2 Corinthians (Swahili)

2 Corinthians (Swahili)

1

1:1b.2CO.001.001 Mimi Paulo, mtume wa Kristo Yesu kwa mapenzi ya Mungu, na ndugu Timotheo, tunawaandikia ninyi mlio kanisa la Mungu huko Korintho, na watu wote wa Mungu kila mahali katika Akaya.

1:2b.2CO.001.002 Tunawatakieni neema na amani kutoka kwa Mungu Baba yetu na Bwana Yesu Kristo.

1:3b.2CO.001.003 Atukuzwe Mungu na Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo, Baba mwenye huruma na Mungu mwenye kuleta faraja yote.

1:4b.2CO.001.004 Yeye hutufariji sisi katika taabu zetu zote, ili nasi tupate kuwafariji wengine katika kila taabu kwa faraja hiyohiyo tunayopokea kutoka kwa Mungu.

1:5b.2CO.001.005 Naam, kadiri mateso ya Kristo yanavyozidi ndani yetu, ni kadiri hiyohiyo tunazidi kufarijiwa naye.

1:6b.2CO.001.006 Ikiwa tunapata taabu, basi ni kwa ajili ya faraja na wokovu wenu. Tukifarijika, ni kwa ajili ya kuwafariji ninyi na kuwaunga mkono mpate nguvu ya kustahimili mateso yaleyale tunayoteseka sisi.

1:7b.2CO.001.007 Tena, matumaini tuliyo nayo kwa ajili yenu ni imara; tunajua kwamba mkishiriki mateso yetu, mtashiriki pia faraja yetu.

1:8b.2CO.001.008 Ndugu, tunataka kuwajulisheni taabu zilizotupata kule Asia; taabu hizo zilitulemea kupita kiasi, hata tukakata matumaini yote ya kuendelea kuishi.

1:9b.2CO.001.009 Naam, tulikuwa kama watu waliohukumiwa kuuawa, ili tufundishwe kumtegemea Mungu mwenye kuwafufua wafu, badala ya kutegemea nguvu zetu sisi wenyewe.

1:10b.2CO.001.010 Yeye alituokoa katika hatari kubwa ya kifo, na anaendelea kutuokoa; sisi tumemwekea tumaini letu kwamba atatuokoa tena,

1:11b.2CO.001.011 ninyi mkiwa mnatuunga mkono kwa kutuombea. Hivyo neema tutakazokuwa tumepata kutokana na maombi ya watu wengi hivyo, ziwe sababu ya watu wengi zaidi kumshukuru Mungu kwa ajili yetu.

1:12b.2CO.001.012 Sisi tunajivunia kitu kimoja: dhamiri yetu inatuhakikishia kwamba tumeishi ulimwenguni hapa, na hasa kati yenu, kwa unyenyekevu na unyofu tuliojaliwa na Mungu; hatukuongozwa na hekima ya kibinadamu bali neema ya Mungu.

1:13b.2CO.001.013 Tunawaandikia ninyi mambo mnayoweza kuyasoma na kuyaelewa. Ninatumaini kwamba mtaelewa vizuri kabisa,

1:14b.2CO.001.014 maana mpaka sasa mmenielewa kiasi fulani tu. Tunajua kwamba katika ile Siku ya Bwana Yesu mtaweza kutuonea sisi fahari kama nasi tunavyowaonea ninyi fahari.

1:15b.2CO.001.015 Nikiwa na matumaini hayo, nilikusudia kuja kwenu hapo awali ili mpate baraka maradufu.

1:16b.2CO.001.016 Nilikusudia kupita kwenu nikiwa safarini kwenda Makedonia, na wakati wa kurudi pia, ili nipate msaada wenu kwa safari yangu kwenda Yudea.

1:17b.2CO.001.017 Je, mnadhani nilipopanga hivyo nimekuwa kama mtu asiye na msimamo? Je, mnadhani kwamba ninafanya uamuzi wangu kwa fikira za kibinadamu na kwamba nasema "Ndiyo" na "Siyo" papo hapo?

1:18b.2CO.001.018 Mungu ni ukweli mtupu; basi, kile tulichowaambia ninyi si jambo la "Ndiyo" na "Siyo".

1:19b.2CO.001.019 Maana Kristo Yesu, Mwana wa Mungu, ambaye mimi, Silwano na Timotheo, tulimhubiri kwenu, hakuwa mtu wa "Ndiyo" na "Siyo"; bali yeye daima ni "Ndiyo" ya Mungu.

1:20b.2CO.001.020 Maana ndani yake ahadi zote za Mungu zimekuwa "Ndiyo". Kwa sababu hiyo, "Amina" yetu husemwa kwa njia ya Kristo kwa ajili ya kumtukuza Mungu.

1:21b.2CO.001.021 Mungu mwenyewe ndiye mwenye kutuimarisha sisi na ninyi pia katika Kristo, na ndiye anayetuweka wakfu;

1:22b.2CO.001.022 ndiye aliyetutia mhuri wa kuwa mali yake yeye na kutujalia Roho mioyoni mwetu kama dhamana ya mambo yote ambayo ametuwekea.

1:23b.2CO.001.023 Mungu ndiye shahidi wangu--yeye anajua moyo wangu! Mimi sikuja tena Korintho, kwa sababu tu ya kuwahurumieni.

1:24b.2CO.001.024 Hatutaki kutumia mabavu juu ya imani yenu; ninyi mko imara katika imani yenu. Wajibu wetu ni kufanya kazi pamoja kwa ajili ya furaha yenu.

2

2:1b.2CO.002.001 Basi nimeamua nisiwatembelee tena kuwatia huzuni.

2:2b.2CO.002.002 Maana nikiwahuzunisha ninyi, basi, ni nani atakayenifariji? Ni walewale niliowahuzunisha!

2:3b.2CO.002.003 Ndiyo maana niliwaandikia--sikutaka kuja kwenu na kuhuzunishwa na ninyi ambao ndio mngepaswa kuwa furaha yangu. Nina hakika kwamba, mimi nikifurahi, ninyi nyote pia mnafurahi.

2:4b.2CO.002.004 Nilipowaandikia hapo awali katika hali ya huzuni na sikitiko moyoni na kwa machozi mengi, haikuwa kwa ajili ya kuwahuzunisha ninyi, bali kwa ajili ya kuwaonyesheni kwamba nawapenda mno.

2:5b.2CO.002.005 Ikiwa kuna mtu aliyemhuzunisha mwingine, hakunihuzunisha mimi--ila amewahuzunisha ninyi nyote, na sipendi kuwa mkali zaidi.

2:6b.2CO.002.006 Adhabu aliyokwisha pata kutoka kwa wengi wenu inamtosha.

2:7b.2CO.002.007 Iliyobakia ni afadhali kwenu kumsamehe mtu huyo na kumpa moyo ili asije akahuzunika mno na kukata tamaa kabisa.

2:8b.2CO.002.008 Kwa hiyo nawasihi: mwonyesheni kwamba mnampenda.

2:9b.2CO.002.009 Madhumuni yangu kuandika ile barua yalikuwa kutaka kujua kama mko tayari kutii katika kila jambo.

2:10b.2CO.002.010 Mkimsamehe mtu, nami pia ninamsamehe. Maana ninaposamehe--kama kweli ninacho cha kusamehe--nasamehe mbele ya Kristo kwa ajili yenu,

2:11b.2CO.002.011 ili tusimpe nafasi Shetani atudanganye; maana twaijua mipango yake ilivyo.

2:12b.2CO.002.012 Nilipofika Troa kuhubiri Habari Njema ya Kristo, nilikuta mlango u wazi kwa ajili ya kazi ya Bwana.

2:13b.2CO.002.013 Lakini nilifadhaika sana kwa kutomkuta ndugu yetu Tito. Ndiyo maana niliwaaga wote pale nikaenda Makedonia.

2:14b.2CO.002.014 Lakini, shukrani kwa Mungu anayetuongoza daima katika msafara wa ushindi wa Kristo. Yeye hutufanya tuueneze ukweli wa Kristo kama harufu nzuri, kila mahali.

2:15b.2CO.002.015 Maana sisi ni kama harufu nzuri ya ubani ambayo Kristo anamtolea Mungu, harufu nzuri inayofikia wote wanaookolewa na wanaopotea.

2:16b.2CO.002.016 Kwa wale wanaopotea, harufu hiyo ni kifo; lakini kwa wale wanaookolewa, harufu hiyo ni uhai. Nani basi, awezaye kushiriki katika kazi ya namna hiyo?

2:17b.2CO.002.017 Sisi si kama wengine ambao hufanya biashara na ujumbe wa Mungu; sisi tunahubiri kwa unyofu mbele ya Mungu, kama watu tuliotumwa na Mungu, tukiwa tumeungana na Kristo.

3

3:1b.2CO.003.001 Je, tunaanza tena kujipendekeza? Je, tunahitaji barua ya utambulisho kwenu, au kutoka kwenu, kama watu wengine?

3:2b.2CO.003.002 Ninyi wenyewe ni barua yetu; barua iliyoandikwa mioyoni mwetu kila mtu aione na kuisoma.

3:3b.2CO.003.003 Ni dhahiri kwamba ninyi ni barua ya Kristo aliyoipeleka kwa mikono yetu. Barua yenyewe imeandikwa si kwa wino, bali kwa Roho wa Mungu hai; imeandikwa si juu ya kipande cha jiwe, bali juu ya mioyo ya watu.

3:4b.2CO.003.004 Tunaweza kusema hayo kwa sababu ya tumaini letu tulilo nalo kwa Mungu kwa njia ya Kristo.

3:5b.2CO.003.005 Si kwamba sisi tunaweza kufanya chochote kwa nguvu zetu wenyewe, ila uwezo wetu wote hutoka kwa Mungu:

3:6b.2CO.003.006 maana yeye ndiye aliyetuwezesha kulihudumia Agano Jipya ambalo si agano la sheria iliyoandikwa, bali Agano la Roho. Maana sheria iliyoandikwa huleta kifo, lakini Roho huleta uzima.

3:7b.2CO.003.007 Sheria iliwekwa kwa kuandikwa juu ya vipande vya mawe. Ingawaje mwisho wake umekuwa kifo, utukufu wake ulikuwa mkuu mno hata wana wa Israeli wasiweze kuutazama uso wa Mose kwa sababu ya mng'ao wake. Tena mng'ao huo ulikuwa wa muda tu. Basi, ikiwa huduma ya kile ambacho kimesababisha kifo imefanyika kwa utukufu mwingi kiasi hicho,

3:8b.2CO.003.008 basi, huduma ya Roho ina utukufu mkuu zaidi.

3:9b.2CO.003.009 Ikiwa basi, kulikuwa na utukufu katika huduma ile iliyoleta hukumu, ni wazi kwamba huduma ile iletayo kukubaliwa kuwa waadilifu itakuwa na utukufu mkuu zaidi.

3:10b.2CO.003.010 Sasa utukufu mkuu zaidi umechukua nafasi ya ule utukufu uliokuja hapo awali, ambao fahari yake imekwisha toweka.

3:11b.2CO.003.011 Maana ikiwa kile kilichokuwa cha muda tu kilikuwa na utukufu wake, bila shaka kile chenye kudumu milele kitakuwa na utukufu mkuu zaidi.

3:12b.2CO.003.012 Kwa vile hili ndilo tumaini letu, sisi twasema kwa uhodari mkuu.

3:13b.2CO.003.013 Sisi hatufanyi kama Mose ambaye alilazimika kuufunika uso wake kwa kitambaa ili watu wa Israeli wasiuone ule mwisho wa mng'ao uliokuwa unafifia.

3:14b.2CO.003.014 Lakini akili zao zilipumbazwa. Mpaka leo hii lisomwapo Agano la Kale, kifuniko hicho bado kipo. Kifuniko hicho kitaondolewa tu mtu anapoungana na Kristo.

3:15b.2CO.003.015 Naam, mpaka hivi leo kila isomwapo Sheria ya Mose akili zao huwa zimefunikwa.

3:16b.2CO.003.016 Lakini, wakati mtu amgeukiapo Bwana, kifuniko hicho huondolewa.

3:17b.2CO.003.017 Hapa "Bwana" ni Roho; na pale alipo Roho wa Bwana ndipo ulipo uhuru.

3:18b.2CO.003.018 Basi, sisi sote ambao nyuso zetu hazikufunikwa, twaonyesha kama katika kioo, utukufu wa Bwana; tunabadilishwa tufanane zaidi na huo mfano wake kwa utukufu mwingi zaidi. Hiyo ni kazi yake Roho wa Bwana.

4

4:1b.2CO.004.001 Basi, Mungu, kwa huruma yake, ametukabidhi kazi hii na hivyo hatufi moyo.

4:2b.2CO.004.002 Tumeyaacha kabisa mambo yote ya aibu na ya kisirisiri. Hatuishi tena kwa udanganyifu, wala kwa kulipotosha neno la Mungu; bali tunaudhihirisha ukweli kwa kuufanya ukweli, na hivyo kujiweka chini ya uamuzi wa dhamiri za watu mbele ya Mungu.

4:3b.2CO.004.003 Maana, kama Habari Njema tunayohubiri imefichika, imefichika tu kwa wale wanaopotea.

4:4b.2CO.004.004 Hao hawaamini kwa sababu yule mungu wa ulimwengu huu amezitia giza akili zao wasipate kuuona wazi mwanga wa Habari Njema ya utukufu wa Kristo, ambaye ni mfano kamili wa Mungu.

4:5b.2CO.004.005 Maana hatujitangazi sisi wenyewe, ila tunamhubiri Yesu Kristo aliye Bwana, sisi wenyewe tukiwa watumishi wenu kwa ajili ya Yesu.

4:6b.2CO.004.006 Mungu ambaye alisema, "Mwanga na uangaze kutoka gizani," ndiye mwenye kuiangaza mioyo yetu, na kutupatia mwanga wa ujuzi wa utukufu wa Mungu uangazao katika uso wa Kristo.

4:7b.2CO.004.007 Basi, sisi tulio na hazina hii tuko tu kama vyombo vya udongo, ili ionekane wazi kwamba nguvu hiyo kuu yatoka kwa Mungu wala si kwetu sisi wenyewe.

4:8b.2CO.004.008 Daima twapata taabu, lakini hatugandamizwi; twapata mashaka, lakini hatukati tamaa;

4:9b.2CO.004.009 twateseka, lakini hatuachwi bila msaada; na ingawa tumeangushwa chini, hatukuangamizwa.

4:10b.2CO.004.010 Kila wakati tumekuwa tukichukua mwilini mwetu kifo cha Kristo, ili uhai wake Yesu pia udhihirike katika miili yetu.

4:11b.2CO.004.011 Naam, katika maisha yetu yote tunakabiliwa na kifo daima kwa ajili ya Yesu, ili uzima wake Yesu udhihirike katika miili yetu inayokufa.

4:12b.2CO.004.012 Hii ina maana kwamba ndani yetu kifo kinafanya kazi, lakini ndani yenu uhai unafanya kazi.

4:13b.2CO.004.013 Maandiko Matakatifu yasema: "Niliamini, ndiyo maana nilinena." Nasi pia, tukiwa na moyo huohuo wa imani, tunaamini, na kwa sababu hiyo twanena.

4:14b.2CO.004.014 Tunajua kwamba yule aliyemfufua Bwana Yesu atatufufua sisi pia pamoja na Yesu na kutuweka mbele yake pamoja nanyi.

4:15b.2CO.004.015 Yote haya ni kwa faida yenu; ili kama vile neema ya Mungu inavyoenea kwa watu wengi zaidi na zaidi vivyo hivyo watu wengi zaidi watoe shukrani nyingi kwa utukufu wa Mungu.

4:16b.2CO.004.016 Kwa sababu hiyo hatufi moyo; na hata kama maumbile yetu ya nje yataoza, lakini kwa ndani tunafanywa wapya siku kwa siku.

4:17b.2CO.004.017 Taabu tunayopata ni kidogo, tena ya muda tu: lakini itatupatia utukufu upitao matazamio yote, utukufu ambao hauna mwisho.

4:18b.2CO.004.018 Hivyo tunatazamia kwa makini si vitu vinavyoonekana, bali visivyoonekana. Maana vinavyoonekana ni vya muda tu; lakini vile visivyoonekana ni vya milele.

5

5:1b.2CO.005.001 Maana tunajua kwamba hema hii ambayo ndani yake tunaishi sasa hapa duniani, yaani mwili wetu, itakapong'olewa, Mungu atatupa makao mengine mbinguni, nyumba ya milele isiyotengenezwa kwa mikono.

5:2b.2CO.005.002 Na sasa, katika hali hii, tunaugua, tukitazamia kwa hamu kubwa kuvikwa makao yetu yaliyo mbinguni.

5:3b.2CO.005.003 Naam, tunapaswa kuvikwa namna hiyo ili tusije tukasimama mbele ya Mungu bila vazi.

5:4b.2CO.005.004 Tukiwa bado katika hema hii ya duniani, tunalia kwa kukandamizwa; si kwamba tunataka kuuvua mwili huu wa kufa, ila tuna hamu ya kuvalishwa ule usiokufa, ili kile chenye kufa kimezwe kabisa na uhai.

5:5b.2CO.005.005 Mungu mwenyewe alitutayarishia mabadiliko hayo, naye ametupa Roho wake awe dhamana ya yote aliyotuwekea.

5:6b.2CO.005.006 Tuko imara daima. Tunajua kwamba kuishi katika mwili huu tu ni kukaa mbali na Bwana.

5:7b.2CO.005.007 Maana tunaishi kwa imani, na si kwa kuona.

5:8b.2CO.005.008 Lakini tuko imara na tungependelea hata kuyahama makao haya, tukahamie kwa Bwana.

5:9b.2CO.005.009 Lakini jambo la maana zaidi, tunataka kumpendeza, iwe tunaishi hapa duniani au huko.

5:10b.2CO.005.010 Maana sote ni lazima tusimame mbele ya kiti cha hukumu cha Kristo, ili kila mmoja apokee anayostahili kwa matendo aliyoyafanya wakati alipokuwa anaishi duniani, mema au mabaya.

5:11b.2CO.005.011 Basi, sisi tunajua umuhimu wa kumcha Bwana, na hivyo tunajitahidi kuwavuta watu. Mungu anatujua waziwazi, nami natumaini kwamba nanyi pia mnatujua kinaganaga.

5:12b.2CO.005.012 Si kwamba tunajaribu tena kujipendekeza kwenu, ila tunataka kuwapa ninyi sababu zetu za kuona fahari juu yenu, ili mpate kuwajibu wale wanaojivunia hali yao ya nje zaidi kuliko jinsi walivyo moyoni.

5:13b.2CO.005.013 Ikiwa tumeonekana kuwa wendawazimu, hiyo ni kwa ajili ya Mungu; na ikiwa tunazo akili zetu timamu, hiyo ni kwa faida yenu.

5:14b.2CO.005.014 Maana mapendo ya Kristo yanatumiliki sisi ambao tunatambua ya kwamba mtu mmoja tu amekufa kwa ajili ya wote, na hiyo ina maana kwamba wote wanashiriki kifo chake.

5:15b.2CO.005.015 Alikufa kwa ajili ya watu wote, ili wanaoishi wasiishi kwa ajili yao wenyewe, bali kwa ajili yake yeye aliyekufa, akafufuliwa kwa ajili yao.

5:16b.2CO.005.016 Basi, tangu sasa, sisi hatumpimi mtu yeyote kibinadamu. Hata kama kwa wakati mmoja tulimpima Kristo kibinadamu, sasa si hivyo tena.

5:17b.2CO.005.017 Mtu yeyote akiungana na Kristo huwa kiumbe kipya, mambo ya kale yamepita, hali mpya imefika.

5:18b.2CO.005.018 Yote ni kazi ya Mungu mwenye kutupatanisha sisi naye kwa njia ya Kristo, akatupa nasi jukumu la kuwapatanisha watu naye.

5:19b.2CO.005.019 Ndiyo kusema: Mungu, amekuwa akiupatanisha ulimwengu naye kwa njia ya Kristo, bila kutia maanani dhambi zao binadamu. Yeye ametupa ujumbe kuhusu kuwapatanisha watu naye.

5:20b.2CO.005.020 Basi, sisi tunamwakilisha Kristo, naye Mungu mwenyewe anatutumia sisi kuwasihi ninyi. Tunawaombeni kwa niaba ya Kristo, mpatanishwe na Mungu.

5:21b.2CO.005.021 Kristo hakuwa na dhambi, lakini Mungu alimfanya ahusike na dhambi kwa ajili yetu, ili sisi kwa kuungana naye, tupate kuushiriki uadilifu wake Mungu.

6

6:1b.2CO.006.001 Basi, tukiwa wafanyakazi pamoja na Mungu, tunawasihi msikubali ile neema mliyopokea kutoka kwa Mungu ipotee bure.

6:2b.2CO.006.002 Mungu asema hivi: "Wakati wa kufaa nimekusikiliza, wakati wa wokovu nikakusaidia." Basi, sasa ndio wakati wa kufaa, sasa ndiyo siku ya wokovu!

6:3b.2CO.006.003 Kusudi tusiwe na lawama yoyote katika utumishi wetu, hatupendi kumwekea mtu yeyote kizuio chochote.

6:4b.2CO.006.004 Badala yake, tunajionyesha kuwa kweli watumishi wa Mungu kwa kila kitu: kwa uvumilivu mwingi wakati wa mateso, shida na taabu.

6:5b.2CO.006.005 Tumepigwa, tumetiwa gerezani na kuzomewa hadharani; tumefanya kazi tukachoka; tumekesha na kukaa bila kula.

6:6b.2CO.006.006 Tunajionyesha kuwa watumishi wa Mungu kwa usafi wa moyo, elimu, uvumilivu na wema; kwa Roho Mtakatifu, kwa upendo usio na unafiki,

6:7b.2CO.006.007 kwa ujumbe wa kweli na kwa nguvu ya Mungu. Uadilifu ndiyo silaha yetu upande wa kulia na upande wa kushoto.

6:8b.2CO.006.008 Tuko tayari kupata heshima na kudharauliwa, kulaumiwa na kusifiwa. Twadhaniwa kuwa waongo, kumbe twasema kweli;

6:9b.2CO.006.009 kama wasiojulikana, kumbe twajulikana kwa wote, kama waliokufa, lakini mwonavyo, sisi ni wazima kabisa.

6:10b.2CO.006.010 Ingawa tumeadhibiwa, hatukuuawa; ingawa tunayo huzuni, twafurahi daima; ingawa tu maskini hohehahe, lakini twatajirisha watu wengi; twaonekana kuwa watu tusio na chochote, kumbe tuna kila kitu.

6:11b.2CO.006.011 Ndugu Wakorintho, tumezungumza nanyi kwa unyofu; mioyo yetu iko wazi kabisa.

6:12b.2CO.006.012 Kama mnaona kuna kizuizi chochote kile, kizuizi hicho kiko kwenu ninyi wenyewe, na si kwa upande wetu.

6:13b.2CO.006.013 Sasa nasema nanyi kama watoto wangu, wekeni mioyo yenu wazi kama nasi tulivyofanya.

6:14b.2CO.006.014 Msiambatane na watu wasioamini. Je, wema na uovu vyapatana kweli? Mwanga na giza vyawezaje kukaa pamoja?

6:15b.2CO.006.015 Kristo anawezaje kupatana na Shetani? Muumini ana uhusiano gani na asiyeamini?

6:16b.2CO.006.016 Hekalu la Mungu lina uhusiano gani na sanamu za uongo? Maana sisi ni hekalu la Mungu aliye hai. Kama Mungu mwenyewe alivyosema: "Nitafanya makao yangu kwao, na kuishi kati yao; Nitakuwa Mungu wao, nao watakuwa watu wangu."

6:17b.2CO.006.017 Kwa hiyo Bwana asema pia: "Ondokeni kati yao, mkajitenge nao, msiguse kitu najisi, nami nitawapokea.

6:18b.2CO.006.018 Mimi nitakuwa Baba yenu, nanyi mtakuwa watoto wangu, waume kwa wake, asema Bwana Mwenye Uwezo."

7

7:1b.2CO.007.001 Basi, wapenzi wangu, tukiwa tumepewa ahadi hizi zote, na tujitakase na chochote kiwezacho kuchafua miili na roho zetu, tuwe watakatifu kabisa, na tuishi kwa kumcha Mungu.

7:2b.2CO.007.002 Tunaomba mtupe nafasi mioyoni mwenu! Hatujamkosea mtu yeyote, hatujamdhuru wala kumdanganya mtu yeyote.

7:3b.2CO.007.003 Sisemi mambo haya kwa ajili ya kumhukumu mtu; maana, kama nilivyokwisha sema, ninyi mko mioyoni mwetu, tufe pamoja, tuishi pamoja.

7:4b.2CO.007.004 Nina imani kubwa sana ninaposema nanyi; naona fahari kubwa juu yenu! Katika taabu zetu nimepata kitulizo kikubwa na kufurahi mno.

7:5b.2CO.007.005 Hata baada ya kufika Makedonia hatukuweza kupumzika. Kila upande tulikabiliwa na taabu: nje ugomvi; ndani hofu.

7:6b.2CO.007.006 Lakini Mungu, mwenye kuwapa shime wanyonge alitupa moyo sisi pia kwa kuja kwake Tito.

7:7b.2CO.007.007 Si tu kwa kule kuja kwake Tito, bali pia kwa sababu ya moyo mliompa ninyi. Yeye ametuarifu jinsi mnavyotamani kuniona, jinsi mlivyo na huzuni, na mnavyotaka kunitetea. Jambo hili linanifurahisha sana.

7:8b.2CO.007.008 Maana, hata kama kwa barua ile yangu nimewahuzunisha, sioni sababu ya kujuta. Naam, naona kwamba barua hiyo iliwatia huzuni lakini kwa muda.

7:9b.2CO.007.009 Sasa nafurahi, si kwa sababu mmehuzunika, ila kwa kuwa huzuni yenu imewafanya mbadili nia zenu na kutubu. Mmehuzunishwa kadiri ya mpango wa Mungu, na kwa sababu hiyo hatukuwadhuru ninyi kwa vyovyote.

7:10b.2CO.007.010 Kuwa na huzuni jinsi atakavyo Mungu, husababisha badiliko la moyo, badiliko lenye kuleta wokovu; hivyo hakuna sababu ya kujuta. Lakini huzuni ya kidunia huleta kifo.

7:11b.2CO.007.011 Sasa mnaweza kuona matokeo ya kuona huzuni jinsi Mungu atakavyo: ninyi mmepata kuwa sasa watu wenye jitihada, wenye hoja, mnashtuka na kuogopa, mna bidii na mko tayari kuona kwamba haki yatekelezwa. Ninyi mmethibitisha kwa kila njia kwamba hamna hatia kuhusu jambo hili.

7:12b.2CO.007.012 Hivyo, ingawa niliandika ile barua, haikuwa kwa ajili ya yule aliyekosa, au kwa ajili ya yule aliyekosewa. Niliandika kusudi ionekane wazi mbele ya Mungu jinsi mlivyo na bidii kwa ajili yetu.

7:13b.2CO.007.013 Ndiyo maana sisi tulifarijika sana. Siyo kwamba tulifarijika tu, ila pia Tito alitufurahisha kwa furaha aliyokuwa nayo kutokana na jinsi mlivyomchangamsha moyo.

7:14b.2CO.007.014 Mimi nimewasifu sana mbele yake, na katika jambo hilo sikudanganyika. Tumewaambieni ukweli daima, na kule kuwasifia ninyi mbele ya Tito kumekuwa jambo la ukweli mtupu.

7:15b.2CO.007.015 Hivyo upendo wake wa moyo kwenu unaongezeka zaidi akikumbuka jinsi ninyi nyote mlivyo tayari kutii, na jinsi mlivyomkaribisha kwa hofu nyingi na kutetemeka.

7:16b.2CO.007.016 Nafurahi sana kwamba naweza kuwategemea ninyi kabisa katika kila jambo.

8

8:1b.2CO.008.001 Ndugu, tunapenda kuwapa habari juu ya neema ambazo Mungu ameyajalia makanisa ya Makedonia.

8:2b.2CO.008.002 Waumini wa huko walijaribiwa sana kwa taabu; lakini furaha yao ilikuwa kubwa hivi hata wakawa wakarimu kupita kiasi, ingawaje walikuwa maskini sana.

8:3b.2CO.008.003 Naweza kushuhudia kwamba walikuwa wakarimu kadiri ya nguvu zao na hata zaidi. Kwa hiari yao wenyewe,

8:4b.2CO.008.004 walitusihi sana wapewe nafasi ya kushiriki katika huduma hii ya kuwasaidia watu wa Mungu.

8:5b.2CO.008.005 Hilo lilikuwa jambo ambalo hatukulitazamia kabisa! Kwanza walijitolea wao wenyewe kwa Bwana, kisha wakajitolea wenyewe kwetu pia, kufuatana na mapenzi ya Mungu.

8:6b.2CO.008.006 Kwa sababu hiyo, tulimsihi Tito aliyeianza kazi hiyo awasaidieni pia muitekeleze huduma hii ya upendo miongoni mwenu.

8:7b.2CO.008.007 Ninyi mna kila kitu: imani, uwezo wa kusema, elimu; bidii yote ya kutenda mema, na upendo wenu kwetu. Hivyo, tunatazamia muwe wakarimu katika huduma hii ya upendo.

8:8b.2CO.008.008 Siwapi ninyi amri, lakini nataka tu kuonyesha jinsi wengine walivyo na bidii ya kusaidia ili nipate kujua jinsi upendo wenu ulivyo wa kweli.

8:9b.2CO.008.009 Maana, ninyi mnajua neema ya Bwana wetu Yesu Kristo: yeye, ingawa alikuwa na kila kitu, alijifanya maskini kwa ajili yenu, ili kutokana na umaskini wake, awatajirishe.

8:10b.2CO.008.010 Kuhusu jambo hili, basi, nawapeni shauri hili: inafaa kwenu kutekeleza sasa yale mliyoanza mwaka jana. Ninyi mlikuwa wa kwanza kuchukua hatua na kuamua kufanya hivyo.

8:11b.2CO.008.011 Basi, kamilisheni shughuli hiyo; na kama vile mlivyokuwa na hamu kubwa ya kusaidia, basi, fanyeni bidii vivyo hivyo, kadiri ya uwezo wenu, kuikamilisha.

8:12b.2CO.008.012 Maana ikiwa mtu ana moyo wa kusaidia, Mungu hupokea kila anachoweza kutoa: hadai zaidi.

8:13b.2CO.008.013 Ninyi hampaswi kuongezewa taabu kusudi wengine wapunguziwe mzigo wao; sivyo, ila ni lazima tujali usawa na haki.

8:14b.2CO.008.014 Kila mlicho nacho sasa cha ziada kiwasaidie wale wanaohitaji, ili nao wakati watakapokuwa na ziada, wawasaidie ninyi katika mahitaji yenu, na hivyo kuwe na usawa.

8:15b.2CO.008.015 Kama Maandiko yasemavyo: "Aliyekusanya kwa wingi hakuwa na ziada, na yule aliyekusanya kidogo hakupungukiwa."

8:16b.2CO.008.016 Namshukuru Mungu aliyeweka ndani ya moyo wa Tito hamu hiyo niliyo nayo mimi ya kuwasaidia.

8:17b.2CO.008.017 Si tu kwamba alikubali ombi letu, ila pia alikuwa na hamu kubwa ya kusaidia, hata akaamua kwa hiari yake mwenyewe kuja kwenu.

8:18b.2CO.008.018 Pamoja naye, tunamtuma ndugu mmoja ambaye sifa zake katika kueneza Habari Njema zimeenea katika makanisa yote.

8:19b.2CO.008.019 Zaidi ya hayo, yeye amechaguliwa na makanisa awe mwenzetu safarini wakati tunapopeleka huduma hii yetu ya upendo, huduma tunayoifanya kwa ajili ya utukufu wa Bwana na uthibitisho wa nia yetu njema.

8:20b.2CO.008.020 Tunataka kuepa lawama zinazoweza kutokea kuhusu usimamizi wetu juu ya zawadi hii karimu.

8:21b.2CO.008.021 Nia yetu ni kufanya vema, si tu mbele ya Bwana, lakini pia mbele ya watu.

8:22b.2CO.008.022 Basi, pamoja na ndugu hao, tumemtuma ndugu yetu mwingine ambaye mara nyingi tumempa majaribio mbalimbali, tukamwona kuwa ni mwenye hamu kubwa ya kusaidia; hata sasa amekuwa na moyo zaidi kwa sababu ana imani sana nanyi.

8:23b.2CO.008.023 Tito ni mwenzangu; tunafanya kazi pamoja kwa ajili yenu; lakini kuhusu hawa ndugu zetu wengine, wanaokuja pamoja nao, hao ni wajumbe wa makanisa, na utukufu kwa Kristo.

8:24b.2CO.008.024 Basi, waonyesheni uthabiti wa upendo wenu, makanisa yapate kuona kweli kwamba fahari ninayoona juu yenu ni ya halali.

9

9:1b.2CO.009.001 Si lazima kuandika zaidi kuhusu huduma hiyo yenu kwa ajili ya watu wa Mungu.

9:2b.2CO.009.002 Ninajua jinsi mlivyo na moyo wa kusaidia, na nilijivuna juu yenu kuhusu jambo hilo mbele ya watu wa Makedonia. Niliwaambia: "Ndugu zetu wa Akaya wako tayari tangu mwaka jana." Hivyo, moto wenu umekwisha wahimiza watu wengi zaidi.

9:3b.2CO.009.003 Basi, nimewatuma ndugu zetu hao, ili fahari yetu juu yenu ionekane kwamba si maneno matupu, na kwamba mko tayari kabisa na msaada wenu kama nilivyosema.

9:4b.2CO.009.004 Isije ikawa kwamba watu wa Makedonia watakapokuja pamoja nami tukawakuta hamko tayari, hapo sisi tutaaibika--bila kutaja aibu mtakayopata ninyi wenyewe--kwa sababu tutakuwa tumewatumainia kupita kiasi.

9:5b.2CO.009.005 Kwa hiyo, nimeona ni lazima kuwaomba hawa ndugu watutangulie kuja kwenu, wapate kuweka tayari zawadi yenu kubwa mliyoahidi; nayo ionyeshe kweli kwamba ni zawadi iliyotolewa kwa hiari na si kwa kulazimishwa.

9:6b.2CO.009.006 Kumbukeni: "Apandaye kidogo huvuna kidogo; apandaye kwa wingi huvuna kwa wingi."

9:7b.2CO.009.007 Kila mmoja, basi, na atoe kadiri alivyoamua, kwa moyo na wala si kwa huzuni au kwa kulazimishwa, maana Mungu humpenda yule mwenye kutoa kwa furaha.

9:8b.2CO.009.008 Mungu anaweza kuwapeni ninyi zaidi ya yale mnayoyahitaji, mpate daima kuwa na kila kitu mnachohitaji, na hivyo mzidi kusaidia katika kila kazi njema.

9:9b.2CO.009.009 Kama yasemavyo Maandiko Matakatifu: "Yeye hutoa kwa ukarimu, huwapa maskini, wema wahudumu milele."

9:10b.2CO.009.010 Na Mungu ampaye mkulima mbegu na mkate kwa chakula, atawapa ninyi pia mbegu mnazohitaji, na atazifanya ziote, ziwe na kuwapa mavuno mengi ya ukarimu wenu.

9:11b.2CO.009.011 Yeye atawatajirisha ninyi daima kwa kila kitu, ili watu wapate kumshukuru Mungu kwa ajili ya zawadi zenu wanazozipokea kwa mikono yetu.

9:12b.2CO.009.012 Maana huduma hii takatifu mnayoifanya si tu kwamba itasaidia mahitaji ya watu wa Mungu, bali pia itasababisha watu wengi wamshukuru Mungu.

9:13b.2CO.009.013 Kutokana na uthibitisho unaoonyeshwa kwa huduma hii yetu, watu watamtukuza Mungu kwa sababu ya uaminifu wenu kwa Habari Njema ya Kristo mnayoiungama, na pia kwa sababu ya ukarimu mnaowapa wao na watu wote.

9:14b.2CO.009.014 Kwa hiyo watawaombea ninyi kwa moyo kwa sababu ya neema ya pekee aliyowajalieni Mungu.

9:15b.2CO.009.015 Tumshukuru Mungu kwa ajili ya zawadi yake isiyo na kifani!

10

10:1b.2CO.010.001 Mimi Paulo mwenyewe ambaye naonekana kuwa mpole nikiwa pamoja nanyi, lakini mkali wakati nikiwa mbali nanyi, nawasihini kwa huruma na wema wake Kristo.

10:2b.2CO.010.002 Nawaombeni msinisababishe kuwa mkali wakati nitakapokuja, maana nina hakika naweza kuwa mkali kwa wote wale wanaotudhania kwamba tunaishi kidunia.

10:3b.2CO.010.003 Kweli tunaishi duniani, lakini hatupigani vita kidunia.

10:4b.2CO.010.004 Maana, silaha tunazotumia katika vita vyetu si silaha za kidunia, ila ni nguvu za Mungu zenye kuharibu ngome zote. Tunaharibu hoja zote za uongo,

10:5b.2CO.010.005 na kubomoa kila kizuizi cha majivuno kilichowekwa kuipinga elimu ya Mungu; tunaziteka fikira zote na kuzifanya zimtii Kristo.

10:6b.2CO.010.006 Mkisha kuwa wakamilifu katika kutii, sisi tuko tayari kuadhibu kila namna ya kutotii.

10:7b.2CO.010.007 Ninyi hutazama mambo kwa nje tu. Je, yupo mtu yeyote anayedhani kwamba yeye ni wa Kristo? Sawa! Basi, afikirie vilevile kwamba sisi pia ni wa Kristo kama yeye alivyo wa Kristo.

10:8b.2CO.010.008 Hata kama nimezidi katika kujivuna kwangu juu ya ule uwezo aliotupa--uwezo wa kuwajenga na sio wa kubomoa--hata hivyo sijutii hata kidogo.

10:9b.2CO.010.009 Sipendi mfikiri kwamba nataka kuwatisha ninyi kwa barua zangu.

10:10b.2CO.010.010 Mtu anaweza kusema: "Barua za Paulo ni kali na zenye maneno mazito, lakini yeye mwenyewe anapokuwa pamoja nasi ni mtu dhaifu, na hata anapoongea maneno yake ni kama si kitu."

10:11b.2CO.010.011 Mtu asemaye hivyo heri akumbuke kwamba hakuna tofauti ya yale tunayoandika katika barua wakati tuko mbali, na yale tutakayofanya wakati tutakapokuwa nanyi.

10:12b.2CO.010.012 Kwa vyovyote hatungethubutu kujiweka au kujilinganisha na wale watu wanaojisifia wenyewe. Watu wenye kujifanya wao kuwa kipimo cha kujipimia, na watu wanaojilinganisha wenyewe kwa wenyewe, ni wapumbavu.

10:13b.2CO.010.013 Lakini sisi hatutajivuna kupita kiasi; kujivuna huko kutabaki katika kile kipimo cha kazi aliyotukabidhi Mungu, kazi ambayo tunaifanya pia kwenu.

10:14b.2CO.010.014 Na kwa vile ninyi mu katika mipaka hiyo, hatukuipita tulipokuja kwenu, tukiwaleteeni Habari Njema juu ya Kristo.

10:15b.2CO.010.015 Basi, hatujivunii kazi waliyofanya wengine zaidi ya kipimo tulichopewa; ila tunatumaini kwamba imani yenu itazidi miongoni mwenu kufuatana na kipimo alichotuwekea Mungu.

10:16b.2CO.010.016 Hapo tutaweza kuihubiri Habari Njema katika nchi nyingine, mbali nanyi; na haitakuwa shauri la kujivunia kazi waliyofanya watu wengine mahali pengine.

10:17b.2CO.010.017 Lakini kama yasemavyo Maandiko: "Mwenye kuona fahari na aone fahari juu ya alichofanya Bwana."

10:18b.2CO.010.018 Anayekubaliwa si yule anayejisifu mwenyewe, bali yule anayesifiwa na Bwana.

11

11:1b.2CO.011.001 Laiti mngenivumilia kidogo, hata kama mimi ni mjinga kiasi fulani! Naam, nivumilieni kidogo.

11:2b.2CO.011.002 Ninawaoneeni wivu lakini ni wivu wa Mungu; maana ninyi ni kama bikira safi niliyemposa kwa mwanamume mmoja tu ambaye ndiye Kristo.

11:3b.2CO.011.003 Lakini naogopa kwamba, kama vile yule nyoka kwa hila zake za uongo alimdanganya Hawa, fikira zenu zaweza kupotoshwa, mkauacha uaminifu wenu wa kweli kwa Kristo.

11:4b.2CO.011.004 Maana mtu yeyote ajaye na kumhubiri Yesu aliye tofauti na yule tuliyemhubiri, ninyi mwampokea kwa mikono miwili; au mnakubali roho au habari njema tofauti kabisa na ile mliyopokea kutoka kwetu!

11:5b.2CO.011.005 Sidhani kwamba mimi ni mdogo kuliko hao "mitume wakuu."

11:6b.2CO.011.006 Labda sina ufasaha wa lugha, lakini elimu ninayo; jambo hili tumelionyesha wazi kwenu, kila mahali na kila wakati.

11:7b.2CO.011.007 Mimi niliihubiri kwenu Habari Njema ya Mungu bila kudai mshahara; nilijinyenyekeza ili nipate kuwakweza ninyi. Je, nilifanya vibaya?

11:8b.2CO.011.008 Nilipofanya kazi kati yenu, mahitaji yangu yaligharimiwa na makanisa mengine. Kwa namna moja au nyingine niliwapokonya wao mali yao nipate kuwatumikia ninyi.

11:9b.2CO.011.009 Nilipokuwa nanyi sikumsumbua mtu yeyote nilipohitaji fedha; ndugu waliotoka Makedonia waliniletea kila kitu nilichohitaji. Nilikuwa mwangalifu sana nisiwe mzigo kwa namna yoyote ile, na nitaendelea kufanya hivyo.

11:10b.2CO.011.010 Naahidi kwa ule ukweli wa Kristo ulio ndani yangu, kwamba hakuna kitakachoweza kunizuia kujivunia jambo hilo popote katika Akaya.

11:11b.2CO.011.011 Kwa nini nasema hivyo? Kwa sababu eti siwapendi ninyi? Mungu anajua kwamba nawapenda!

11:12b.2CO.011.012 Nitaendelea kufanya kama ninavyofanya sasa, ili nisiwape nafasi wale wanaotafuta nafasi, nafasi ya kujivuna kwamba eti wanafanya kazi kama sisi.

11:13b.2CO.011.013 Maana, hao ni mitume wa uongo, wafanyakazi wadanganyifu wanojisingizia kuwa mitume wa Kristo.

11:14b.2CO.011.014 Wala si ajabu, maana hata Shetani mwenyewe hujisingizia kuwa malaika wa mwanga!

11:15b.2CO.011.015 Kwa hiyo si jambo la kushangaza ikiwa na hao watumishi wake wanajisingizia kuwa watumishi wa haki. Mwisho wao watapata kile wanachostahili kufuatana na matendo yao.

11:16b.2CO.011.016 Tena nasema: Mtu asinifikirie kuwa mpumbavu. Lakini kama mkifikiri hivyo, basi, nichukueni kama mpumbavu ili nami nipate kuwa na cha kujivunia angaa kidogo.

11:17b.2CO.011.017 Ninachosema sasa si kile alichoniagiza Bwana; kuhusu jambo hili la kujivuna, nasema tu kama mtu mpumbavu.

11:18b.2CO.011.018 Maadam wengi hujivuna kwa sababu za kidunia, nami pia nitajivuna.

11:19b.2CO.011.019 Ninyi ni wenye busara, ndiyo maana hata mnawavumilia wapumbavu!

11:20b.2CO.011.020 Mnamvumilia hata mtu anayewafanya ninyi watumwa, mtu mwenye kuwanyonya, mwenye kuwakandamiza, mwenye kuwadharau na kuwapiga usoni!

11:21b.2CO.011.021 Kwa aibu nakubali kwamba sisi tulikuwa dhaifu. Iwe iwavyo, lakini kama kuna mtu yeyote anayethubutu kujivunia kitu--nasema kama mtu mpumbavu--mimi nathubutu pia.

11:22b.2CO.011.022 Je, wao ni Waebrania? Hata mimi. Je, wao ni Waisraeli? Hata mimi. Wao ni wazawa wa Abrahamu? Hata mimi.

11:23b.2CO.011.023 Wao ni watumishi wa Kristo? Hata mimi--nanena hayo kiwazimu--ni mtumishi wa Kristo zaidi kuliko wao. Mimi nimefanya kazi ngumu zaidi, nimekaa gerezani mara nyingi zaidi, nimepigwa mara nyingi zaidi na nimekaribia kifo mara nyingi.

11:24b.2CO.011.024 Mara tano nilichapwa vile viboko thelathini na tisa vya Wayahudi.

11:25b.2CO.011.025 Nilipigwa viboko mara tatu, nilipigwa mawe mara moja; mara tatu nilivunjikiwa meli baharini, na humo nikakesha usiku kucha na kushinda mchana kutwa.

11:26b.2CO.011.026 Kila mara safarini nimekabiliwa na hatari za mafuriko ya mito, na hatari za wanyama; hatari kutoka kwa wananchi wenzangu na kutoka kwa watu wa mataifa mengine; hatari za mjini, hatari za porini, hatari za baharini, hatari kutoka kwa ndugu wa uongo

11:27b.2CO.011.027 Nimefanya kazi na kutaabika, nimekesha bila usingizi mara nyingi; nimekuwa na njaa na kiu; mara nyingi nimefunga na kukaa katika baridi bila nguo.

11:28b.2CO.011.028 Na, licha ya mengine mengi, kila siku nakabiliwa na shughuli za makanisa yote.

11:29b.2CO.011.029 Kama mtu yeyote ni dhaifu, nami pia ni dhaifu; mtu yeyote akikwazwa, nami pia huwa na wasiwasi.

11:30b.2CO.011.030 Ikinilazimu kujivuna, basi, nitajivunia udhaifu wangu.

11:31b.2CO.011.031 Mungu na Baba wa Bwana Yesu--jina lake litukuzwe milele--yeye anajua kwamba sisemi uongo.

11:32b.2CO.011.032 Nilipokuwa Damasko, mkuu wa mkoa, aliyekuwa chini ya mfalme Areta, alikuwa akiulinda mji wa Damasko ili apate kunikamata.

11:33b.2CO.011.033 Lakini, ndani ya kapu kubwa, niliteremshwa nje kupitia katika nafasi ukutani, nikachopoka mikononi mwake.

12

12:1b.2CO.012.001 Nitajivuna basi, ingawa haifai! Lakini sasa nitasema juu ya maono na ufunuo alivyonijalia Bwana.

12:2b.2CO.012.002 Namjua mtu mmoja Mkristo, ambaye miaka kumi na minne iliyopita alinyakuliwa mpaka katika mbingu ya tatu. (Sijui kama alikuwa huko kwa mwili au kwa roho; Mungu ajua.)

12:3b.2CO.012.003 Narudia: najua kwamba mtu huyo alinyakuliwa mpaka peponi. (Lakini sijui kama alikuwa huko kwa mwili au kwa roho; Mungu ajua.)

12:4b.2CO.012.004 Huko akasikia mambo ya siri ambayo binadamu hastahili kuyatamka.

12:5b.2CO.012.005 Basi, nitajivunia juu ya mtu wa namna hiyo, na si juu yangu mimi binafsi, isipokuwa tu juu ya udhaifu wangu.

12:6b.2CO.012.006 Kama ningetaka kujivuna singekuwa mpumbavu hata kidogo, maana ningekuwa nasema ukweli mtupu. Lakini sitajivuna; sipendi mtu anifikirie zaidi ya vile anavyoona na kusikia kutoka kwangu.

12:7b.2CO.012.007 Lakini, kusudi mambo haya makuu niliyofunuliwa yasinifanye nilewe majivuno, nilipewa maumivu mwilini kama mwiba, mjumbe wa Shetani mwenye kunipiga nisijivune kupita kiasi.

12:8b.2CO.012.008 Nilimsihi Bwana mara tatu kuhusu jambo hili ili linitoke.

12:9b.2CO.012.009 Lakini akaniambia: "Neema yangu inatosha kwa ajili yako; maana uwezo wangu hukamilishwa zaidi katika udhaifu." Basi, ni radhi kabisa kujivunia udhaifu wangu ili uwezo wake Kristo ukae juu yangu.

12:10b.2CO.012.010 Kwa hiyo nakubali kwa radhi udhaifu, madharau, taabu, udhalimu na mateso, kwa ajili ya Kristo; maana ninapokuwa dhaifu, ndipo ninapokuwa na nguvu.

12:11b.2CO.012.011 Nimekuwa kama mpumbavu, lakini, ninyi mmenilazimisha kuwa hivyo. Ninyi ndio mngalipaswa kunisifu. Maana, ingawa mimi si kitu, kwa vyovyote, mimi si mdogo zaidi kuliko hao "mitume wakuu."

12:12b.2CO.012.012 Miujiza na maajabu yaonyeshayo wazi kwamba mimi ni mtume yalifanyika miongoni mwenu kwa uvumilivu wote.

12:13b.2CO.012.013 Je, mlipungukiwa nini zaidi kuliko makanisa mengine, isipokuwa tu kwamba mimi kwa upande wangu sikuwasumbueni kupata msaada wenu? Samahani kwa kuwakoseeni haki hiyo!

12:14b.2CO.012.014 Sasa niko tayari kabisa kuja kwenu mara ya tatu, na sitawasumbua. Maana ninachotafuta si mali zenu, bali ni ninyi wenyewe. Ni kawaida ya wazazi kuwawekea watoto wao akiba, na si watoto kuwawekea wazazi wao.

12:15b.2CO.012.015 Mimi ni radhi kabisa kutumia nilicho nacho, na hata kujitolea mimi mwenyewe kabisa, kwa faida ya roho zenu. Je, mtanipenda kidogo ati kwa kuwa mimi nawapenda ninyi mno?

12:16b.2CO.012.016 Basi, mtakubali kwamba sikuwa mzigo kwenu. Lakini labda mtu mwingine atasema: "Kwa vile Paulo ni mwerevu, amewafanyieni ulaghai."

12:17b.2CO.012.017 Je, mimi niliwanyonyeni kwa njia ya mjumbe yeyote niliyemtuma kwenu?

12:18b.2CO.012.018 Mimi nilimwita Tito, nikamtuma kwenu na ndugu yetu mwingine. Je, Tito aliwanyonyeni? Je, hamjui kwamba sisi tumekuwa tukiongozwa na roho yuleyule, na mwenendo wetu ni mmoja?

12:19b.2CO.012.019 Labda mnafikiri kwamba mpaka sasa tumekuwa tukijitetea wenyewe mbele yenu! Lakini, tunasema mambo haya mbele ya Mungu, tukiwa tumeungana na Kristo. Mambo hayo, yote, wapenzi wangu, ni kwa ajili ya kuwajenga ninyi.

12:20b.2CO.012.020 Naogopa, huenda nitakapokuja kwenu nitawakuta katika hali nisiyopenda, nami itanilazimu kuwa katika hali msiyoipenda. Naogopa huenda kukawa na ugomvi, wivu, uhasama, ubishi, masengenyano, kunong'ona, majivuno na fujo kati yenu.

12:21b.2CO.012.021 Naogopa huenda hapo nitakapokuja safari ijayo Mungu wangu atanifanya niaibike mbele yenu, nami nitaomboleza kwa ajili ya wengi wa wale waliotenda dhambi lakini hawakujutia huo uchafu, tamaa zao mbaya na uzinzi waliokuwa wamefanya.

13

13:1b.2CO.013.001 Hii ni mara yangu ya tatu kuja kwenu. "Kila tatizo litatatuliwa kwa ushahidi wa watu wawili au watatu," yasema Maandiko.

13:2b.2CO.013.002 Nilikwisha sema, na kama ilivyokuwa safari ya pili, sasa nasema tena nikiwa mbali: wale wote waliotenda uovu bila kutubu, na pia wale wengine, nitakapokuja, watakiona cha mtema kuni.

13:3b.2CO.013.003 Mtajionea wenyewe kwamba Kristo anasema ndani yangu. Kwenu Kristo si dhaifu; bali nguvu yake yafanya kazi miongoni mwenu.

13:4b.2CO.013.004 Maana hata kama alisulubiwa kwa sababu ya udhaifu, lakini sasa anaishi kwa uwezo wa Mungu. Sisi pia tu dhaifu kwa kuungana naye lakini tutaishi naye kwa uwezo wa Mungu kwa ajili yenu.

13:5b.2CO.013.005 Jichunguzeni ninyi wenyewe mpate kujua kama kweli mnayo imani. Jichunguzeni ninyi wenyewe. Je, hamjui kwamba Kristo Yesu yumo ndani yenu? Kama sivyo, basi ninyi mmeshindwa.

13:6b.2CO.013.006 Lakini natumaini kwamba ninyi mnajua kuwa sisi hatukushindwa.

13:7b.2CO.013.007 Tunamwomba Mungu msifanye uovu wowote, lakini si kusudi tuonekane kama watu waliokwisha faulu, bali mpate kutenda mema, hata kama sisi tunaonekana kuwa tumeshindwa.

13:8b.2CO.013.008 Maana hatuwezi kuupinga ukweli; uwezo tulio nao ni wa kuuendeleza ukweli.

13:9b.2CO.013.009 Tunafurahi kwamba sisi tu dhaifu, lakini ninyi mna nguvu; kwa hiyo tunaomba mpate kuwa wakamilifu.

13:10b.2CO.013.010 Basi, ninaandika barua hii nikiwa mbali, ili nitakapofika kwenu nisilazimike kuwa mkali kwenu kwa kutumia ule uwezo alionipa Bwana; naam, uwezo wa kujenga na si wa kubomoa.

13:11b.2CO.013.011 Kwa sasa, ndugu, kwaherini! Muwe na ukamilifu, shikeni mashauri yangu, muwe na nia moja; kaeni kwa amani. Naye Mungu wa mapendo na amani atakuwa pamoja nanyi.

13:12b.2CO.013.012 Salimianeni kwa ishara ya upendo.

13:13b.2CO.013.013 (G13-12) Watu wote wa Mungu huku wanawasalimuni.

13:14b.2CO.013.014 (G13-13) Neema ya Bwana Yesu Kristo na upendo wa Mungu na umoja wa Roho Mtakatifu, viwe nanyi nyote.


Holder of rights
Multilingual Bible Corpus

Citation Suggestion for this Object
TextGrid Repository (2025). Swahili Collection. 2 Corinthians (Swahili). 2 Corinthians (Swahili). Multilingual Parallel Bible Corpus. Multilingual Bible Corpus. https://hdl.handle.net/21.11113/0000-0016-B987-F