobatizwa mkaungana na Kristo ni kama vile mmemvaa Kristo.

3:28b.GAL.003.028 Hivyo, hakuna tena tofauti kati ya Myahudi na Mgiriki, mtumwa na mtu huru, mwanamume na mwanamke. Nyote ni kitu kimoja katika kuungana na Kristo Yesu.

3:29b.GAL.003.029 Ikiwa ninyi ni wa Kristo, basi ni wazawa wa Abrahamu, na mtapokea yale aliyoahidi Mungu.

4

4:1b.GAL.004.001 Basi, nasema hivi: mrithi, akiwa bado mtoto, hawi tofauti na mtumwa ingawaje mali yote ni yake.

4:2b.GAL.004.002 Wakati huo wote yuko chini ya walezi na wadhamini mpaka wakati ule uliowekwa na baba yake.

4:3b.GAL.004.003 Hali kadhalika na sisi tulipokuwa bado watoto, tulikuwa watumwa wa pepo watawala wa ulimwengu.

4:4b.GAL.004.004 Lakini wakati ule maalumu ulipotimia, Mungu alimtuma Mwanawe aliyezaliwa na mwanamke, akaishi chini ya Sheria

4:5b.GAL.004.005 apate kuwakomboa wale waliokuwa chini ya Sheria ili sisi tufanywe wana wa Mungu.

4:6b.GAL.004.006 Kwa vile sasa ninyi ni wana, Mungu amemtuma Roho wa Mwanae mioyoni mwenu, Roho ambaye hulia "Aba," yaani "Baba."

4:7b.GAL.004.007 Basi, wewe si mtumwa tena, bali mwana. Na ikiwa ni mwana, basi, wewe utapokea yote Mungu aliyowawekea watoto wake.

4:8b.GAL.004.008 Zamani hamkumjua Mungu na hivyo mkatumikia miungu isiyo miungu kweli.

4:9b.GAL.004.009 Lakini sasa, kwa vile mnamjua Mungu, au tuseme mnajulikana na Mungu, mnawezaje tena kurudi kwa wale pepo maskini na dhaifu hata kutaka kuwatumikia tena?

4:10b.GAL.004.010 Bado mnaadhimisha siku, miezi na miaka!

4:11b.GAL.004.011 Nahofu kwamba labda kazi niliyoifanya kwa ajili yenu imepotea bure!

4:12b.GAL.004.012 Ndugu, nawasihi muwe kama mimi, kwa vile hata mimi nimekuwa kama ninyi. Hamkunitendea ubaya wowote.

4:13b.GAL.004.013 Mnajua kwamba ugonjwa wangu ndio ulionipatia fursa ya kuwahubirieni Habari Njema kwa mara ya kwanza.

4:14b.GAL.004.014 Hata hivyo, wakati ule hamkunidharau wala kunikataa kwa sababu ya udhaifu wangu ingawa mlishawishiwa kufanya hivyo; lakini mlinipokea kama malaika wa Mungu, kama vile ningekuwa Kristo Yesu mwenyewe.

4:15b.GAL.004.015 Mlikuwa wenye furaha; sasa kumetokea nini? Naapa kwamba wakati ule mngaliweza hata kuyang'oa macho yenu na kunipa mimi.

4:16b.GAL.004.016 Je, sasa nimekuwa adui yenu kwa sababu ya kuwaambieni ukweli?

4:17b.GAL.004.017 Hao watu wengine wanawahangaikia ninyi, lakini nia zao si njema. Wanataka kuwatenganisha nami ili ninyi muwahangaikie wao.

4:18b.GAL.004.018 Kwa kweli ni jambo jema daima kuwahangaikia wengine katika mambo mema, na si tu wakati mimi nipo pamoja nanyi.

4:19b.GAL.004.019 Watoto wangu, kama vile mama mja mzito anavyotaabika wakati wa kujifungua, mimi nataabika tena kwa ajili yenu mpaka hapo hali yake Kristo itakapoundwa ndani yenu.

4:20b.GAL.004.020 Laiti ningekuwa pamoja nanyi sasa, maana ningalipata msimamo ufaao juu yenu! Nina wasiwasi sana nanyi!

4:21b.GAL.004.021 Niambieni, enyi mnaopenda kutawaliwa na sheria: Je, mnasikia isemavyo Sheria?

4:22b.GAL.004.022 Imeandikwa katika Maandiko Matakatifu kwamba Abrahamu alikuwa na watoto wawili: mmoja kwa mwanamke mtumwa, na wa pili kwa mwanamke huru.

4:23b.GAL.004.023 Yule wa mwanamke mtumwa alizaliwa kama kawaida, lakini yule wa mwanamke huru alizaliwa kutokana na ahadi ya Mungu.

4:24b.GAL.004.024 Mambo hayo yamekuwa mfano; mama hao wawili ni mfano wa maagano mawili; la kwanza ni lile lililofanyika mlimani Sinai, mwakilishi wake ni Hagari, na watoto wake wanazaliwa utumwani.

4:25b.GAL.004.025 Hagari anawakilisha mlima Sinai ulioko Arabia, na ni mfano wa Yerusalemu ya sasa, ulio mtumwa pamoja na watoto wake.

4:26b.GAL.004.026 Lakini Yerusalemu ya juu mbinguni ni mji ulio huru, nao ni mama yetu.

4:27b.GAL.004.027 Maana imeandikwa: "Furahi, ewe uliye tasa usiyezaa; paaza sauti wewe usiyepata kujifungua mtoto; maana watoto wa yule aliyeachwa ni wengi zaidi kuliko wa yule aliye na mume."

4:28b.GAL.004.028 Sasa, basi, ndugu zangu, ninyi ni watoto wa Mungu kutokana na ahadi yake kama alivyokuwa Isaka.

4:29b.GAL.004.029 Lakini kama vile siku zile yule mtoto aliyezaliwa kwa njia ya kawaida alimdhulumu yule aliyezaliwa kwa uwezo wa Roho wa Mungu, vivyo hivyo na siku hizi.

4:30b.GAL.004.030 Lakini Maandiko Matakatifu yasemaje? Yasema: "Mfukuze mama mtumwa pamoja na mwanawe; maana mtoto wa mtumwa hatarithi pamoja na mtoto wa mama huru."

4:31b.GAL.004.031 Kwa hiyo, basi, ndugu, sisi si watoto wa mtumwa bali wa mama huru.

5

5:1b.GAL.005.001 Kristo alitupa uhuru akataka tubaki huru. Basi, simameni imara wala msikubali tena kuwa chini ya nira ya utumwa.

5:2b.GAL.005.002 Sikilizeni! Ni mimi Paulo ninayesema nanyi! Kama mkikubali kutahiriwa, Kristo hatawafaidia chochote.

5:3b.GAL.005.003 Nasema tena wazi: kila anayekubali kutahiriwa itambidi kuishika Sheria yote.

5:4b.GAL.005.004 Kama mnatazamia kukubaliwa kuwa waadilifu kwa njia ya Sheria, basi, mmejitenga mbali na Kristo; mko nje ya neema ya Mungu.

5:5b.GAL.005.005 Kwa upande wetu, lakini, sisi tunatumaini kwamba kwa nguvu ya Roho tunakubaliwa kuwa waadilifu kwa njia ya imani.

5:6b.GAL.005.006 Maana ikiwa tumeungana na Kristo Yesu, kutahiriwa au kutotahiriwa hakuna maana; cha maana ni imani ifanyayo kazi kwa mapendo.

5:7b.GAL.005.007 Mwenendo wenu ulikuwa mzuri! Nani, basi aliyewazuia kuuzingatia ukweli?

5:8b.GAL.005.008 Aliyesababisha hali hiyo si Mungu ambaye amewaiteni.

5:9b.GAL.005.009 "chachu kidogo tu huchachusha donge lote la unga!"

5:10b.GAL.005.010 Kutokana na kuungana kwetu na Bwana, nina tumaini kubwa kwamba ninyi hamtakuwa na msimamo tofauti nami. Tena yeyote huyo anayewavurugeni--awe nani au nani--hakika ataadhibiwa.

5:11b.GAL.005.011 Na kwa upande wangu, ndugu zangu, kama bado ninahubiri kwamba kutahiriwa ni lazima, kwa nini basi, bado ninadhulumiwa? Kama ingalikuwa hivyo, mahubiri yangu juu ya msalaba wa Kristo yasingalileta aibu yoyote.

5:12b.GAL.005.012 Laiti hao wanaowavurugeni wangejikatakata wenyewe!

5:13b.GAL.005.013 Ninyi, ndugu, mliitwa muwe watu huru. Lakini uhuru huo usiwe kisingizio cha kutawaliwa na tamaa za kidunia; ila mnapaswa kutumikiana kwa upendo.

5:14b.GAL.005.014 Maana Sheria yote hutimizwa katika kushika amri hii moja: "Mpende jirani yako kama unavyojipenda mwenyewe."

5:15b.GAL.005.015 Lakini ikiwa mtaumana na kutafunana kama wanyama, jihadharini msije mkaangamizana wenyewe kwa wenyewe!

5:16b.GAL.005.016 Basi, nasema hivi: mwenendo wenu na uongozwe na Roho, nanyi hamtafuata tena tamaa za kidunia.

5:17b.GAL.005.017 Maana, tamaa za kidunia hupingana na matakwa ya Roho; na matakwa ya Roho hupingana na tamaa za kidunia. Mambo hayo mawili hayaafikiani; kwa sababu hiyo hamwezi kufanya yale mnayotaka ninyi wenyewe.

5:18b.GAL.005.018 Kama mkiongozwa na Roho, basi, hamko tena chini ya Sheria.

5:19b.GAL.005.019 Basi, matendo ya kidunia yanajulikana: uzinzi, uasherati, ufisadi;

5:20b.GAL.005.020 kuabudu sanamu, uchawi, uadui, ugomvi, wivu, hasira, choyo, mabishano, mafarakano;

5:21b.GAL.005.021 husuda, ulevi, ulafi na mambo mengine kama hayo. Nawaambieni tena kama nilivyokwisha sema: watu wanaotenda mambo hayo hawatakuwa na nafasi yao katika ufalme wa Mungu.

5:22b.GAL.005.022 Lakini matokeo ya kuongozwa na Roho ni mapendo, furaha, amani, uvumilivu, wema, fadhili, uaminifu,

5:23b.GAL.005.023 upole na kuwa na kiasi. Hakuna Sheria inayoweza kupinga mambo hayo.

5:24b.GAL.005.024 Wale walio wa Kristo wameisulubisha hali yao ya kidunia pamoja na mawazo yake mabaya na tamaa zake.

5:25b.GAL.005.025 Tukiishi kwa msaada wa Roho, na tuufuate mwongozo wake.

5:26b.GAL.005.026 Basi, tusijivune, tusichokozane wala kuoneana wivu.

6

6:1b.GAL.006.001 Ndugu, kama mkimwona mtu fulani amekosea, basi, ninyi mnaoongozwa na Roho mwonyeni mtu huyo ajirekebishe; lakini fanyeni hivyo kwa upole, mkiwa na tahadhari msije nanyi wenyewe mkajaribiwa.

6:2b.GAL.006.002 Saidianeni kubeba mizigo yenu na hivyo mtatimiza sheria ya Kristo.

6:3b.GAL.006.003 Mtu akijiona kuwa ni kitu, na kumbe si kitu, huyo anajidanganya mwenyewe.

6:4b.GAL.006.004 Lakini kila mmoja na aupime vizuri mwenendo wake mwenyewe. Ukiwa mwema, basi, anaweza kuona fahari juu ya alichofanya bila kuwa na sababu ya kujilinganisha na mtu mwingine.

6:5b.GAL.006.005 Maana kila mmoja anao mzigo wake mwenyewe wa kubeba.

6:6b.GAL.006.006 Mwenye kufundishwa neno la Mungu na amshirikishe mwalimu wake riziki zake.

6:7b.GAL.006.007 Msidanganyike; Mungu hafanyiwi dhihaka. Alichopanda mtu ndicho atakachovuna.

6:8b.GAL.006.008 Apandaye katika tamaa za kidunia, atavuna humo uharibifu; lakini akipanda katika Roho, atavuna kutoka kwa Roho uzima wa milele.

6:9b.GAL.006.009 Basi, tusichoke kutenda mema; maana tusipolegea tutavuna mavuno kwa wakati wake.

6:10b.GAL.006.010 Kwa hiyo, tukiwa bado na wakati, tuwatendee watu wote mema, na hasa ndugu wa imani yetu.

6:11b.GAL.006.011 Tazameni jinsi nilivyoandika kwa herufi kubwa, kwa mkono wangu mwenyewe.

6:12b.GAL.006.012 Wale wanaotaka kuonekana wazuri kwa mambo ya mwili ndio wanaotaka kuwalazimisha ninyi mtahiriwe. Wanafanya hivyo kwa sababu moja tu: kusudi wao wenyewe wasije wakadhulumiwa kwa sababu ya msalaba wa Kristo.

6:13b.GAL.006.013 Maana, hao wenyewe waliotahiriwa hawaishiki Sheria; huwataka ninyi mtahiriwe wapate kujivunia alama hiyo mwilini mwenu.

6:14b.GAL.006.014 Lakini mimi sitajivunia kamwe chochote isipokuwa msalaba wa Bwana wetu Yesu Kristo; maana kwa njia ya msalaba huo ulimwengu umesulubiwa kwangu, nami nimesulubiwa kwa ulimwengu.

6:15b.GAL.006.015 Kutahiriwa au kutotahiriwa si kitu; cha maana ni kuwa kiumbe kipya.

6:16b.GAL.006.016 Wanaoufuata mwongozo huo nawatakia amani na huruma; amani na huruma kwa Israeli--Wateule wa Mungu.

6:17b.GAL.006.017 Basi, sasa mtu yeyote asinisumbue tena, maana alama nilizo nazo mwilini mwangu ni zile za Yesu.

6:18b.GAL.006.018 Ndugu, nawatakieni ninyi nyote neema ya Bwana wetu Kristo. Amina.


Holder of rights
Multilingual Bible Corpus

Citation Suggestion for this Object
TextGrid Repository (2025). Swahili Collection. Galatians (Swahili). Galatians (Swahili). Multilingual Parallel Bible Corpus. Multilingual Bible Corpus. https://hdl.handle.net/21.11113/0000-0016-B98A-C